Hakuna Uhamisho Wanafunzi Wapya wa Kidato cha Tano - LEKULE

Breaking

29 Jun 2016

Hakuna Uhamisho Wanafunzi Wapya wa Kidato cha Tano


SERIKALI imesema shule zote zenye nafasi za wanafunzi wa kujiunga na kidato cha tano mwaka huu, zimejaa hivyo hakuna nafasi ya mwanafunzi kubadilishiwa shule au mchepuo aliochagua.

Hayo yalibanishwa jana katika taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari mjini hapa na Msemaji wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Rebecca Kwandu.
 
Kwandu alisema baada ya serikali kutangaza wanafunzi waliojiunga na kidato cha tano, baadhi ya wazazi na wanafunzi wamekuwa wakifika ofisi za Tamisemi kuomba kubadilishiwa shule au tahasusi (michepuo) walizochaguliwa.
 
“Tunapenda kuwaarifu kwamba shule zote zenye nafasi za wanafunzi wa kujiunga na kidato cha tano mwaka 2016 zimejaza, hivyo hakuna kinachoweza kubadilishwa,” alisema Kwandu.
 
Aidha, Kwandu alisema vigezo ambavyo vilitumika katika uchaguzi huo ni pamoja na ufaulu na uchaguzi wa wanafunzi wenyewe juu ya masomo wanayopenda kuendelea nayo kidato cha tano na sita.
 
“Kulingana na utaratibu uliowekwa na serikali, mwanafunzi mwenye sifa za kuchaguliwa kuendelea kidato cha tano na vyuo vya ufundi ni yule ambaye ufaulu wake ni kuanzia daraja la kwanza hadi la tatu. Wanafunzi hao wamepangwa kulingana na ufaulu wao masomo waliyochagua na nafasi zilizopo,” alisisitiza.
 
Pia alisema nafasi za shule walizopangiwa wanafunzi zimezingatia miundombinu ya shule husika na uwezo, na kwamba kila shule imepewa wanafunzi kulingana na nafasi zilizopo, hivyo hakutakuwa na nafasi ya kuwabadilisha kutoka shule moja kwenda nyingine kwa sasa.
 
Kutokana na hali hiyo, aliwataka wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano na vyuo vya ufundi kuripoti katika shule na vyuo walivyopangiwa kama walivyoelekezwa.
 

Alisema mwanafunzi ambaye hataripoti ifikapo Julai 24, ambayo ni tarehe ya mwisho kwa muda uliopangwa, atakuwa amepoteza nafasi yake kwa kuwa itachukuliwa na mwanafunzi mwingine ambaye hakupata nafasi awali.

No comments: