WIZARA ya Katiba na Sheria imesema iko haja ya hukumu zinazotolewa katika Mahakama nchini, ziandikwe katika Kiswahili kuwezesha haki kutendeka na ionekane imetendeka.
Naibu Waziri, Ummy Mwalimu alisema hayo jana wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Amina Mwidau (CUF) aliyeshauri serikali kuangalia uwezekano wa hukumu kutolewa kwa lugha hiyo.
“Ni kweli kwamba kuna haja sasa hata hukumu zinazotolewa katika Mahakama ziandikwe kwenye Kiswahili ili haki iweze kutendeka na ionekane imetendeka,”si ya Tuki ili tuweze kutengeneza istilahi na misamiati itakayoweza kutumika katika mahakama zetu,” Mwalimu alisema.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri, pia wamefanya mawasiliano na Baraza la Kiswahili Tanzania (Bakita) na wanaendelea kushauriana juu ya hilo.
Katika kuelezea namna ambavyo serikali inaendelea kuimarisha Kiswahili, Mwalimu alisema hivi sasa miswada yote inayoletwa bungeni inakuja katika lugha mbili; Kiswahili na Kiingereza.
Alisisitiza kwamba katika Katiba Inayopendekezwa Ibara ya 4, inasisitiza kwamba lugha ya taifa itakuwa ni Kiswahili na itatumika katika mawasiliano yote rasmi serikalini.
Alihimiza wananchi kuipigia kura katiba hiyo kuhakikisha Kiswahili kinatumika katika Mahakama. Awali akijibu swali la msingi la Mbunge wa Kilwa Kusini, Selemani Bungara (CUF), Naibu Waziri alisema matumizi ya Kiswahili katika ngazi zote za Mahakama yanaruhusiwa kwa sababu ni matakwa ya sheria.
Alisema ili kuhakikisha uamuzi wa Mahakama unaeleweka kwa pande zote, sheria inaelekeza kuwa pale ambapo mshitakiwa ataomba nakala ya hukumu, kama inawezekana, itatafsiriwa katika lugha anayotaka mshitakiwa bila kuchelewa na bila malipo.
Mbunge Bungara katika swali la msingi, alisema Mahakama kuanzia ngazi ya Wilaya hadi Rufaa hutumia Kiingereza kuendesha mashauri mahakamani na kufanya wateja wengi washindwe kukidhi matakwa ya Mahakama kama vile kuandaa nyaraka za kesi na kuwafanya kukosa haki zao za msingi hasa pale wanapokosa uwezo wa kuweka wakili.
Bungara alihoji, “iweje serikali haioni umefika wakati sasa mahakama zetu kutumia Kiswahili kuendeshea mashitaka na kuandika hukumu ili kuwawezesha Watanzania wengi kuelewa na kufuatilia masharti mahakamani.”
No comments:
Post a Comment