Saa zinazoweza kutumiwa kuiba mitihani - LEKULE

Breaking

5 Mar 2016

Saa zinazoweza kutumiwa kuiba mitihani

saaSaa hizo zinauzwa katika Amazon an eBay
Saa za kisasa ambazo zimetengenezwa mahususi kutumiwa kudanganya wakati wa mtihani zimekuwa zikiwakosesha usingizi walimu na wasimamizi wa mitihani.
Saa hizo zina uwezo wa kuweka akiba data na maelezo ambayo yanaweza kusomeka mtu anapofanya mtihani.
Aidha, zina kitufe cha dharura ambacho kinaweza kubadili uso wa saa hizo haraka sana na badala ya kuonesha habari ziwe zinaonesha uso wa kawaida wa saa.
Saa hizo zinatangazwa katika soko la kuuza bidhaa mtandaoni la Amazon.
Mojawapo ya aina ya saa hizo ina uwezo wa kuweka akiba data ya 4GB. Nyingine, ambayo itaanza kuuzwa baadaye mwaka huu, itakuwa na uwezo wa 8GB na inaweza kuhifadhi hata video.
Baadhi ya saa hizo, zina kifaa kidogo sana cha kusikizia ambacho hakitumii nyaya, jambo linalowezesha mtu kusikiliza kilichohifadhiwa kwenye saa hiyo bila kuonekana.
Tangazo moja katika mtandao wa Amazon linasema mtu anaweza kununua saa ya aina hiyo kwa $61 (£43).
Kuna pia matangazo ya saa hizo eBay.
Naibu mwalimu mkuu wa shule moja kutoka Bath, Uingereza anasema saa hizo zinaweza zikawashawishi wanafunzi kuhadaa katika mtihani.
Bw Joe Sidders wa shule ya Monkton Combe Senior School amesema ingawa saa hizo zinaweza kudhibitiwa kwa kutumia sheria zinazoharamisha simu na kompyuta kutoka vyumba vya mitihani, ni changamoto kubwa sana kwa watu wanaosimamia mitihani.
Amesema uuzaji wa saa hizo unafaa kudhibitiwa.
Kuna pia “kalamu za kuiba mtihani” ambazo zinaweza kuhifadhi habari na maelezo.
Ongezeko la matumizi ya saa kuiba yamefanya baadhi ya mashirika kupiga marufuku saa katika vyumba vya mitihani Uingereza.

No comments: