Mawaziri wa Afrika Mashariki Watoa Maazimio Matatu Kuhusu Mgogoro wa Burundi - LEKULE

Breaking

19 May 2015

Mawaziri wa Afrika Mashariki Watoa Maazimio Matatu Kuhusu Mgogoro wa Burundi


MAWAZIRI wa Afrika Mashariki kutoka nchi tano za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), walikutana jana kwa saa 1:08 asubuhi jijini Arusha kujadili hali ya uchaguzi nchini Burundi kutokana na maazimio matatu.
 
Miongoni mwa maazimio hayo ni kuitaka Tume ya Uangalizi ya Uchaguzi wa Burundi kutoka nchi za EAC, inayoongozwa na Jaji Joseph Warioba kuendelea na kazi hiyo nchini humo mara moja.
 
Aidha, imeazimiwa kuwa, Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa EAC, Dk Harrison Mwakyembe na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya EAC, Dk Richard Sezibera kutembelea Burundi mapema iwezekanavyo kwa lengo la kujionea hali halisi katika nchi hiyo.
 
Kikao hicho cha dharura kilichofanyika makao makuu ya EAC jijini Arusha kuanzia saa 6:12 mchana na kumalizika saa 7:24 mchana huo kikiwa chini ya uenyekiti wa Dk Mwakyembe, kilihudhuriwa na karibu mawaziri wote wanaoshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, isipokuwa, Valentine Rugaine wa Rwanda ambaye haikuelezwa sababu za kushindwa kushiriki.
 
Dk Sezibera alizungumza na wanahabari na kusema moja ya mambo yaliyojadiliwa katika kikao hicho ni pamoja na kupokea taarifa ya kikao cha wanasheria wakuu wa nchi za EAC, kilichofanyika mwishoni mwa wiki jijini hapa. 
 
“Baraza la mawaziri limepokea taarifa ya kikao cha wanasheria wakuu wa nchi za EAC kilichokuwa na lengo la kujadili hali ya Burundi.
 
“Taarifa hii iliyowasilishwa itakabidhiwa kwa wakuu wa nchi za EAC katika mkutano wa makuu hao unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni,” alisema.
 
Kwa mujibu wa Dk Sezibera baraza hilo la mawaziri, liliazimia mambo makuu matatu, ikiwa ni pamoja na Tume ya Jaji Warioba kuendelea na kazi hiyo nchini Burundi, Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa EAC na Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo kutembelea Burundi, huku mawaziri wa EAC wakipewa jukumu la kutembelea kambi za wakimbizi zilizopo Rwanda na Tanzania kwa lengo la kujionea hali halisi ya maisha ya wakimbizi katika kambi zote zilizopo katika nchi hizo.
 
Awali, Waziri anayeshughulikia Afrika Mashariki kutoka Burundi, Leontine Nzeyimana aliwataka wananchi wa Burundi kuwa watulivu katika kipindi hiki cha kuelekea katika uchaguzi mkuu.
 
Aidha, aliwataka wananchi hao kutambua kuwa Burundi ni mali yao na hawana nchi nyingine, hivyo ni vyema wakawa na subira kwa kuwa uchaguzi upo pale pale.
 
Kikao hicho cha dharura ni mwendelezo wa vikao vya kutafuta suluhu ya machafuko ya kisiasa, yanayoonekana kuinyemelea Burundi hasa baada ya Rais Pierre Nkurunziza kutangaza kuwania urais kwa awamu ya tatu katika uchaguzi mkuu wa mwezi ujao.
 
Uamuzi huo unapingwa na makundi kadhaa na wiki iliyopita Nkurunziza alinusurika kupinduliwa na mahasimu wake.

No comments: