WIZARA ya Elimu, Sayansi na Ufundi imetoa waraka wa elimu kuhusu elimumsingi bila malipo na kutoa orodha ya shule za msingi 11 za Serikali ambazo hazihusiki na utoaji wa elimu bure uliotangazwa na Rais John Magufuli.
Elimumsingi inajumuisha elimu ya awali, ya msingi na sekondari ambayo itaanza Januari mwakani.
Katika
Waraka Elimu Namba 6 wa Mwaka 2015 kuhusu utekelezaji wa elimu bure kwa
shule za msingi na sekondari, wizara hiyo imetaja shule hizo kuwa ni
Shule ya Msingi Olympio (Dar es Salaam); Shule ya Msingi Diamond (Dar es
Salaam); Shule ya Msingi Oysterbay (Dar es Salaam); Shule ya Msingi
Iringa (Iringa) na Shule ya Msingi Mkapa (Mbeya).
Nyingine
ni Shule ya Msingi Angaza (Mbeya); Shule ya Msingi Nuru (Mbeya); Shule
ya Msingi Lupilisi (Ruvuma); Shule ya Msingi Tanga (Tanga); Shule ya
Msingi Arusha (Arusha) na Shule ya Msingi Kisimani iliyoko mkoani
Arusha.
Wizara
hiyo pia imesema waraka huo hauzihusu shule zinazomilikiwa na mashirika
ya umma ama taasisi za umma ambazo zinaendeshwa kwa taratibu sawa na
shule za binafsi.
Katika
waraka huo, wizara hiyo imetoa majukumu yanayotakiwa kufanywa na Wizara
hiyo, Tamisemi, wakurugenzi wa manispaa na halmashauri ya wilaya, wakuu
wa shule, bodi za shule, wazazi na wananchi.
Majukumu ya wazazi na walezi
Kuanzia
Januari, wazazi wanatakiwa tu kununua sare za shule na michezo, vifaa
vya kujifunzia vikiwemo madaftari na kalamu, na chakula kwa wanafunzi wa
kutwa na kugharimia matibabu kwa watoto wao.
Wanatakiwa
pia kulipia nauli ya kwenda shule na kurudi kwa wanafunzi wa kutwa na
wanafunzi wa bweni wakati wa likizo; kununua magodoro, shuka, vifaa vya
usafi binafsi kwa wanafunzi wanaosoma shule za bweni na wanaoishi katika
hosteli zinazotumiwa na serikali; na kukemea na kutoa taarifa kuhusu
mienendo inayokwenda kinyume na elimumsingi bila malipo.
Wazazi
na wananchi wengine pia wanatakiwa kuendelea kujitolea nguvukazi na
mali ili kuleta ustawi na maendeleo ya shule zilizoko ndani ya jamii.
Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi
Katika
waraka huo, Wizara ina jukumu la kutenga fedha za kugharimia
utayarishaji na uendeshaji wa mitihani ya kitaifa kulingana na idadi ya
wanafunzi; kutenga fedha kwa ajili ya Uthibiti Ubora wa Shule na kutenga
fedha za kufanya ufuatiliaji na tathmini ya utoaji wa elimumsingi bila
malipo na kuchukua hatua stahiki pale inapobidi.
Inachotakiwa
kufanya Tamisemi Kwa upande wa Tamisemi, waraka huo unaielekeza wizara
hiyo kutoa miongozo ya matumizi ya fedha za umma kwa wakuu wa shule,
kuratibu uandaaji wa mipango na bajeti ili kupata mipango na bajeti ya
taifa kila mwaka inayozingatia mahitaji halisi ya elimumsingi bila
malipo.
Pia
Tamisemi inatakiwa kufanya ukaguzi wa ndani, ufuatiliaji na tathmini za
mara kwa mara ili kuhakikisha elimumsingi bila malipo inatolewa kwa
ufanisi na viwango vya ubora inavyostahili.
Kuratibu
utoaji mipango na bajeti za ruzuku ya uendeshaji wa shule ikiwemo
ulinzi, umeme, maji na ununuzi wa chaki na karatasi pamoja na vifaa
vingine vya kufundishia na kujifunzia.
Kutenga
na kutuma fedha shuleni kwa ajili ya uendeshaji na usimamizi wa
mitihani na majaribio mbalimbali shuleni ikiwemo tathmini endelezi,
kununua vitabu, kemikali na vifaa vya maabara, samani yakiwemo madawati,
vifaa vya michezo, matengenezo ya mashine na mitambo pamoja na kujenga
na kukarabati miundombinu ya shule.
Kutenga
na kutuma fedha shuleni za kugharimia wanafunzi wenye mahitaji maalumu
waliopo kwenye shule na vitengo vya elimu maalumu kwa kuwapatia chakula
yaani mlo mmoja kwa wanafunzi wa kutwa na milo mitatu kwa wanafunzi wa
bweni pamoja na vifaa na visaidizi.
Wakuu wa shule
Waraka
huo unawataka wakuu wa shule kuwapa maelekezo wazazi kuhusu aina ya
vifaa vinavyohitajika mfano rangi ya kitambaa cha sare ya shule, sare za
michezo, idadi na aina ya madaftari watakayotumia wanafunzi ili wazazi
wanunue wenyewe.
Pia
wanatakiwa kusimamia na kuhakikisha fedha inayotolewa na Serikali
inatumika kama ilivyokusudiwa kulingana na taratibu za fedha za Serikali
na kutoa takwimu na taarifa sahihi za idadi ya wanafunzi na mahitaji
mengine ya shule.
Kamati au Bodi za Shule
Wizara
katika waraka huo inataka kamati za shule kufuatilia na kusimamia
matumizi ya fedha zinazotolewa na Serikali ili ziweze kuleta tija;
kuhakikisha kuwa sera, nyaraka, maelekezo na miongozo ya Serikali
inazingatiwa na kutoa ushauri stahiki.
Kuwashirikisha
wazazi, walezi, walimu na wanafunzi katika maamuzi na maazimio ya
masuala mbalimbali yanayohusu maslahi na maendeleo ya shule kwa ujumla.
Pia
waraka huo umeainisha majukumu ya walimu ambao kazi yao kubwa ni
kusimamia sera na miongozo ya utoaji wa elimu bure. Wanafunzi ambao ndio
walengwa wakuu wa utoaji wa elimu pia wametakiwa kuhakikisha wanakuwepo
shule katika kipindi chote cha masomo.
No comments:
Post a Comment