SERIKALI imesisitiza agizo lake la kusitisha ujenzi wa ofisi za wizara na taasisi zake katika jiji la Dar es Salaam badala yake uelekezwe mjini Dodoma, ikiwa ni hatua ya kuhamishia makao makuu mjini Dodoma.
Naibu Waziri , Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Aggrey Mwanri alisema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Chilonwa, Ezekiah Chibulunje (CCM) aliyetaka kufahamu sababu za Serikali kushindwa kupeleka bungeni muswada wa sheria ya kutambua mji wa Dodoma kuwa Makao Makuu ya Nchi.
Awali katika majibu ya swali la msingi la Chibulunje, Mwanri alisema kuanzia mwaka wa fedha 2010/2011, serikali ilitoa agizo la kuzuia ujenzi wa majengo mapya ya wizara katika jiji la Dar es Salaam.
Agizo hilo lilitolewa mara baada ya serikali kupitia Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu kukamilisha kuandaa mapitio ya Mpango Kamambe wa mji wa Dodoma, ambao umewezesha kutenga eneo maalumu lenye ukubwa wa hekta 8,033 kwa ajili ya ujenzi wa mji wa serikali.
Akijibu swali la mbunge juu ya sababu za serikali kushindwa kuleta muswada bungeni wa sheria ya kutambua Dodoma kuwa Makao Makuu, Mwanri alisema kwa sasa waraka wa Baraza la Mawaziri wa kutunga sheria husika uko katika hatua za kupata maoni ya Sekretarieti ya Baraza.
No comments:
Post a Comment