Dar es Salaam.
Baada ya vikao mfululizo wiki hii, hatimaye Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) unatarajia kumtangaza mgombea urais wake kesho.
Baada ya vikao mfululizo wiki hii, hatimaye Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) unatarajia kumtangaza mgombea urais wake kesho.
Taarifa
zilizopatikana jana zimeeleza kuwa baada ya kikao cha viongozi wa ngazi
za juu wa Ukawa, umoja unaoundwa na NLD, Chadema, CUF na NCCR – Mageuzi
kilichofanyika juzi, mambo kadhaa yameafikiwa na kama hakutokuwa na
mabadiliko yoyote, mteule wa urais kupitia umoja huo atabainishwa.
Mwenyekiti
Mwenza wa Ukawa, Dk Emmanuel Makaidi alithibitisha kuwa tayari
makubaliano ya kugawana kata na majimbo kwa nafasi za udiwani na ubunge
yamekamilika na kilichobaki ni utekelezaji.
“Tumeshakubaliana
namna ya kugawana kata na majimbo 13 yaliyobaki na Jumamosi tutaweka
wazi kwa wananchi. Pamoja na hilo pia tutamtangaza mgombea urais na
chama anachotoka,” alisema Dk Makaidi.
Siku chache
baada ya baadhi ya wabunge kupewa adhabu ya kutohudhuria vikao vya Bunge
na Spika Anne Makinda, Jumanne ya wiki hii Chadema ilifanya mkutano wa
dharura kujadili mambo kadhaa ya kitaifa.
Siku moja
baada ya kikao hicho, viongozi wa waandamizi wa Ukawa walikutana na
kujadili mambo yanayohusu umoja huo kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
Hata
baada ya vikao hivyo, mpaka jana Chadema iliendelea na vikao vyake vya
ndani kujadili mambo kadhaa kabla ya kikao cha Kamati Kuu ya Ukawa
kinachotarajiwa kufanyika leo kupitisha jina la mgombea urais.
Naibu
Katibu Mkuu wa Chadema Bara, John Mnyika alithibitisha kuendelea kwa
vikao vya ndani vya chama hicho na kueleza kuwa hawezi kusema chochote
kwa sababu ajenda bado zinajadiliwa na kwamba kesho taarifa za uhakika
zitatolewa kwa vyombo vya habari.
“Kwa kifupi ni kwamba
kikao bado kinaendelea. Nimetoka mara moja tu kupokea simu yako.
Mazungumzo yatakapokamilika tutawajulisha (vyombo vya habari),” alisema
Mnyika.
Mvutano
Wakati
hilo likisubiriwa, zipo taarifa kuwa kuna mvutano baina ya vyama ndani
ya umoja huo hasa katika nafasi ya mgombea urais baada ya kuwapo kwa
watia nia zaidi ya mmoja.
Chanzo cha uhakika kutoka
ndani ya umoja huo kilisema kuwa Kamati Kuu ya Ukawa ina kazi kubwa ya
kuhakikisha kuwa maridhiano yanafikiwa ili kumpata mgombea atakayeungwa
mkono na vyama vyote katika jitihada za kuiondoa CCM madarakani.
“Licha
ya kutangaza kugawana kata na majimbo yaliyobaki jina la mgombea urais
litatangazwa pia. Hilo litafanyika endapo mwafaka utapatikana katika
kikao cha Kamati Kuu kitakachofanyika kesho (leo). Kikao kikiridhia
chama gani kitoe mgombea, basi Watanzania watamjua hiyo Jumamosi,”
kilisema chanzo hicho.
Chadema na CUF bado viliendelea
na vikao vyake vya ndani jana. Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi wa CUF,
Shaweji Mketo alisema hakuna taarifa ambayo ingeweza kutolewa jana.
Alipoulizwa
juu ya makubaliano yaliyopitishwa katika kikao cha Ukawa alijibu:
“Hakuna maazimio yaliyofikiwa, bado tupo katika mjadala.”
Kuhusu
kuungwa mkono miongoni mwa vyama vingine vya Ukawa kwa Mwenyekiti wa
CUF, Profesa Ibrahim Lipumba aliyetangaza nia, Mketo alisema hana
taarifa.
Wenyeviti wenza wengine wa vyama hivyo
hawakupatikana kuzungumzia suala hilo. Hata walipopigiwa simu zao za
mkononi, ziliita pasi na kupokewa.



No comments:
Post a Comment