WATENDAJI
12 wa serikali ya Zanzibar, akiwamo Naibu Mhasibu Mkuu wa Serikali
wamesimamishwa kazi kutokana na upotevu mkubwa wa fedha.
Akizungumza na waandishi wa habari visiwani Zanzibar jana, Waziri wa
Fedha na Mipango, Dk. Khalid Salum Mohamed, alisema kati ya watendaji
hao wamo wahasibu wakuu wa wizara sita wanaohusika na upotevu huo wa
fedha.
“Kwa masikitiko makubwa naomba kutoa taarifa kuwa tumebaini
upotevu wa fedha za serikali ambao tumeanza kuuchukulia hatua,” alisema
waziri huyo.
Alisema upotevu huo wa fedha unaonekana sio wa
bahati mbaya, bali ni jambo la kupangwa na umetekelezwa kwa njama za
watendaji wa vitengo vya fedha uliowahusisha wahasibu.
Aidha,
alisema hadi sasa kuna hundi zenye thamani ya Sh. milioni 571
zimeshindwa kulipwa kwa sababu ya uhalifu huo na hatua za awali za
kutathmini upotevu huo zinaonyesha kuwa kiasi ambacho kinahusika na wizi
huo kinaweza kuwa kikubwa zaidi ya hicho.
“Tulipopata taarifa za awali juu ya upotevu huu hatua za haraka zilichukuliwa na kubaini wahusika wakuu”alisema Dk. Khalid.
Alisema
taarifa za awali zinaonyesha upotevu huo wa fedha umetokana na njama za
baadhi ya watendaji wa kitengo cha malipo katika Wizara ya Fedha na
Mipango wakishirikiana na baadhi ya wahasibu wa wizara tofauti za
serikali.
Waziri huyo alisema hatua hiyo imezingatia matakwa ya
Sheria ya Fedha za Umma namba 12 ya mwaka 2005 na kanuni zake na Sheria
ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2014 na kanuni zake.
Alisema kutokana
na ukubwa wa upotevu huo wa fedha, hatua itakayofuata ni kuundwa kwa
bodi ya uchunguzi ambayo itakuwa na watu wanne watakaoteuliwa na Katibu
Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango.
Alisema azma ya serikali ni
kuimarisha utawala bora na kuimarisha usimamizi wa fedha za umma, hivyo
watendaji wote wanapaswa kufahamu kuwa azma hiyo inatekelezwa bila ya
kuyumba wala kumuonea haya mtu yeyote.
No comments:
Post a Comment