Serikali Kuachana na Nguzo za Umeme za Miti - LEKULE

Breaking

13 Feb 2015

Serikali Kuachana na Nguzo za Umeme za Miti



SERIKALI imesema inaendeleza jitihada za kuachana na matumizi ya nguzo za umeme za miti, badala yake itatumia nguzo za zege ikiwa ni hatua mojawapo ya kuboresha huduma ya usambazaji na upatikanaji wa umeme nchini.
 
Hayo yalibainika mwishoni mwa wiki katika kikao baina ya uongozi wa Kampuni ya Sunshine Group Ltd na wataalamu wa sekta ya umeme kutoka Wizara ya Nishati na Madini na Shirika la Umeme nchini (Tanesco).
 
Katika kikao hicho, Kampuni ya Sunshine iliwasilisha mapendekezo ya kuanzisha kiwanda cha kutengeneza nguzo za umeme za zege kwa ajili ya matumizi ya nchini.
 
Akieleza msimamo wa Serikali kuhusu mapendekezo hayo, Kamishna Msaidizi wa Umeme, Innocent Luoga alisema Serikali ina dhamira ya kutumia nguzo za umeme zilizotengenezwa kwa zege na kuachana na za miti zinazotumika sasa kutokana na manufaa yake.
 
Luoga aliyataja manufaa ya kutumia nguzo za zege kuwa ni pamoja na uimara wa nguzo husika.
 
 “Huwezi kulinganisha uimara wa nguzo za zege na hizi za miti tunazotumia hivi sasa. Nguzo za zege ni madhubuti na imara zaidi,” alisema.
 
Akifafanua, Luoga alisema kutokana na uimara wa nguzo za zege, uhai wake ni wa muda mrefu kulinganisha na nguzo za miti.
 
“Uhai wa nguzo za zege ni kati ya miaka 70 hadi 100, wakati uhai wa nguzo za miti ni miaka 50,” alisema Luoga na kusisitiza kuwa sifa hiyo ya uhai mrefu wa nguzo za zege inazalisha manufaa mengine kwa Serikali na wananchi kwa ujumla endapo nguzo hizo zitatumika.
 
Faida nyingine za kutumia nguzo za zege, zilizotajwa na wataalamu katika kikao hicho ni pamoja na kuwa rafiki wa mazingira ambapo huepusha ukataji wa miti.
 
Nyingine ni uwezo wake wa kutopitisha maji na kutoshika moto kwa urahisi. Akihitimisha mazungumzo husika, Luoga alisema Serikali itaendelea kufanya mazungumzo na kampuni hiyo na wawekezaji wengine wenye nia ya kutengeneza nguzo za umeme za zege ili kufikia makubaliano yatakayowezesha pande zote mbili kunufaika.
 
“Mkakati wetu ni kwa Tanesco kutengeneza nguzo za zege kwa matumizi ya ndani ya nchi lakini ni vyema tukapata wawekezaji wengine watakaosaidia kutengeneza nguzo hizo kwani mahitaji ni makubwa sana,” alisema.

No comments: