Dodoma/Dar.
Rais Jakaya Kikwete amesema idadi ya wanachama wa CCM waliojitokeza kuwania urais ni kubwa, hivyo ni lazima wawape viongozi muda wa kuwachuja lakini akawataka wasiwanunie baada ya kufanya uamuzi.
Rais Jakaya Kikwete amesema idadi ya wanachama wa CCM waliojitokeza kuwania urais ni kubwa, hivyo ni lazima wawape viongozi muda wa kuwachuja lakini akawataka wasiwanunie baada ya kufanya uamuzi.
Rais Kikwete alisema hayo jana
katika hotuba yake ya kuvunja Bunge ambayo iliibua waziwazi ushabiki
kwa wagombea, hasa baada ya kumtaja aliyekuwa waziri mkuu wake wa
kwanza, Edward Lowassa kwa ajili ya kumshukuru.
Akitoa salamu zake kwa wagombea hao, Rais Kikwete aliwapongeza na kuwatakia mafanikio mema katika safari yao.
“Wale
wanaogombea urais waliomo humu (bungeni) nawatakia kila la kheri na
nawashukuru kwa kuonyesha nia ya kunipokea mzigo huu mzito. Nawatakiwa
heri katika matamanio yenu,” alisema Rais Kikwete ambaye aliingia Ikulu
mwaka 2005.
“Mko wengi, wote ni vigogo na mmetupa kazi kama kamati kuwachuja kwa hiyo msitununie tukifanya maamuzi.”
Lowassa afunika
Wakati
akihitimisha hotuba hiyo, Rais aliwashukuru watu mbalimbali waliofanya
kazi kwenye Serikali yake, lakini hali ilikuwa tofauti alipomtaja
Lowassa ambaye alifanya naye kazi kwa miaka miwili.
Alimshukuru pia, Makamu wake, Dk Mohamed Gharib Bilal, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na baadaye wabunge na viongozi wengine.
Alianza
kwa kuwashukuru huku akiwataja majina. Kila alipotaja majina ya
viongozi hao, wabunge walipiga makofi kwa kugonga meza zao. Hata
alipomtaja Dk Bilal na Pinda, wabunge hao walishangilia kwa kawaida.
Hata
hivyo, alipofikia kutaja jina la Lowassa, kelele za wabunge zilikuwa
maradufu, wengi wao wakipiga meza kushangilia, hali iliyomfanya Rais
Kikwete anyamaze kwa sekunde kama 50 na ndipo Lowassa aliposimama na
kuinamisha kichwa kuonyesha kukubali shukrani hizo.
Wabunge
waliendelea kumshangilia hadi alipoketi na ndipo Rais Kikwete
akaendelea kutoa shukrani kabla ya kuhitimisha hotuba yake ya saa mbili
na dakika 20.
Awaweka wagombea gizani
Kuahirishwa
kwa vikao vya juu vya uchujaji makada wanaowania kugombea urais kwa
tiketi ya CCM, kumesababisha wagombea, wapambe wao na wanachama kubaki
gizani kwa kutoelewa kinachoendelea na hivyo kutoa nafasi ya kuenea
uvumi na ubashiri wa aina mbalimbali.
Kwa mujibu wa
ratiba iliyotolewa awali na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye
vikao vya juu vya uchujaji wa wagombea vilikuwa vianze juzi, kwa Kamati
ya Usalama na Maadili kujadili taarifa za wagombea urais na kutoa
ushauri kwa Kamati Kuu. Taarifa zilizopatikana jana jioni zilieleza kuwa
kikao hicho kilitarajiwa kuanza usiku wa jana ingawa kulikuwa na utata
mkubwa.
Ratiba hiyo ilionyesha kuwa kikao cha Kamati
Kuu kilikuwa kifanyike jana, lakini kutokana na sababu zisizojulikana
hakikufanyika na badala yake imeelezwa kitafanyika leo, siku ambayo
ilikuwa imepangwa rasmi kwa ajili ya mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa
(NEC) unaojumuisha wajumbe zaidi ya 400.
Kwa mujibu wa
ratiba hiyo, Mkutano Mkuu wa CCM ambao ndiyo wenye jukumu la kutoa
mgombea urais, ulipangwa kufanyika kesho na keshokutwa, lakini taarifa
zilizopatikana baadaye zilisema utafanyika kwa siku moja tu ya kesho.
Nape
alipotafutwa mara mbili kwa nyakati tofauti jana, majibu yake yalikuwa
mafupi; “ratiba niliyotoa ndiyo hiyohiyo, ifuateni kama mnataka
kuandika”.
Alipotafutwa jioni baada ya kuenea tetesi
kwamba vikao vyote vitafanyika leo, hakupokea simu lakini alituma ujumbe
mfupi wa maandishi ukisema: “Siwezi kuongea sasa… Samahani nipo
kikaoni, tuma meseji”. Lakini hata alivyotumiwa ujumbe hakujibu.
Baadhi
ya wajumbe wa Kamati Kuu walipoulizwa kikao chao kingefanyika lini,
walisema hawakuwa na taarifa na kwamba na wao walikuwa wanasubiri kupewa
taarifa.
Mmoja wa wajumbe wa NEC aliyekuwa akizunguka
kwenye ofisi za makao makuu ya CCM, huku akionyesha amechoka, alisema:
“Hapa nilipo hata sifahamu tutafanya lini kikao, nipo tu nazunguka
hapa.”
Giza hilo ambalo limewakumba wagombea na wajumbe
wa vikao, pia limesababisha kuenea kwa tetesi dhidi ya hatima za
wagombea na kutoa fursa kwa wajumbe wenyewe kuzodoana.
“Mgombea
wako keshamalizwa, kikao cha kamati ya maadili kimeshamkata,” ni
miongoni mwa tetesi walizokuwa wakirushana roho wajumbe wa vikao vya
CCM, ingawa taarifa za uhakika ni kuwa kikao hicho kilikuwa
hakijafanyika.
Wengine waliokuwa na uelewa mpana walijibu kwamba vikao havijafanyika, hivyo kuhoji mgombea angekatwa na kikao gani.
Taarifa
nyingine zilidai kuwa Kamati ya Usalama na Maadili ina dozi za baadhi
ya wagombea maarufu na kwamba alama za ufaulu kwenye kamati hiyo
zimewamaliza wengi.
Wagombea wanena
Pamoja
na ratiba ya vikao hivyo kubadilikabadilika, makada waliojitokeza
kuwania urais kwa tiketi ya CCM hawakuonekana kusumbuliwa na jambo hilo.
Mbunge
wa Sengerema, William Ngeleja alisema hana tatizo na kuchelewa kwa
vikao hivyo kwa kuwa vina ratiba zake na maandalizi yapo ndani ya
ratiba. Alisema viongozi wataendelea kutoa miongozo na anaamini msemaji
wa chama ataendelea kuujulisha umma kinachoendelea.
Mgombea
mwingine, Dk Hamis Kigwangalla alisema hakuwa na taarifa rasmi za
kutofanyika kwa vikao kama vilivyopangwa, lakini akasema hilo halikuwa
na madhara kwa wagombea na anaona sababu za kufanya hivyo ni kupunguza
presha.
“Naamini vikao vyote vitakaa na chama chetu
kuvisogeza mbele ni jambo la kawaida tumeshazoea. Nikiwa mmoja wa
wagombea, sina shaka wala wasiwasi wowote, ratiba iliyopangwa ya vikao
hivi imekutana na jambo kubwa.
Rais anatakiwa kuvunja
Bunge na baadhi ya wajumbe watahudhuria shughuli hiyo, hivyo lazima
visogezwe mbele,” alisema mgombea mwingine January Makamba.
Mwalimu
Banda Sonoko alisema kila kitu ni maandalizi hivyo anaamini kesho
watakuwa wamepata mgombea, kwani vikao hivyo vimeingiliwa na mambo
mengi, ndiyo maana vimesogezwa.
“Sina tatizo lolote,
natambua mwenyekiti wangu pia ni Rais ana shughuli nyingi. Hili ni jambo
zito, wahusika wanahitaji wasaa ili wasije kutupatia mgombea ambaye
hafai, sidhuriki na hii chelewa chelewa, nitavumilia na kujigharimia kwa
muda wote lakini tupate mgombea safi,” alisema Balozi Ali Karume.
Mjumbe
wa kamati ya kampeni ya Lowassa, Hussein Bashe alisema hili siyo jambo
la ajabu, bali ni kawaida kutokana na maelekezo ya chama vikao ni mpaka
Julai 12.
“Kuahirisha vikao vya Kamati ya Maadili, Kamati Kuu na NEC siyo jambo la kutilia shaka,” alisema.
Msemaji
wa Stephen Wasira, Masyaga Matinyi alisema anaamini kanuni, taratibu na
katiba ya chama vitaheshimiwa hivyo mchakato utakuwa wa haki.
“(Wasira)
Anaamini vikao vitafanyika kwa mujibu wa taratibu zilizopangwa, hivyo
kuahirishwa huko hakuwezi kuvuruga mchakato,” alisema Matinyi.
Kada
mwingine kwenye mbio hizo, Elidephonce Bilohe alisema anamwomba Mungu
ili kuahirishwa kwa vikao hivyo kumpe neema kwa jina lake kupitishwa
kuwa mgombea urais wa chama hicho.
“Jana (juzi)
nilikwenda ofisi za CCM nikakutana na ofisa wa ngazi ya juu ya chama
akaniambia kama tukihitajika na kikao chochote tutaitwa. Basi
nikaondoka, nipo hapa nyumbani namwomba Mungu anisaidie niweze kuipata
nafasi hii,” alisema Bihole.
Boniface Ndengo alisema kuahirishwa kwa vikao hivyo vya mchujo wa wagombea anaona hakuna tatizo.
“Nilishafanya sehemu yangu niliyotakiwa, sioni kama kuna usumbufu wowote,” alisema Ndengo.
Leonce
Mulende alisema suala hilo halimpi matatizo ya kisaikolojia kwa sababu
limewekewa programu za msingi, hivyo anafikiri watafikia hatima vizuri.
Balozi Patrick Chokala alisema: “Wenye shughuli zao ndiyo wanajua sababu za kuchelewa, wacha tusubiri watamaliza tu.”
No comments:
Post a Comment