Pinda Amjibu Lowassa.....Asema Umaskini hauwezi kuondolewa kwa siku 100 - LEKULE

Breaking

11 Oct 2015

Pinda Amjibu Lowassa.....Asema Umaskini hauwezi kuondolewa kwa siku 100


Waziri Mkuu, Mizengo Pinda amewabeza wanaosema umaskini wa Watanzania unaweza kuondolewa ndani ya siku 100.

Akizungumza na wakazi wa Usevya na vijiji vya jirani kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya Usevya, Wilaya ya Mlele mkoani Katavi, Pinda alisema umaskini wa Watanzania si wa siku moja.

“Ninashangaa kusikia watu wakijitapa kuwa eti wataendesha nchi kwa kasi ya ajabu na kwamba, ndani ya siku 100 watamaliza shida zote na kuondoa umaskini miongoni mwa Watanzania.

“Kazi ya kuongoza nchi inataka umakini, uzoefu na watu waliobobea kwenye uongozi. Hii si kazi ya majaribio hata kidogo. Eleweni kuwa changamoto ni sehemu ya maendeleo,” alisema.

Mgombea urais kupitia Chadema, Edward Lowassa, amekuwa akisema anachukia umaskini na ataweza kuuondoa katika kipindi kifupi akiingia Ikulu.

Akimzungumzia mgombea urais wa CCM, Pinda alisema: “Tuaminini CCM na tupeni nafasi tufanye kazi kwa kumpa kura zote Dk Magufuli, mbunge wa CCM na madiwani wa CCM.”

Alimpamba Dk Magufuli kuwa ni mchapakazi anayeweza kukabiliana na kero mbalimbali za Watanzania na hakuna mwenye shaka na utendaji wake.

Kwa upande mwingine, Pinda amewaonya wanaobeza juhudi za kuleta maendeleo zilizofanywa na Serikali tangu wakati wa Uhuru.

Alisema wapo wanaofananisha maendeleo ya Rwanda na Tanzania wakati ukubwa wa nchi hiyo ni kilometa za mraba 27,000 wakati Tanzania ni 945,000 ambayo ni kubwa mara 35 zaidi ya Rwanda. “Ukubwa wa Rwanda ni sawa na wilaya moja tu ya Mlele ambayo ina zaidi ya kilometa 29,000.


Tuna wilaya ngapi kubwa kuliko Rwanda?” Alihoji na kuongeza: “Acheni tabia ya kulinganisha vi-nchi vidogo na Tanzania. Kazi ya kuleta maendeleo siyo ndogo.”

No comments: