RAIS
Dk. John Magufuli ameombwa kuzuia upitishwaji wa silaha za kivita
zinazodaiwa kupitishwa katika Bandari ya Dar es Salaam kwenda nchini
Burundi.
Ombi
hilo lilitolewa mjini hapa jana na vyama sita vya wanaharakati wa haki
za binadamu na kiraia vilivyowasilisha maombi yao mbele ya Kamati ya
Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) inayoendelea kusikiliza
maombi hayo mjini hapa.
Wanaharakati
hao wameiambia Kamati hiyo ya Bunge kwamba, silaha hizo zinazodaiwa
kupitia nchini Tanzania hutumiwa na Serikali ya Burundi yakiwamo makundi
ya vijana wanaodaiwa kuiunga mkono Serikali.
Mbele
ya Kamati ya Migogoro na Usuluhishi ya Bunge la Afrika Mashariki, Rais
wa Muungano wa raia wa Burundi wanaopinga muhula wa tatu wa Rais Pierre
Nkurunziza, Vilalis Nshihirimana, alidai silaha hizo zimechangia
umwagaji wa damu nchini humo.
Alisema
zipo taarifa za uhakika kuwa silaha hizo zimekuwa zikipitia Dar es
Salaam ambako kwa nchini Burundi hali ya usalama imeendelea kuzorota
huku mauaji ya raia wasio na hatia yanayofanywa na vyombo vya Serikali
ikiwamo polisi, jeshi na makundi ya vijana yakiendelea kushamiri.
“Tunamuomba Rais Magufuli na Serikali ya Tanzania wazuie silaha hizo kuingia Burundi kupita Bandari ya Dar es Salaam,” alisema Nshihirimana na kuongeza:
“Taarifa
hizi za silaha kuingia Burundi kupitia Dar es Salaam ni za uhakika na
tumezipata kutoka kwa watoa taarifa wetu ambao tunalazimika kuwalinda
lakini ni kweli silaha zinaweza kuingizwa kwa kupitia hata ndege
zinazoenda Burundi lakini ni wajibu wa kila mmoja wetu kuhakikisha kuna
usalama wa kutosha kwa wananchi wa Burundi,” alisema.
Kwa upande wake Mbunge wa EALA, Dora Byamukama kutoka nchini Uganda, aliomba kupewa ushahidi wa tuhuma hizo.
Naye
mbunge wa EALA kutoka nchini Burundi, Hafsa Mossy, aliwataka
walalamikaji hao kueleza silaha hizo ziliingizwa na akina nani na
kuwataka kuzungumzia silaha zilizozagaa na zinazotumiwa kushambulia
miundombinu na maofisa wa Serikali zinatoka wapi.
Kwa
upande wake Mbunge wa EALA kutoka Tanzania, Adam Kimbisa, aliwataka
wanaharakati hao kuacha kutoa kauli zisizo na ushahidi na zinazoweza
kuvuruga uhusiano baina ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
(EAC).
“Haya
madai ni very sensitive (nyeti mno) na isitoshe hayana ushahidi wowote
kwa kuwa hakuna arms embargo (vikwazo vya silaha) ilivyowekewa Burundi
na pia silaha zinaweza kuingizwa hata kwa kutumia usafiri wa ndege, sasa
tusianze kunyoosheana vidole wakati tunatafuta suluhu ya mgogoro wa
jirani zetu,” alisema Kimbisa.
Wanaharakati
hao wanawasilisha maombi kwa Kamati hiyo ya Bunge la EALA ya kutaka
Bunge hilo likutane kujadili na kuutolea azimio mgogoro wa kisiasa
unaoendelea nchini Burundi tangu Aprili mwaka jana baada ya Rais
Nkurunziza kutangaza azma ya kuongeza muhula wa tatu wa kuiongoza nchi
hiyo.
Wakati
wanaharakati hao wakitoa madai hayo dhidi ya Tanzania, mwishoni mwa
mwaka jana Serikali ya Burundi ilidai kukamata silaha nyingi kutoka kwa
wafuasi wa upinzani.
Ilidaiwa kuwa waliokamatwa ni wafuasi wa chama kikuu cha upinzani cha FNL kinachoongozwa na Agathon Rwasa.
Kukamatwa kwa silaha hizo kulitokana na kundi la watu wenye silaha kudaiwa kuingia nchini humo.
Ilidaiwa
wakati watu hao wakikabiliana na jeshi la nchi hiyo katika Mkoa wa
Kayanza, Kaskazini mwa Burundi, polisi walifanikiwa kukamata bunduki
thelathini katika kijiji kimoja cha Mkoa wa Muyinga, Kaskazini Mashariki
mwa nchi hiyo.
Siku chache baadaye polisi hao hao walidai kukamata silaha nyingine kutoka kwa vijana wa chama tawala cha CNDD-FDD.
Kumekuwa
na mapigano ya mara kwa mara nchini Burundi kati ya kundi la watu wenye
silaha na vikosi vya usalama na jeshi la nchi hiyo.
Pamoja
na kwamba vyombo vya usalama vimekuwa vikidai kudhibiti hali hiyo, hata
hivyo uchaguzi uliomuingiza madarakani Rais Nkurunziza hivi karibuni
umeamsha hasira kubwa hususani kutoka kwa wapinzani wake na hivyo kuzua
hali ya shaka.
No comments:
Post a Comment