Mahakama ya Kadhi, Ripoti ya Msola Kutikisa Bunge - LEKULE

Breaking

2 Feb 2015

Mahakama ya Kadhi, Ripoti ya Msola Kutikisa Bunge


Bunge linaendelea na mkutano wake wa 18, ambao kamati mbalimbali zitaendelea kuwasilisha taarifa kwa ajili ya majadiliano.

Licha ya kamati za kisekta na zisizo za kisekta, kabla ya Bunge kuahirishwa wiki hii, pia Kamati Teule iliyoundwa kuchunguza na kuchambua Sera mbalimbali zinazohusu masuala ya ardhi, kilimo, mifugo, maji na uwekezaji kubaini kasoro zilizomo katika matumizi ya ardhi, pia itawasilisha taarifa yake.
Kwa mujibu wa ratiba ya mkutano huo, miswada miwili itasomwa na kupitishwa na wabunge. Miswada hiyo ni ya Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa mwaka 2014 na ule wa Sheria ya Usimamizi wa Kodi wa mwaka 2014.
Ndani ya wiki hii, pia wabunge watajadili taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) zilizowasilishwa katika mkutano wa Bunge wa 15 uliofanyika Aprili, mwaka jana. Taarifa  hizo za CAG zitajadiliwa na wabunge kwa siku mbili mfululizo. Zinahusu hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Serikali za Mitaa na Mashirika ya Umma.
Kamati za kisekta zitakazowasilisha taarifa zake wiki hii ni Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira; Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji; Katiba, Sheria na Utawala; Tawala za Mikoa na Serikali za  Mitaa na Kamati ya Masuala ya Ukimwi. 
Nyingine zitakazowasilisha taarifa zake kwa ajili ya majadiliano ni Kamati ya Ulinzi na Usalama; Kamati ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa; Kamati ya Uchumi, Viwanda na Biashara; Huduma za Jamii na Kamati ya Maendeleo ya Jamii.
Wiki iliyopita, Bunge lilipokea na kupitisha taarifa za Kamati za Bunge zinazosimamia Fedha za Umma ambazo ni Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC); Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) na Kamati ya Bajeti. Pia Kamati ya Miundombinu na ya Nishati na Madini, ziliwasilisha taarifa na kujadiliwa katika kupitishwa na wabunge.
Wakati mjadala wa taarifa za kamati ulianza wiki iliyopita, wingu la uchaguzi mkuu linaonekana kutanda miongoni mwa wabunge, kutokana na wengi kujikita kwenye kero za majimboni mwao kuliko za kitaifa.
Wengi walilalamikia miundombinu ya majimboni mwao; hususani barabara, viwanja vya ndege na usafiri wa treni. Pia kwa upande wa taarifa ya Kamati ya Nishati ya Madini, wengi waliochangia, walilalamikia vijiji vyao kutofikiwa na umeme.
Mathalani, katika kujadili taarifa za Kamati ya Miundombinu na ile ya Nishati na Madini, wabunge wengi waliochangia, walitetea maeneo wanayotoka tofauti na taarifa za kamati zilivyoainisha,  kiasi ambacho hata Spika wa Bunge, Anne Makinda alibaini hali hiyo.
Akizungumza baada ya mjadala wa kamati hizo kuhitimishwa mwishoni mwa wiki, Spika Makinda alipongeza taarifa zote za kamati za kudumu za Bunge zilizowasilishwa kwa kusema zimeboreshwa inavyopaswa.
Makinda alisema katika michango ya wabunge, wengi wamechangia kwa kujielekeza kwenye majimbo  tofauti na taarifa za kamati zilivyowasilisha.  Aliweka wazi kwamba hayo yanajitokeza kutokana na ukweli kwamba hiki ni kipindi cha ‘lala salama’ kwa maana ya kipindi kuelekea uchaguzi mkuu.
Baada ya kamati zote kukamilisha uwasilishaji wa taarifa wiki iliyopita, utakuja Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali, kabla ya taarifa ya Kamati Teule iliyoundwa kuchunguza na kuchambua sera mbalimbali zinazohusu  masuala ya Ardhi, Kilimo, Mifugo, Maji na uwekezaji  kubaini kasoro zilizomo katika matumizi ya ardhi.
Kamati hiyo teule iliundwa na Spika Makinda Novemba mwaka jana. Alifikia hatua hiyo baada ya Bunge kuridhia kuundwa kwake kutokana na malalamiko ya wabunge bungeni, kuhusu migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji, ambayo kwa muda mrefu haijapatiwa ufumbuzi na kusababisha madhara ikiwamo mauaji.
Alipoiunda, Makinda alisema baada ya kazi yake, kamati itapeleka mapendekezo yake bungeni yatekelezwe na serikali kupunguza au kuondoa migogoro ya muda mrefu kati ya wakulima, wafugaji, wawekezaji na watumiaji wengine wa ardhi.
Hadidu rejea za kamati hiyo ni kuchambua sera mbalimbali zinazohusu matumizi ya ardhi kubainisha kasoro zilizomo na kuchunguza mikakati ya utekelezaji wa sera hizo iliyowekwa na serikali.
Imefanya pia mapitio ya taarifa nyingine za kamati na tume zilizoundwa nyuma kushughulikia migogoro ya wakulima na wafugaji.
Hadidu nyingine ni kuchambua mikakati yote ya serikali ya kusuluhisha migogoro ya wakulima na wafugaji; Kuchambua mikakati ya kulinda vyanzo vya maji pamoja na uharibifu wa mazingira.
Kamati hiyo katika hadidu nyingine, inapaswa kutoa mapendekezo yatakayoondoa migogoro iliyopo na kudumisha uhusiano mzuri na utangamano kati ya wakulima na wafugaji na pia itapendekeza hatua za kuchukua za kiuwajibikaji.
Walioteuliwa kuunda kamati na kufanya kazi hiyo ni Profesa Peter Msola (Kilolo-CCM), Jenista Mhagama (Peramiho-CCM), Magdalena Sakaya (Viti Maalumu-CUF), Joseph Selasini (Rombo-Chadema) na Christopher ole Sendeka (Simanjiro-CCM).

No comments: