HATIMAYE Rais Jakaya Kikwete ametimiza ahadi yake aliyoitoa Agosti mwaka jana katika Chuo Kikuu cha Mzumbe cha Morogoro, kwamba amekusudia kufuta ada ya shule za sekondari nchi nzima.
Akizindua Sera mpya ya Elimu na Mafunzo 2014 katika Shule ya Sekondari ya Majani ya Chai, Kipawa jijini Dar es Salaam jana, Rais Kikwete alitangaza kufutwa kwa ada ya sekondari, kuanzia mwakani.
Kwa tangazo hilo, Bajeti ya mwisho ya uongozi wa Rais Kikwete itakayoanza kujadiliwa Mei mwaka huu, itatakiwa kuwa na fungu la kulipa gharama ambazo wananchi wamekuwa wakitoa kwa watoto wao wanaosoma elimu ya sekondari katika shule za Serikali nchi nzima.
Kwa sasa wazazi wamekuwa wakilipa Sh 20,000 kwa shule za kutwa na Sh 70,000 kwa shule za bweni, ili watoto wao wapate elimu ya sekondari.
Ubora
Alisema sera hiyo imezingatia stadi za msingi ambazo ni kuandika, kusoma na kuhesabu, ili kuwezesha watoto kujengwa kwenye msingi mzuri na hata kwenye Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) hilo limezingatiwa.
“Hata kwenye mpango wa BRN tumelizungumza ili kuhakikisha inatolewa elimu bora. Tusifanye mambo ya kuchekesha mtoto anafika madarasa ya juu hajui kuandika, kusoma na kuhesabu.
“Kuanzia sasa kama mtoto anafika darasa la pili, hajui kusoma, kuandika na kuhesabu (KKK), ni bora asiende darasa la tatu…naamini watoto wakiimarishwa katika stadi za KKK itaondoa matatizo haya,” alisema.
Tathimini ya Msingi ya Taifa kwa ajili ya uwezo wa wanafunzi katika KKK, kwa wanafunzi wa Darasa la Pili iliyofanyika mwaka jana, ilibaini kuwa asilimia 98 ya wanafunzi wa Darasa la Pili nchini, walikuwa hawaelewi wanachokisoma.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa alisema, tathimini hiyo imefanywa kwa baraka za Wizara yake kwa kushirikiana na Shirika la Misaada la Marekani (USAID), ili kupata taarifa kuhusu hali halisi ilivyo ya wanafunzi wa Tanzania kumudu stadi za KKK wanapofika Darasa la Pili.
Mafanikio
Mbali na mafanikio ya kufikia uwezo wa kuanza kutoa elimu ya msingi na sekondari bure, huku msisitizo ukiwekwa katika utoaji wa elimu bora, Rais Kikwete pia ilitangaza mafanikio mengine katika sekta ya elimu ambayo yamefikiwa katika uongozi wake wa miaka kumi.
Rais Kikwete alisema sasa elimu imepewa kipaumbele katika sera na shughuli za serikali, ndio maana Bajeti ya Elimu, ndio kubwa kuliko bajeti zote.
Alifafanua kuwa mwaka 2005/06 bajeti hiyo ilikuwa Sh bilioni 6.7, wakati mwaka huu wa fedha imepanda na kufikia Sh trilioni 3.1.
Hatua hiyo ya kibajeti kwa mujibu wa Rais Kikwete, ni ongezeko la mara tano ya Bajeti ya mwaka 2005 sawa na asilimia 20 ya Bajeti ya Serikali ambayo inatengwa kwa ajili ya elimu.
Katika suala la mikopo kwa ajili ya wanafunzi wa elimu ya juu, Rais Kikwete alisema imetoka Sh bilioni 56 kwa mwaka wa fedha 2005/06, hadi kufikia Sh bilioni 345 kwa mwaka huu wa fedha.
Aidha, kwa mwaka jana, wanafunzi wanaonufaika na mikopo ya elimu ya juu, waliongezeka kutoka wanafunzi 16,000 mwaka 2005 hadi kufikia 95,000.
Kwa upande wa shule za msingi, alisema zimeongezeka kutoka 14,000 kwa mwaka 2005 hadi kufikia shule 16,343 kwa mwaka 2014, huku shule za sekondari zikiongezeka kutoka 531 kwa mwaka 2005, hadi kufikia 4,576, mwaka 2014.
Idadi wanafunzi wanaojiunga na sekondari, Rais Kikwete alisema imeongezeka kutoka wanafunzi 524,325 mwaka 2005 na kufikia wanafunzi milioni 1.8.
Rais Kikwete alisema pia vyuo vya ufundi vimeongezeka kutoka vyuo 184 mwaka 2005 na kufikia vyuo 744 kwa mwaka 2014, huku vyuo vikuu vikiongezeka kutoka vyuo vikuu 26 mwaka 2005 na kufikia vyuo vikuu 50 kwa mwaka 2014.
Alikumbusha kuwa kama sio kuanzishwa kwa shule za kata, idadi ya wanafunzi pia isingeongezeka.
“Hali imebadilika, sasa wanafunzi wengi wanakwenda shule na vyuoni na suala la watoto na vijana kupata fursa ya kusoma, sio tatizo katika sekta ya elimu, sasa kinachotakiwa ni kuhakikisha inapatikana elimu bora kwa kuboresha mazingira ya elimu,” alisema Rais Kikwete.
No comments:
Post a Comment