SHIDA YA MAJI JIJI LA DAR ES SALAAM KUWA HISTORIA - LEKULE

Breaking

2 Mar 2016

SHIDA YA MAJI JIJI LA DAR ES SALAAM KUWA HISTORIA



 Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi Dawasa Mhandisi Romamus Mwang’ingo (Kushoto)  akitoa maelekezo kwa Mkuu wa msafara wa kamati ya Ushauri ya mkoa wa Dar es Salaam Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Raymond Mushi (Kulia) juu ya ufanyaji kazi wa mitambo ya Ruvu chini.

 Mafundi wakiwa katika harakati za kulaza bomba litakalotumika kuleta maji kwenye tanki kubwa lililopo kibamba toka Ruvu chini na juu kwa ajili ya uhifadhi na usambazaji maji katika Jiji la Dar es salaam. 

Mafundi wakikarabati bomba kuu la kusambaza maji toka Ruvu juu katika kuhakikisha upatikanaji wa huduma ya maji katika Jiji la Dar es Salaam na maeneo jirani.

 Mkuu wa msafara wa kamati ya Ushauri ya mkoa wa Dar es Salaam Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Raymond Mushi (Katikati) akisikiliza maelezo juu ya ufanyaji wa kazi wa mitambo inayotumika kusambaza maji toka Ruvu juu kutoka kwa Meneja Mradi toka kampuni ya WABAG Mr. Pintu Dutta wakati wa kamati ya Ushauri ya mkoa wa Dar es Salaam ilipotembelea mitambo hiyo. 

 Mkuu wa msafara wa kamati ya Ushauri ya mkoa wa Dar es Salaam Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Raymond Mushi (Kushoto) akisikiliza maelezo juu ya ramani inayoonesha usambazaji wa maji toka Ruvu Juu kwenda katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es salaam kutoka kwa Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi Dawasa Romamus Mwang’ingo.

Na Raymond Mushumbusi MAELEZO
March 1 2016
Tatizo la ukosefu wa huduma ya maji katika baadhi ya maeneo ya Jiji la Dar es Salaam linatarajiwa kuwa historia mara baada ya kukamilika kwa ujenzi wa tanki kubwa lenye uwezo wa kuhifadhi maji lita million 10 kwa siku lililopo Kibamba.
Hayo yamebainika mara baada ya wajumbe wa Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Dar es Salaam walipotembela mradi huo unaofadhiliwa na nchi ya India ambapo mbali na kujionea ujenzi wa tanki hilo pia walitembelea na kujionea ulazaji wa bomba litakayokuwa linasafirisha maji toka vyanzo vya maji vya Ruvu Chini na Ruvu Juu na kwenda kuifadhiwa katika tanki hilo tayari kwa kusambazwa katika maeneo ya Jiji la Dar es Salaam na viunga vyake.
Hata hivyo Disemba 31, 2015 Serikali ya Tanzania na India zilisaini mkataba wa ufadhili wa Dola Millioni 59.3 ili kutekeleza mradi wa ulazji wa bomba la maji kutoka Mlandizi mpaka Kimara na kuishia Kinyerezi ikiwa ni pamoja na ujenzi wa tanki hilo la Kibamba.
Mradi huo unatarajiwa kukamilika Marchi 31 mwaka huu ambapo mpaka sasa umekamilika kwa asilimia 90 ili uanze kusambaza maji katika Mkoa wa Dar es Salaam na viunga vyake.
Mkuu wa msafara wa Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Dar es Salaam alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Raymond Mushi aliyemuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Said Meck Sadiq ambaye ndio mwenyekiti wa kamati hiyo amesema lengo la kamati hiyo ni kuona Jiji zima linakuwa na huduma ya maji safi na salama kwa matumizi mbalimbali na kuondokana na suala la maji ya mgao linalolikumba Jiji la Dar es salaam kwa miaka mingi.
“ Tatizo la maji litakuwa historia katika Jiji letu maana mradi huu ni mkubwa sana na utawezesha watu wengi kupata huduma ya maji safi na salama na tutaondokana na uhaba wa maji katika baadhi ya maeneo na yale ambayo yalikuwa hayana kabisa huduma ya maji kwa kipindi kirefu sana yatapatiwa huduma hiyo”
“ Nawaomba wananchi na wafanyakazi wa Dawasco kutunza miundombinu hii kwani ni hazina kubwa si kwetu tu hata kwa vizazi vijavyo, na ni marufuku kwa watu kujenga nyumba katika eneo lilipopita bombala maji, alama maalum ziwekwe ili kuonesha kuwa sehemu hii bomba limepita ili kuzuia uharibifu wa miundombinu” Alisema Mushi.
Mara baada ya kukamilika kwa ujenzi wa tanki la Kibamba litakuwa na uwezo wa kusambaza maji katika maeneo yafuatayo; Ruvu, Kiluvya, Kibamba, Mbezi, Kimara, ubungo, Segerea, hadi kinyerezi ambapo bomba linatakuwa limeishia hapo na maeneo yote ambayo yanapata maji kupitia mtambo wa Ruvu Juu na Chini na wale amabao bado hawajaunganishwa na huduma ya maji wataunganishwa ili waweze kupata huduma hiyo kwa urahisi zaidi.
Aidha, mmoja kati ya wajumbe wa kamati ya ushauri ya mkoa wa Dar es Salaam mbunge wa viti maalum Ilala (CHADEMA) Mhe. Anatropia Theonest amesema huduma ya maji ni suala muhimu sana kwa maendeleo ya nchi yoyote, hivyo basi Serikali iliwekee uzito na kulitekeleza kwa nguvu zake zote na kuonya wale wanaohujumu miundombimu ya maji kuchukuliwa hatua za kisheria, iwe ni kwa wafanyakazi wa idara za maji au wananchi ili kuhakikisha huduma hiyo inawanufaisha wananchi.
Kamati ya ushauri ya mkoa wa Dar es Salaam inaundwa na wakuu wa Wilaya zote za mkoa wa Dar es salaam, Mameya wote, wabunge wa Mkoa wa kuchaguliwa, kuteuliwa au viti maalum na kamati hiyo inakuwa chini ya Uwenyekiti wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.

No comments: