Familia Ya Rais Mstaafu Jakaya Kikwete Yatoa TAMKO Zito....Yasisitiza Haihusiki na Utoroshaji wa Makontena Bandarini.Mwenye Ushahidi Autoe - LEKULE

Breaking

25 Dec 2015

Familia Ya Rais Mstaafu Jakaya Kikwete Yatoa TAMKO Zito....Yasisitiza Haihusiki na Utoroshaji wa Makontena Bandarini.Mwenye Ushahidi Autoe


Mbunge wa Chalinze, Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete,  ambaye ni mtoto wa Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete ,kwa niaba ya familia yake ametoa tamko zito kupinga tuhuma mbalimbali zinaozoelekezwa kwake na familia yake.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam Jana,Ridhiwani alisema baada ya Rais Kikwete kumaliza muda wa miaka 10  madarakani, baadhi ya watu wamekuwa wakiiandama familia yao kwa tuhuma mbalimbali.

Alisema baadhi ya tuhuma zinamhusisha yeye mwenyewe kwa lengo la kuupotosha uuma.

Alizitaja tuhuma hizo kuwa ni utoroshaji wa makontena kwenye bandari ya Dar es Salaam na kusisitiza kwamba tuhuma zote zinazotolewa hazina ukweli wowote bali zimelenga kumchafua yeye na familia yake.

Ridhiwani alisema tangu serikali ya awamu ya tano ianze kuwabana  watu wanaokwepa kulipa kodi za serikali,baadhi ya watu wanafanya jitihada za kumhusisha  na  watuhumiwa  hao.

Alisema hajawahi kuagiza bidhaa yoyote kutoka nje,kuwa na kontena la kulipiwa ushuru,kukwepa au kumuombea msamaha wa kupunguziwa kodi mfanyabiashara yeyote aliyeagiza kontena kutoka nje, hivyo mwenye ushahidi juu ya hilo autoe.

"Kama kuna mtu mwenye ushahidi autoe hadharani mimi niuone,dunia iuone, nawahakikishia ushahidi huo haupo na hautokuwepo labda uwe wa kughushi na wakifanya hivyo wataumbuka.


"Sina na sijawahi kumiliki lori au basi katika maisha yangu.Sina hisa wala ubia na mtu yeyote  au kampuni ya malori au mabasi." Alisema Ridhiwani na kuongeza;

"Naambiwa hapa nchini siku hizi kila jengo jipya linalojengwa inasemekana ni langu na vituo vipya vya mafuta naambiwa ni vyangu.Huo ni uongo mtupu.

"Naomba nimalizie kama nilivyoanza,yanasemwa mengi lakini ni maneno ya uzandiki na uzushi mtupu usio na chembe ya ukweli.

"Wanaosema, kuandika na kueneza maneno hayo wanajua wanasema uongo isipokuwa wanafanya hivyo kwa nia mbaya dhidi yangu na familia yangu.Nawaomba watanzania muwapuuze."

No comments: