Waziri
wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, amesema serikali inatarajia
kukusanya kiasi cha Sh. trilioni 1.3 ndani ya mwezi huu pekee.
Aidha,
amesema ili kuhakikisha serikali inapata mapato ya kutosha, atasimamia
vyema suala la kukusanya kodi zinazostahili na kutengeneza mazingira ya
watu kulipa kodi.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana katika viwanja vya Ikulu mara baada ya
kuapishwa, Dk. Mpango alisema kwa kipindi cha mwezi mmoja serikali
inaweza kukusanya kiasi hicho cha fedha.
“Nimekaa
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kwa kipindi cha wiki tatu, nimeona
kuwa kiasi hiki cha Sh. trilioni 1.3 kinaweza kukusanywa. Kwa wiki
iliyopita ya sikukuu, niliona makusanyo ni mazuri na mpaka ifikapo
mwisho wa mwezi huu, tutatimiza kiasi hicho,” alisema.
Ulipaji Kodi
Akizungumzia
suala la wafanyabishara kukwepa kodi, alisema hakuna serikali inayoweza
kujiendesha duniani kote bila kukusanya kodi.
Alisema: “Kipengele
cha kwanza, wale wanaokwepa kodi tutawabana ili walipe kodi
inayostahili, ni lazima Watanzania wajenge utaratibu wa kulipa kodi
halali na kwa hiari,” alisema Dk. Mpango.
Alisema serikali itafanya marekebisho ya mfumo wa kodi ili wafanyabiashara wafanye biashara zao vizuri.
“Kama
hakuna mfumo wa kuwafanya wafanyabiashara wakubwa kulipa kodi,
tutaendelea kuwakamata wafanyabishara wadogo wadogo wale wale kila
siku,” alisema.
Kadhalika
aliweka wazi lengo la serikali kuwaondolea kodi za kero wafanyabishara
wadogo wadogo kama mama lishe, wauza vitumbua na wauza samaki .
Changamoto zilizopo TRA
Akizungumzia
changamato alizobaini akiwa TRA kwa kipindi cha siku 27, alisema wapo
watumishi wasiowaaminifu ambao anaamini wako katika sekta mbalimbali
nchini.
“TRA
kuna watendaji wazuri wanaofanya kazi kwa weledi, lakini kuna wale
wachache ambao wanaharibu sifa ya TRA na hao tutahakikisha tunawaondoa
ili kufikia lengo la kukusanya kodi kwa uaminifu,” alisema.
Alisema
changamoto iliyopo ni baada ya kutokea kwa kashfa ya ukwepaji kodi
watendaji wa TRA wote kwa sasa wanaonekana kuwa ni waovu.
Malengo ya Rais Magufuli
Akizungumzia
malengo na ahadi za Rais Magufuli alizowaahidi Watanzania ikizingatiwa
kuwa, wizara hiyo ndio yenye dhamana kubwa ya utekelezaji alisema yote
yatatekelezeka kama watendaji watatimiza majukumu yao.
Alisema
kila kiongozi akisimamia vema jukumu lake alilopewa na wizara yake
ikikusanya kodi inayotakiwa kwa wakati, mambo yote aliyoahidi rais
yatatekelezeka ikiwamo elimu bure kuanzia elimu ya awali hadi kidato cha
nne na milioni 50 katika kila kijiji nchi nzima.
“Ni
lazima tufanye kazi kwa bidii na maarifa ambayo Mungu ametujalia na
kuwa na nidhamu kwa kila jambo tunalolifanya kwa Watanzania wote,
tusingoje watu wengine waje watujengee nchini yetu,” alisema.
Kuongezeka kwa Thamani ya Shilingi
Dk.
Mpango akizungumzia namna wizara yake itakavyowezesha thamani ya
shilingi kupanda, alisema suala hilo linawezekana kwa kuongeza nguvu
kwenye kuuza bidhaa za kutosha nje ya nchi.
“Kitaalam
ili kuongeza thamani ya shilingi yetu, tunaweza kuiongezea nguvu hasa
kwa kuuza bidhaa za kutosha nje ya nchi ili kupata fedha za kigeni za
kukidhi mahitaji ya watu ya kuagiza bidhaa,” alisema.
Alisema pia ni muhimu kutilia mkazo uzalishaji wa bidhaa nyingi zinazoliingizia taifa fedha za kigeni.
Alitaja biashara hizo kuwa ni utalii unaoliingizia taifa fedha za kigeni, biashara na nchi jirani na mazao yenye thamani kubwa.
Alisema pia ni vema kulisimamia soko la fedha na benki kuu ili viwango vya kukopa vishuke na kusimamia ipasavyo sekta ya fedha.
“Haya
yanawezekana chini ya Gavana wa Benki Kuu, Prof. Benno Ndulu, ambaye
anasimamia vema sekta hiyo ili viwango vya kukopa vishuke na Watanzania
wafundishwe kujiwekea akiba na kukopa kupitia saccos, benki na vicoba,” alisema.
Namna ya kukuza Uchumi wa Nchi
Dk.
Mpango, alisema ili kukuza uchumi wa nchi ni lazima kuwa na utaratibu
wa kujenga viwanda vikubwa nchini vinavyozalisha kwa wingi jambo
litakaloongeza pato la taifa.
“Nchini
kwa sasa kuna kiwanda kimoja kikubwa cha Bia cha Breweries (TBL)
ambacho ndicho tunakitegemea ndio maana bei ya vileo vinapanda kila
siku. Lakini vingekuwapo kama hivyo 10, nina uhakikisha tungekusanya
mapato ya kutosha,” alisema.
Aibu ya kuomba misaada nje
Dk. Mpango, alisema miongoni mwa mambo yanayomnyima raha ni safari za kwenda ughaibuni kuomba misaada kwa nchi wahisani.
Alisema
kitendo hicho ni cha aibu na kwa muda mrefu kimekuwa kikimsonesha
moyoni hasa kwa kuwa anafahamu kuwa taifa lake lina utajiri mkubwa.
"Nimekwenda
nje mara nyingi nikiongozana na mawaziri wa fedha waliopita kwenda
kuomba misaada.Huwa najisikia aibu sana,tunadhalilika sana.
"Hatuna
sababu ya kuwa ombaomba,tunachotakiwa kukifanya ni kuimarisha mfumo wa
ukusanyaji kodi na kuwaondolea mzigo wananchi wa hali ya chini," Alisema Dr. Mpango
No comments:
Post a Comment