JK apuliza kipyenga urais 2015 - LEKULE

Breaking

2 Feb 2015

JK apuliza kipyenga urais 2015


Wakati Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikitarajia kutangaza ratiba yake ya mchakato wa uteuzi wa wagombea wake katika uchaguzi mkuu wa Oktoba, mwaka huu, Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete, jana alipuliza kipyenga cha mbio za urais.
Alisema kwamba kama wanachama walioanza kujitokeza kuwania uteuzi wa urais hawana sifa, wananchi na wanachama wasisite kushawishi watu wengine wenye sifa wajitokeze kuchukua fomu.
Rais Kikwete alitoa rai hiyo jana wakati akihutubia mamia ya wananchi kwenye kilele cha maadhimisho ya miaka 38 ya kuzaliwa kwa CCM yaliyofanyika kitaifa mjini Songea katika uwanja wa Majimaji.
“Uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba, mwaka huu wa kupata rais wa awamu ya tano, utakuwa wa kihistoria, nataka rais atoke CCM na maelezo ni rahisi tu; Mwalimu Nyerere alishawahi kusema rais anaweza kutoka chama chochote cha siasa, lakini rais bora lazima atoke CCM, na huu ni wosia mzuri na muhimu sana,” alisema.
Hadi   sasa  makada   wa   CCM waliotangaza nia kuwania urais kupitia chama hicho ni Naibu Waziri wa Sayansi, Teknolojia na Mawasiliano, January Makamba; Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba; Mbunge wa Nzega, Dk. Hamis Kigwangalla; Waziri Mkuu wa sasa, Mizengo Pinda na Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu.
Wanaotajwa kuwania ni Mbunge wa Songea Mjini, Dk. Emmanuel Nchimbi; Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja; Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe; Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta na mawaziri  wakuu wastaafu, Edward Lowassa na Frederick Sumaye.
Wengine ni Spika wa Bunge, Anne Makinda; Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Asha-Rose Migiro; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalum), Prof. Mark Mwandosya na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira.
Rais Kikwete alisema viongozi na wanachama wa CCM ni lazima wawe mstari wa mbele kupata mgombea aliye bora ambaye siku atakapotangazwa wananchi hawatakuwa na wasiwasi naye.
“Siyo wakiulizwa waanze kusema hapa hapana, tutakuwa tumepuuza wosia wa muasisi wa Taifa, Mwalimu Nyerere,” alisema.
“Nyerere alisema bila CCM imara nchi itayumba, viongozi tusikubali tuwe wa kwanza kukiuka wosia huu, laana yake itakuwa kubwa kwa Taifa na nchi itayumba, watu wazuri CCM wapo na kama walioanza kujitokeza sasa hawafai, tuwashawishi wajitokeze wengine wakachukue fomu, hata sisi tulishawishiwa japo hatukuwa na mpango wa kuwania urais,” alisema.
Alisema kujitokeza au kumshawishi mtu agombee uongozi siyo dhambi na kwamba chama hicho kisifanye ajizi katika jambo hilo la kupata viongozi bora kwa sababu lina maslahi ya chama na nchi kwa ujumla.
Rais Kikwete alisema suala la kushinda dola ndiyo madhumuni makuu na msingi wa chama hasa ikizingatiwa kuwa CCM siyo chama cha kucheza mpira au cha burudani na kwamba zipo kanuni na vigezo vya kupata viongozi walio bora ambao wanachunjwa katika ngazi zote za vikao vya chama.
“Hapataharibika jambo, CCM itawapatia wagombea bora ambao wananchi watawakubali, cha msingi wagombea wasingatie masharti ya kikatiba ya chama, kanuni na maadili ya kuteuliwa, asiyezingatia hayo asije akakilaumu Chama bali ajilaumu mwenyewe kwa kutozingatia kanuni zilizowekwa,” alisema.
Rais Kikwete alisema tangu Tanzania ilipoingia katika mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992 CCM imeendelea kuimarika, kudumisha amani na mshikamano , Watanzania na wananchi wameendelea kukiamini Chama hicho.
Alisema ushindi ambao CCM imeupata katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika mwishoni mwaka jana ni dalili nzuri kwa vyama vya wapinzani, akisema hawana chao katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Hata hivyo, alisema wanachama wa CCM wasibweteke na ushindi uliopatikana katika uchaguzi huo kwa sababu uchaguzi mkuu ujao unaweza kuwa na changamoto nyingi ambazo ni lazima zihitajike nguvu ili kukiwezesha Chama kupata ushindi wa kishindo.
Alisema viongozi na wanachama wa CCM ni lazima watambue kuwa nguvu ya Chama inaanza kwenye chama, hivyo lazima kuwe na ari na nguvu mpya ya viongozi na wanachama wa CCM kwani bila umoja ushindi hauwezekani.
Rais Kikwete alisema wakati uchaguzi mkuu ukiwa umekaribia, wapo baadhi ya viongozi ambao hawajafanya chochote katika maeneo yao na kwamba wanamsikitisha sana kwa kuwa watasababisha chama kupata upinzani mkali.
ATAHADHARISHA  FEDHA CHAFU
Alisema yapo mambo kadhaa ambayo Chama kilikubaliana ambayo ni pamoja na kila ngazi ya chama wilaya na mkoa kuhakikisha inakuwa na mfuko wa uchaguzi ambao mwaka huu ndiyo unatakiwa kufanya kazi.
“Nawatadharisha msichukue fedha za moto mtaungua vidole, msichukue kila fedha nyingine zina matatizo, tunapoanza safari ya miaka 39 tunapashwa kuondoa utegemezi wa fedha, misaada, ruzuku na misaada ya wafanyabiashara kwa sababu si mambo endelevu,” alisema.
Rais Kikwete alisema huu ni mwaka wa kuhakikisha kunakuwa na nyenzo za kazi ambazo ni jumuiya za CCM ili kukiwezesha chama kuungwa mkono na jamii pana ya Watanzania.
Rais Kikwete aliongeza kwa ukifanya maandalizi mazuri sasa wakati wa uchaguzi hutahangaika, utakuwa unavaa suti tu kwani kila kitu kitakuwa mteleremko, usipofanya maandalizi utafanya henya henya, lazima jasho likuvuje.
Alisema wanachama na viongozi wa CCM wanatakiwa kufanya kazi kwa nguvu zaidi kasi na ari zaidi kama kauli mbiu ya chama inavyoeleza kwa kutambua ahadi ambazo zilitolewa wakati wa uchaguzi mkuu uliopita na kuzifuatilia kama zimetelekezwa.
“Zipo ahadi za rais, chama mkoa, wilaya  ambazo nyingine tulibanwa tukaziahidi,” alisema.
Alisema mwaka 2015 ni wa kuongeza ukumbwa wa jeshi ambalo ni wanachama, hivyo jitihada zifanyike kuongeza idadi ya wanachama na kwamba Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, ameagiza kuongeza kadi mpya milioni mbili.
Alisema jambo lingine ni kwa viongozi wa chama hicho kuwatembelea wananchi na kuzungumza nao, lakini makatibu wa CCM wamekuwa hawafanyi hivyo.
Rais Kikwete alisema amekuwa akiwatuma watu kufuatilia maagizo yake na kumweleza kuwa wamekuwa hawatekelezi ipasavyo na kuonya kuwa viongozi na wanachama wa CCM lazima watambue kuwa CCM haiwezi kupata ushindi kwa watu wasiowatembelea kusikiliza kero zao.
Alimpongeza Kinana kwa kazi kubwa anayofanya ya kukiimarisha chama tofauti na viongozi wa chama hicho wa ngazi ya wilaya na mikoa.
“Tumewapa magari tena ya mkonga mtembelee wananchi, lakini hawawaoni, wenzetu wa upizani wanafanya vyema katika hili, bila kuwatembelea wananchi hatuwezi kuwa na uhakika wa kushinda,” alisema.
Rais Kikwete alisema viongozi waache kung’ang’ania kukaa ofisini, badala yake watoke kuzungumza na wananchi na kuwashawishi waichague CCM.
KURA YA MAONI 
Rais Kikwete alisema maandalizi kwa ajili ya kura ya maoni kuamua Katiba Inayopendelezwa yanaendelea na kinachofanyika sasa ni uandikishaji wapiga kura pamoja na uchapishaji na usambazaji wa katiba hiyo.
“Watani wetu watatoa elimu hasi na sisi tutoe elimu chanya ili ipite,” alisema.
Alisema Katiba Inayopendekezwa imebeba maslahi ya nchi na misingi yote imezingatiwa, lakini wapinzani wanaikataa kwa sababu tu muundo wa serikali tatu haupo.
Alisema kitendo cha vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kutangaza kususia kura za maoni kinasikitisha na hakimshangazi kwa kuwa tangu mchakato wa katiba mpya umeanza wamekuwa wakizua kila jambo jipya.
Aliwaambia Watanzania kuwa haoni sababu ya kuikataa Katiba Inayopendekezwa la sivyo Katiba ya sasa ya mwaka 1977 itakuwa inaendelea kwa vile hakuna nyingine hadi miaka ijayo hadi rais ajaye au baada ya huyo.
Alisema anaweza kuja mwingine na kusema hakuna haja ya kuandikwa katiba mpya.

No comments: