MAMLAKA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta), imebuni kifaa cha kudhibiti wizi wa magari na pikipiki za abiria maarufu bodaboda, kwa kutumia simu.
Kwa
kutumia kifaa hicho, dereva atakuwa na uwezo wa kuzima pikipiki au gari
kwa kutumia simu ya mkononi, ambayo namba yake itakuwa imefungwa katika
chombo hicho cha usafiri.
Akizungumzia
kifaa hicho, Mwalimu wa Teknolojia ya Mawasiliano wa Veta, Valerian
Sanga alisema alishirikiana na mwalimu mwenzake wa chuo hicho
anayefundisha masuala ya umeme, Christian Brighton kubuni kifaa hicho
kilichowachukua miaka miwili kukamilika.
“Wiki
tatu zilizopita ndio tumekamilisha kifaa hiki na kuanza kufanya kazi,
tukafunga kwenye pikipiki hii (akionesha) kupima na kuonesha watu namna
ya kuweka ulinzi kwenye vifaa vyao kwa kuwa mifumo kama hii, inauzwa
katika kampuni za nje lakini ni gharama sana,” alisema.
Mwalimu huyo anatoka Kituo cha Veta Kipawa jijini Dar es Salaam, ambacho kilibuni mfumo huo ili kudhibiti wizi wa pikipiki.
Ubunifu
huo ulichangia mamlaka hiyo, kupata tuzo ya mshindi wa jumla wa
Maonesho ya Kimataifa ya 40 Dar es Salaam, yanayoendelea katika viwanja
vya Mwalimu Julius Nyerere.
Sanga alisema kifaa hicho kina GPS na kinatumia mawasiliano ya simu kwa kutumia GSM, itakayo saidia kujua sehemu pikipiki au gari lilipo, lakini pia kikimwezesha mmiliki kuzima na kuwasha usafiri wake popote ulipo.
Sanga alisema kifaa hicho kina GPS na kinatumia mawasiliano ya simu kwa kutumia GSM, itakayo saidia kujua sehemu pikipiki au gari lilipo, lakini pia kikimwezesha mmiliki kuzima na kuwasha usafiri wake popote ulipo.
“Unatumia
simu ya mkononi ambayo namba zako zinakuwa zimefungwa katika chombo cha
usafiri, ili zikuwezeshe kuzima kama kimeibiwa ambapo baada ya dakika
tano kitazima na hakitawaka mpaka utume tena ujumbe wa kutaka iwake,” alisema.
Sanga
alisema kwa sasa wanafunga kifaa hicho kwa gharama ya Sh 400,000,
lakini anatarajia baadaye watakapopata oda nyingi, watapunguza bei kwani
kwa siku nne tangu kuanza maonesho hayo wameshapata watu wengi
wanaohitaji.
“Tunategemea
kupata watu wengi wanohitaji na tayari watu wawili; mmoja ana pikipiki
ishirini na mwingine kumi, wametaka tuwafungie huku tukiamini mpaka
maonesho yaishe tutapata wengi zaidi,”alisema.
Alisema
ili kukidhi mahitaji hayo, wamekuwa wakifundisha wanafunzi wa chuo
hicho ili washirikiane katika kutengeneza vifaa hivyo kwa wingi ikiwa
watajitokeza wengi wanaozihitaji.
Baadhi
ya watu waliotembelea kuona pikipiki hiyo, walishangazwa na utaalamu
huo kufanyika nchini na kutaka serikali kusaidia, hususani wakati huu wa
taifa linapojiandaa kwa uchumi wa viwanda.
Mmoja
wa wananchi hao, Godwin Mlulu alisema kifaa hicho kimekuja wakati
muafaka kutokana na kukithiri kwa wizi wa pikipiki. Lakini alipendekeza
bei ipunguzwe, kwa kuwa wamiliki wengi wa pikipiki za biashara, ni wenye
kipato cha chini.
No comments:
Post a Comment