Makusanyo
ya mapato katika halmashauri nchini, yameongezeka kufikia asilimia 800
hadi 900 baada ya kuanza kutumika kwa mfumo wa kukusanya mapato kwa njia
ya kielektroniki katika halmashauri 164.
Hayo
yalibainishwa jana na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jaffo wakati wa mkutano wake na
waandishi wa habari mjini Dodoma
Jaffo
alisema Serikali imesanifu na kutengeneza mfumo wa kukusanya na kutoa
ankara na hati za madai kwa kodi na tozo mbalimbali katika mamlaka za
Serikali za Mitaa ili kuachana na utaratibu wa kukusanya mapato kwa
kutumia hati zinazoandikwa kwa mkono.
Alisema
tangu halmashauri kuanza kutumia mfumo wa kukusanya mapato kwa njia ya
kieletroniki, makusanyo yameongezeka kwa asilimia 800 hadi 900, hali
ambayo inadhihirisha ukusanyaji mapato kwa njia ya stakabadhi za
kuandikwa kwa mikono fedha nyingi zilikuwa zikipotea.
Alisema
msingi wa kuanzishwa kwa matumizi ya mfumo huo ni kuanzisha matumizi ya
benki ya TEHAMA katika kukusanya kodi na tozo mbalimbali na kuachana na
utaratibu wa kukusanya mapato hayo kwa kutumia stakabadhi za kuandikwa
kwa mkono, ambao hutengeneza mianya ya wizi na ubadhirifu wa fedha.
Alisema
mfumo huo umekusudia kurahisisha utoaji wa stakabadhi na utunzaji
kumbukumbu na kudhibiti upotevu wa mapato katika vyombo vinavyokusanya
fedha za umma.
Alisema
serikali iliagiza ifikapo Julai 1, 2015, halmashauri zote ziwe zimeanza
matumizi ya ukusanyaji wa mapato kwa mfumo wa kielektroniki, lakini
ilipofika tarehe hiyo halmashauri 51 sawa na asilimia 28.18 ya
halmashauri zote nchini, ndizo zilikuwa zimetekeleza agizo hilo.
Aidha,
hadi mwanzoni mwa Desemba 2015 ni halmashauri 86 pekee sawa na asilimia
47.78 ndizo zilikuwa zimeingia katika hatua mbalimbali za utekelezaji
wa agizo la serikali licha ya kupewa muda hadi Desemba 31, 2015.
Alisema
kutokana na kusuasua kwa zoezi hilo la serikali, ndipo agizo la
msisitizo lilitolewa na Ofisi ya Rais Tamisemi kuwa ifikapo Januari 10,
mwaka huu halmashauri zote ziwe zimeingia katika mfumo huo; hivyo hadi
Januari 12, halmashauri 164 sawa na asilimia 90.6 zimeingia katika hatua
mbalimbali za ufungaji na matumizi ya mfumo.
Pia
halmashauri 17 mpya sawa na asilimia 9.4, hazijaanza mchakato wa
kufunga mfumo kwa sababu mbalimbali, zikiwemo kutokuwa na ofisi ya
kudumu, kutofikiwa na Mkongo wa Taifa, umeme na zingine hazijagawana
mali na halmashauri mama. Alizitaka zijipange kufunga mfumo huo.
No comments:
Post a Comment