Nape: Nitaanza Kushughulikia Sheria na Nidhamu Michezoni - LEKULE

Breaking

14 Dec 2015

Nape: Nitaanza Kushughulikia Sheria na Nidhamu Michezoni


Waziri wa Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo, Nape Nnauye ameahidi kushughulikia sheria mbalimbali zinazosimamia sekta hiyo ili kuongeza nidhamu michezoni.

Nape aliyeapishwa juzi kuanza kibarua hicho, ataiongoza wizara hiyo iliyokuwa ikiongozwa na Dk Fenella Mukangara, huku ndoto za Watanzania zikiwa ni kuona kiwango cha michezo kilichoporomoka, kinakua.

Akizungumza na mwandishi wetu jana alisema utovu wa nidhamu kwa baadhi ya viongozi na wachezaji umekuwa ukiitafuna sekta hiyo kwa kiwango kikubwa na kusababisha kushuka kwa michezo.

Alisema zipo baadhi ya sheria zinazohitaji marekebisho ili ziwe na tija na kwamba ana uhakika kuwa zitasaidia kurejesha thamani ya michezo, ikiwamo soka na sanaa.

“Michezo ikisonga mbele na timu zetu zikifanya vizuri tutavutia wawekezaji wengi kwenye sekta hii kwa sababu suala siyo kufurahi, tunatakiwa tuichukulie sekta hii muhimu kama sehemu ya kuzalisha ajira na kukuza uchumi wa Taifa letu na mtu binafsi,” alisema Nnauye na kuongeza:


“Ni kweli kwamba kiwango cha michezo nchini kipo chini na maeneo ya mwanzo ya ninayodhani yanapaswa kushughulikiwa ni kwenye sheria. Natamani kuona tunakuwa na sheria zenye tija, zitakazosaidia kumaliza utovu wa nidhamu unaoitafuna sekta hii,” alisema.

No comments: