Taasisi
ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), imewapandisha mahakamani
Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Evarista Kalalu na wakurugenzi wawili kwa
makosa mawili yanayohusiana na rushwa kinyume na Kifungu cha 32 cha
Sheria ya Takukuru Namba 11 ya mwaka 2007.
Katika
kesi hiyo inayowaunganisha maofisa wengine wawili wa halmashauri ya
wilaya ya Mufindi, wanatuhumiwa kuisababishia halmashauri hasara ya Sh
milioni 3.
Kesi
hiyo iliyopewa jina la kesi ya uhujumu uchumi namba moja ya mwaka
2015, ilifunguliwa jana katika Mahakama ya Wilaya ya Mufindi mkoani
hapa.
Mkuu
wa wilaya hiyo na watuhumiwa hao wengine kwa pamoja wamekana mashitaka
yao mbele ya Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Victoria Nongwa.
Watuhumiwa
wengine katika shitaka hilo ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya
Mikindani mkoani Mtwara, Limbakisye Shimwela ambaye wakati kosa hilo
likitendeka kati ya Desemba 2010 na Februari 2011, alikuwa Mkurugenzi wa
halmashauri ya wilaya ya Mufindi na mwingine ni Mkurugenzi wa
halmashauri ya Biharamulo mkoani Kagera, Nasibu Bakari.
Watuhumiwa
wengine waliofikishwa katika mahakama hiyo, kutokana na ushiriki wao wa
makosa katika kesi hiyo ni Ofisa Mipango wa Halmashauri ya Mufindi,
Cosmas Mduda na Fundi Ujenzi wa wilaya hiyo, Fedrick Zaveri.
Akisoma
shitaka linalowakabili watuhumiwa hao mahakamani hapo, Mwendesha
mashitaka wa Takukuru Mkoa wa Iringa, Imani Mizizi alidai mbele ya
Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo kuwa kati ya Desemba 2010 na Februari
2011 watuhumiwa hao kwa pamoja walikula njama ya kutenda kosa la
rushwa kinyume na kifungu cha 32 Sheria ya Kuzuia na Kupambana na rushwa
Namba 11 ya mwaka 2007.
Katika
kosa la pili, linalowakabili watuhumiwa watatu katika kesi hiyo, ambao
ni Shimwela ambaye ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mtwara/Mikindani,
Bakari ambaye ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo na
Cosmas ambaye ni fundi ujenzi, ni lile la matumizi mabaya ya ofisi
kinyume na kifungu cha 31 cha sheria kuzuia na Kupambana na Rushwa.
Ilidaiwa
mahakamani hapo kuwa kati ya Desemba 2010 na Februari 2011, watuhumiwa
hao watatu walitumia ofisi vibaya kwa kuingia mkataba na Fedrick Zaveri
kwa ajili ya ujenzi wa vyoo, bafu za kuogea na mfumo wa maji katika
shule ya sekondari ya Ihalimba bila kufuata Sheria ya Manunuzi ya Umma
ya mwaka 2004.
Ilidaiwa kuwa kutokana na hatua hiyo, watuhumiwa waliisababishia hasara ya Sh milioni tatu Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi.
Watuhumiwa
wote wamekana kosa na kuachiwa kwa dhamana baada ya kukidhi masharti ya
kila mmoja kuwa na wadhamini wawili na bondi ya Sh milioni moja kwa
kila mdhamini.
Hakimu Victoria aliahirisha kesi hiyo hadi Machi 13 mwaka huu, watu hao watakapokuja kusomewa maelezo ya awali.
No comments:
Post a Comment