Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ni ya kibaguzi? - LEKULE

Breaking

26 Mar 2015

Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ni ya kibaguzi?

Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) ya mjini The Hague ilianza kazi zake karibu miaka 15 iliyopita.
Wababe wa kivita kadhaa, wanamgambo na wakuu wa nchi wameshafikishwa mbele ya mahakama hiyo, wakishtakiwa kwa uhalifu mkubwa wanaodaiwa wameufanya dhidi ya raia.
Mahakama hiyo ni matokeo ya mlolongo wa historia ya mwanadamu kupambana na dhuluma na ukatili unaofanywa na mwanadamu mwenzake anayetumia vibaya madaraka aliyonayo.
Katika miaka ya 1990, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, lilianzisha mahakama za kimataifa za uhalifu wa kivita uliofanyika Yugoslavia na Rwanda.
Ilipofika mwaka 2002, zaidi ya nchi 60 zilikuwa tayari zimetia saini Mkataba wa Roma wa kuanzisha mahakama ya kudumu ya kimataifa ya uhalifu, makao yake yakiwa The Hague, Uholanzi.
Kwa mujibu wa mkataba huo, mahakama hiyo inajishughulisha na mauaji ya kimbari, uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu. Ina dhamana ya kufungua mashtaka pale nchi inaposhindwa au inapokataa kuyashughulikia maovu hayo katika ngazi ya kitaifa.
Mtu binafsi anaweza kushtakiwa ikiwa amefanya uhalifu huo katika nchi iliyotia saini mkataba huo au mtu huyo akiwa anatokea katika nchi iliyotia saini mkataba huo.
Hata hivyo, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupitia azimio lake linaweza kuitaka mahakama hiyo ifungue kesi kuhusu uhalifu uliotokea hata katika nchi isiyokuwa mwanachama.
Hali hii imeshatokea kwa nchi kama Sudan na Libya. Kimsingi, shughuli za mahakama hiyo haziwezi kuzuiwa hata na Baraza ila tu zinaweza kusitishwa kwa angalau mwaka mmoja.
Kesi zinazoendelea
Katika ofisi ya Mwendeshaji Mkuu wa mahakama hiyo, Fatou Bensouda kuna picha za watu 24 ambao hivi sasa wanapelelezwa wakiwamo wakuu wa nchi, mawaziri na majenerali wengi kutoka Afrika.
Hata ilipoundwa, watu wengi walisema mahakama hiyo itakuwa ya Kiafrika, wakimaanisha kwamba wengi watakaoshtakiwa watakuwa Waafrika. Hivyo, wanasiasa wa Kizungu hawana haja ya kuiogopa. Swali ni je, kuna ubaguzi katika kazi ya mahakama hiyo?
Baadhi ya wanasiasa wa Kiafrika wanaipinga na kuiita kuwa ni chombo cha mataifa ya kikoloni. Kati ya wale wasiotaka kusikia chochote juu ya mahakama hiyo ni Rais Omar Al-Bashir wa Sudan ambaye amechukua juhudi za ziada kuchafua jina la mahakama hiyo.
Mwaka 2009 Al-Bashir alishtakiwa na mahakama hiyo kwa uhalifu wa kivita dhidi ya binadamu pamoja na mauaji ya kimbari. Msimamo wake wa kuikaidi mahakama hiyo umeungwa mkono na Waafrika kadhaa. Hata Umoja wa Afrika (AU) haushirikiani kwa dhati na mahakama hiyo.
Rais Yoweri Museveni wa Uganda, aliye madarakani tangu mwaka 1987, aliwahi kutoa wito kwa nchi za Kiafrika kujitoa kutoka Mkataba wa Roma ulioanzisha mahakama hiyo.

Upinzani wa viongozi wa Kiafrika dhidi ya Mahakama ya The Hague, umesababisha Bensouda asimamishe upelelezi uliokuwa unafanywa dhidi ya Rais Al-Bashir.
Sababu ni kwamba amehisi hana nafasi ya kufanikiwa akimshtaki kiongozi huyo kwa vile hajapata ushirikiano wa kutosha huko Sudan ambako ndiko kwenye ushahidi wote kuhusu kesi hiyo.
Licha ya sura iliyojitokeza kwamba mahakama hiyo ni ya upande mmoja, ni dhidi ya Waafrika, lakini uchunguzi unaonyesha Waafrika wengi wanaitaka. Wao hawakubaliani na ile hoja kwamba mahakama hiyo inaendeleza matakwa ya mataifa ya kikoloni.
Lini Wazungu watafikishwa The Hague?
Wakati huohuo kuna watu wanaohoji kwamba kuaminika kwa mahakama hiyo ya kimataifa, kutazidi pale watu watakapomuona kiongozi wa Kizungu akisimamishwa kizimbani huko The Hague.
Wanataka viongozi wa Kizungu nao wakamatwe ukimtoa mmoja tu aliyewahi kuhukumiwa, ambaye ni Rais Slobodan Milosevic wa Yugoslavia.
Wanawataja watu kama Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, Tony Blair, Rais wa zamani wa Marekani, George W. Bush na aliyekuwa Waziri wake wa ulinzi, Donald Rumsfeld. Hawa waliendesha vita ya uvamizi vya Iraq vilivyosababisha kutokea uhalifu mkubwa wa kivita na vifo vya maelfu ya watu.
Wakati wa vita hiyo, mamia ya watu waliteswa kimyakimya, ikidaiwa kwamba viongozi hao wa Marekani walijua na kuyaridhia mambo hayo. Wadadisi wanasema kuna hoja nzito ya kuweza kuwashtaki wanasiasa hao na hakuna shida ya kupata ushahidi dhidi yao.
Hata hivyo, swali ni kuwa kuna mtu mwenye akili anayefikiria kwamba Bush anaweza kufikishwa The Hague? Bila shaka haiwezekani. Katu! Kizuizi kikubwa ni kwamba Marekani haijatia saini mkataba wa kuyakubali mamlaka ya Mahakama ya ICC.
Fatou Bensouda hakubali kwamba Mahakama ya The Hague inabagua katika kuendesha shughuli zake. Waziri huyo wa sheria wa zamani wa Gambia, anadai kwamba yeye na wenzake, wengi wakiwa ni Waafrika kuliko Wazungu, wanaishughulikia zaidi Afrika kwa vile ni katika bara hilo ambako kunafanyika visa vingi vilinavyokwenda kinyume na haki za binadamu.
Bensouda anaeleza kwamba yeye anaendesha pia upelelezi juu ya uhalifu wa kivita uliofanyika Georgia, Columbia na Honduras. Katika nchi hizo, bado uhalifu haujafikia kiwango cha Afrika kwa ukubwa na wingi.
Hivi sasa aliyekuwa Rais wa Ivory Coast, Laurent Gbagbo anakabiliwa na mashtaka kwani baada ya kushindwa katika uchaguzi wa urais mwaka 2010 na kukataa kuondoka madarakani, wafuasi wake waliwaandama wapinzani wao kwa kuwafanyia ukatili.
Kwa msaada wa Ufaransa, Gbagbo alikamatwa na kufikishwa The Hague. Lakini mwenzake wa Kenya, Uhuru Kenyatta, amefutiwa mashtaka licha ya awali, kushtakiwakutokana na machafuko baada ya uchaguzi wa Kenya wa mwaka 2007/08.
Zaidi ya nchi 120 zimeuidhinisha Mkataba wa Roma na kuyakubali Mamlaka ya ICC. Nchi zenye watu wengi, zikiwamo Urusi, China na Marekani, pamoja na nchi zote za Kiarabu na Israel zimekataa kuingia katika mkataba huo.
Ikiwa hakuna Mzungu atakayeshtakiwa mbele ya mahakama hiyo na wanaoburuzwa huko The Hague watabaki kuwa ni Waafrika, mahakama hiyo itapata shida kuaminiwa barani Afrika.

No comments: