Makonda Apiga Marufuku Kuvuta Sigara Hadharani......Pia Kapiga Marufuku Kuvuta Shisha - LEKULE

Breaking

3 Jul 2016

Makonda Apiga Marufuku Kuvuta Sigara Hadharani......Pia Kapiga Marufuku Kuvuta Shisha

Baada ya kutangaza vita dhidi ya mashoga juzi, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda jana alitangaza vita nyingine; hataki uvutaji shisha akisema inachanganywa na vilevi vinavyoharibu vijana. 

Makonda, ambaye alikuwa akihutubia Tamasha la Vijana lililoandaliwa na Upendo Media Group kwenye Uwanja wa Taifa aliagiza wavuta shisha hadharani, sigara na mashoga wakamatwe ndani ya siku saba. 
“Ni marufuku biashara ya shisha kwenye mkoa wangu. Wanaofanya bishara hiyo wote nitawakamata. Mimi ndiye mbabe wa vita,” alisema Makonda na kuongeza: “Nina imani watakuwa wamefungasha virago vyao iwe ni kwenye klabu au baa maana humo wanachanganya vitu vingi; bangi na vilevi ambavyo vina madhara.” 
Alisema vijana wa vyuo na sekondari ndiyo waathirika wakubwa wa kilevi hicho, ambacho huvutwa kwa njia ya bomba la mpira linalotoka kwenye jiko maalumu ambalo tumbaku huunguzwa na kutoa moshi. 

“Baada ya siku saba tutakutana (Gereza la Segerea),” alisema. 
“Kwa utafiti nilioufanya chini ya TFDA, shisha ina madhara makubwa kwa wanaoivuta na wasiovuta. Inasababisha kansa ya mapafu na koo. 

“Na pia inasababisha utegemezi ambapo mtu bila kuvuta hawezi kuona maisha, lakini pia inapunguza uwezo wa kufikiri na inamaliza nguvu kazi katika taifa,” aliongeza. 
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), kiwango cha shisha inayovutwa kwa saa moja, ni sawa na kuvuta sigara kati ya 100 na 200. 

Utafiti wa shirika hilo unaonyesha kuwa mvuta sigara wa kawaida huingiza nusu lita ya moshi kwa kila sigara, lakini mvuta shisha ni zaidi ya hivyo. 
Kuhusu uvutaji wa sigara, Makonda alisema ndani ya siku saba zijazo ni marufuku kuvuta sigara hadharani na kila anayehitaji kufanya hivyo atapaswa kutafuta sehemu iliyojitenga ili akate kiu yake. 
“Kila anayevuta sigara, atapaswa kuvuta sehemu ambayo hatawabughudhi wenzake. 

"Tumechoka kupanda magari na watu wanaovuta sigara, kukaa hoteli na watu wa aina hiyo. Sasa mvutaji anapaswa kuvuta sehemu ya peke yake, na sio kwenye jumuiko la watu. Madhara ni makubwa kwa tusiovuta kuliko wanaovuta,” alisema. 
Maagizo ya Makonda yanakuja ikiwa ni wiki moja tangu apige marufuku abiria na dereva wa bodaboda kusafiria chombo hicho bila ya kuvaa kofia ngumu. 
Alisema kupanda pikipiki bila kofia hiyo ni dhamira ya kutaka kujiua kwa sababu dereva na abiria wakipata ajali ni rahisi zaidi kupoteza maisha iwapo kichwa kitajipiga ardhini. 
“Nimewasiliana na kamati yangu ya usalama barabarani ya mkoa. Hili nitalisimamia kikamilifu lazima wote wavae helmet na wakikamatwa wote watashtakiwa,” alisema. 
Mapema mwaka huu, mara baada ya kuteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa, Makonda alitoa maagizo matatu yanayohusu ombaomba wa barabarani kuondoka na kubomolewa kwa majengo makubwa yaliyojengwa kinyume na taratibu na yasiyo na maegesho.

Agizo la tatu la Makonda lilikuwa ni wamiliki wa baa kutopiga muziki nje ya utaratibu wa vibali vyao. 
Makonda pia alirudia wito wake wa kutaka watu wanaojishughulisha na biashara ya ushoga wakamatwe mara moja. 
Alisema miaka michache iliyopita Taifa lilikataa msaada wenye sharti la ushoga, lakini inashangaza kuwa bado zipo taasisi zisizo za kiserikali zilizoundwa kwa ajili ya kutoa misaada kwa watu wanaojihusisha na vitendo hivyo.

 “Nimefanya mazungumzo na  Waziri wa Katiba na Sheria. Hatutaki hili liendelee kwa sababu hiyo naiagiza TCRA kuwa wapo watu wanaojitangaza kwenye instagram na vyombo vya habari kwamba wao ni mashoga, wakamatwe haraka iwezekanavyo na kama kuna shoga ana akaunti kwenye mitandao ya kijamii na wale wafuasi wake wote ni watuhumiwa sawasawa na mhusika,” alisema. 
Ushoga, ambao ni uhusiano wa mapenzi wa watu wa jinsia moja, ni marufuku nchini, kwa mujibu wa Sheria ya Adhabu. 

Kwa mujibu wa Sura ya 16, sehemu ya 154, mtu anayejihusisha na ngono na mtu mwingine kinyume na maumbile au anayemruhusu mtu mwingine kufanya naye ngono kinyume na maumbile, atakuwa amefanya kosa la jinai na kustahili kifungo cha miaka 14 jela. 

No comments: