MBUNGE wa Viti Maalum (CCM), Munira Mustafa Khatib, ameitaka serikali kukifutia usajili Chama cha Wananchi (CUF), kwa madai kuwa kimekuwa kikishiriki katika matukio ya kupigwa na kuharibu mali za wananchi visiwani Pemba.
Mbunge huyo alitoa kauli hiyo jana, alipokuwa akiuliza swali la nyongeza katika kipindi cha maswali na majibu bungeni.
“Kutokana
na kuwapo matukio ya wananchi kupigwa hususan wanachama wa CCM, ni
kwanini serikali isikifutie usajili chama cha CUF kwakuwa ndio chanzo
cha matukio hayo visiwani pemba,”alihoji Mbunge huyo.
Katika swali
la Msingi la Mbunge wa Chambani (CUF), Yusufu Salim Hussein, naye
alihoji kama serikali inatambua tatizo la raia kupigwa na kuharibiwa
mali zao kwa upande wa Zanzibar, ambalo limekuwa likiongezeka siku hadi
siku na hatua gani zimechukuliwa.
Kutokana na masuala hayo,
wabunge walionekana wakisimama kuuliza maswali ya nyongeza na Mbunge wa
Viti Maalum (CCM), Tauhida Cassian Nyimbo, alihoji serikali inachukua
hatua gani kwa viongozi wa CUF ambao wamekuwa wakitoa kauli za vitisho
kupitia mitandao ya kijamii na kuwafanya wananchi visiwani humo kuwa na
hofu hasa kipindi hichi cha kuelekea sikukuu ya Idd el Fitri.
Naye
Mbunge wa Dimani (CCM), Hafidh Ali Tahir, alihoji ni kwa namna gani
serikali itawashughulikia baadhi ya viongozi ambao wamekuwa na tabia ya
kuvunja sheria na maagizo ya viongozi kuhusu mikutano ya hadhara.
Akijibu
maswali hayo, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yusuf
Masauni, alisema serikali inatambua kwamba kila unapofika wakati wa
Uchaguzi Mkuu hasa katika kisiwa cha Pemba, baadhi ya watu hujichukulia
sheria mkononi kwa kuwapiga wengine na kuharibu mali zao.
Kutokana
na hali hiyo, alisema serikali itaendelea kuongeza vikosi vya ulinzi na
usalama katika maeneo yote tete na kuhakikisha utii wa sheria bila
shuruti unazingatiwa.
“Pia serikali itaendelea kuwaelimisha
wananchi madhara ya kujichukulia sheria mikononi dhidi ya wengine wasio
na hatia,” alisema Masauni.
Alitoa wito kwa wananchi wote kuacha
mihemko ya itikadi za kisiasa wakati na kabla ya uchaguzi kwani hatua
kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Kuhusu viongozi
wanaokiuka maagizo ya serikali kuhusu mikutano ya kisiasa, Masauni
alisisitiza mikutano hiyo haitakiwi kwa wakati huu hadi hapo polisi
itakapoona inafaa na kuvitaka vyama vya siasa kutii maagizo ya serikali.
“Hakuna
mtu ambaye yuko juu ya sharia. Wale watakaoleta ukorofi watachukuliwa
hatua kali bila kujali kama ni kiongozi wa aina gani na mahali gani
anatokea. Lazima sheria ichukue mkondo wake,” alisema.
Kuhusu
suala la kukifuta CUF, Naibu Waziri huyo alisema jukumu hilo si la
serikali bali limo mikononi mwa Msajili wa vyama vya siasa, ambaye
anatakiwa kuliangalia kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo.
Aidha,
alisema nchi iko salama na serikali itaendelea kuhakikisha amani na
utulivu vinakuwapo wakati wa sikukuu hiyo na kuwataka wananchi kupuuza
kauli za uchochezi zinazotolewa na wanasiasa.
Baada ya kipindi
hicho, Mbunge wa Mwibara, (CCM), Kangi Lugola, aliomba mwongozo kwa
Naibu Spika akisema ni kwa nini serikali ipo bungeni; isitoe majibu
kuhusiana na matukio yanayofanywa na CUF ambayo mbunge mwenzake
amependekeza kifutiwe usajili na badala yake inatoa jukumu kwa msajili
wa vyama vya siasa wakati ni sehemu ya serikali.
Kutokana na
mwongozo huo, Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, alisema atatoa
majibu ya mwongozo huo baada ya kupitia sheria ya vyama vya siasa
inasemaje.
No comments:
Post a Comment