Tamko la Jukwaa la Wahariri kuhusu kufutwa kwa gazeti la MAWIO - LEKULE BLOG

Breaking

Header Ads

Thursday, 21 January 2016

Tamko la Jukwaa la Wahariri kuhusu kufutwa kwa gazeti la MAWIOUTANGULIZI 
1. JUKWAA la Wahariri Tanzania (TEF) limeshtushwa na kusononeshwa na hatua ya Serikali kupitia kwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye KULIFUTA katika daftari la Msajili wa Magazeti, Gazeti la Mawio.

2. TEF inaichukulia hatua hii kama aina mpya ya ukandamizaji wa uhuru vyombo vya habari nchini. Kwa serikali zilizopita, tulikuwa tukipambana na vitendo vya kufungiwa kwa magazeti kwa muda maalum, wakati adhabu kubwa iliyowahi kutolewa ilikuwa ni ile ya kufungiwa kwa muda usiojulikana kwa Gazeti la Mwanahalisi, kabla gazeti hilo kurejeshwa kwa umma na Mahakama.

3. Uamuzi wa kulifuta Mawio (hata kama lilifanya makosa) umetufikirisha sana. Tumetafakari kwa kina na kujiuliza kwamba pengine habari ambazo ziliandikwa na gazeti hili, zilikuwa hatari kwa kiasi gani kwa nchi kiasi cha kufikiwa uamuzi huo? Ni magazeti mangapi yatafuata kufutwa baada ya Mawio ikiwa serikali itaendelea na ubabe wa aina hii?

4. Ndiyo maana tunaiona hatua ya Serikali kulifuta Mawio kama aina mpya ya ukandamizaji wa uhuru wa habari ambayo imeasisiwa na Serikali ya Awamu ya Tano, inayoongozwa na Rais John Magufuli. Tunajiuliza ikiwa kwa miezi takriban mitatu tu tangu kuanza kazi kwa serikali mpya tayari imefuta gazeti, itakuwaje katika safari ya miaka mitano (miezi 60) ambayo atakuwa madarakani?

MSIMAMO WA TEF 
TEF inapinga uamuzi wa serikali kulifuta Mawio kutokana na sababu zifuatazo:

1. Zipo kasoro nyingi za kimfumo zinazosababisha uamuzi wa Serikali kutokubalika. Hii haimaanishi kwamba vyombo vya habari havifanyi makosa, la hasha; lakini hata pale vyombo hivyo vinapofanya makosa yoyote yale, taratibu za kuyashughulikia ni kinyume kabisa cha misingi ya utawala bora, haki na demokrasia.

2. Mfumo wa sasa wa kushughulikia matatizo au kasoro za kitaaluma katika vyombo vya habari ni kandamizi kwani unamfanya Waziri kuwa “Mhariri Mkuu” na ana mamlaka ya kutoa adhabu kwa kuzingatia mtizamo wake, hata kama mtizamo huo unakinzana na misingi ya taaluma.

3. Tunauona uamuzi wa serikali kuwa na nia mbaya kwani hata katika taarifa yake kwa umma, haikuweka wazi habari ambazo zimesababisha kufutwa kwa Mawio. Badala yake taarifa ya serikali inatoa kauli ya jumla kwamba wahariri wa gazeti hilo “wameonywa mara nyingi lakini wamekuwa hawabadiliki”. Hakuna anayefahamu walionywa lini wala kuhusu nini?

4. Utaratibu uliotumika kulifuta Mawio ni uleule wa matumizi ya Sheria kandamizi ya Magazeti ya 1976 ambayo takriban kwa miaka 20 imekuwa ikipigiwa kelele kutokana na kumpa mtu mmoja (Waziri) mamlaka ya kuamua suala kubwa la kuwanyima watu wengi (kwa idadi yoyote) haki ya kupata habari. Hii ni tofauti na taaluma nyingine ambazo Serikali inaziheshimu kwa kupeleka masuala husika katika vyombo vya sheria au mabaraza ya uamuzi.

5. Kwa taaluma ya habari, Serikali bado imeendelea kujipa mamlaka ya “kukamata, kushtaki, kusikiliza kesi, kuhukumu na kufunga” Maana kama ilikuwa ni kesi iliyozaa hukumu ya kufutwa, basi uendeshaji wake ulifanyika katika “mahakama ya siri”, na usiri huu matokeo yake ni hukumu ya siri ambayo haikuwapa wahusuka kutoa utetezi wa kile kilichokuwa kikilalamikiwa dhidi yao. Hakuna anayefahamu nani alikuwa mlalamikaji katika kesi hiyo, utetezi wa washtakiwa ni upi na chombo gani kilichopima uzito wa mashtaka dhidi ya utetezi na kutoa uamuzi!.

6. Mfumo wa aina hii ni kichaka ambacho Serikali imekuwa ikikitumia kufanya kile ambacho kimeandikwa katika taarifa ya Waziri kwamba Wahariri wa Mawio walionywa mara kadhaa! Hivi walionywa na nani, wapi na kwa sababu zipi? Kama kile kinacholalamikiwa kingekuwa kimefikishwa katika chombo rasmi cha utoaji haki, kila kitu kingekuwa wazi kwa umma kwamba mashtaka ni yapi na utetezi wa washtakiwa ni upi.

7. Mwenendo wa aina hii wa kufuta magazeti iwe ni kwa muda siyo tu kwamba inaathiri dhana nzima ya utawala bora, bali inaliweka Taifa katika hatari ya kutumbukia katika uovu, hasa pale wenye dhamana watakapofanya wapendavyo kwa kuwa tu vyombo vya habari vitakuwa vimezibwa midomo.

8. Kwa kuwa hii inaonekana kuwa dhamira rasmi ya Serikali kutumia sheria kandamizi kudhibiti demokrasia na uhuru wa habari, tunatoa mwito kwa watawala wetu kutafakari upya suala hili na kuachana kabisa na dhamira hiyo isiyokuwa na tija kwa nchi yetu.

IMETOLEWA NA 
JUKWAA LA WAHARIRI TANZANIA (TEF)

DAR ES SALAAM 
Post a Comment