UKAWA Watishia Kumpeleka Rais Magufuli Katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) - LEKULE

Breaking

29 Jun 2016

UKAWA Watishia Kumpeleka Rais Magufuli Katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC)



Wabunge wa Ukawa wamemtaka Rais John Magufuli kutoa tamko juu ya uvunjifu wa haki za binadamu Zanzibar na kwamba wana mpango wa kumpeleka katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) wakidai yanayotokea visiwani humo yana baraka zake. 

Katika mkutano wao na wanahabari jana, wabunge hao wamemtaka Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba kwenda Zanzibar kujionea hali halisi badala ya kupata taarifa kutoka kwa wasaidizi wake. 
Hata hivyo, CCM imesema kuwa inalaani tamko hilo na kuwa kama Ukawa wanaona kuna masuala yanayohitaji kurekebishwa na kuhitaji hatua za haraka za Serikali watumie vyombo vinavyotambulika kisheria kama Bunge badala ya kuishia kulalamika “vichochoroni”. 
Akitoa tamko la wabunge hao jana, Mbunge wa Vunjo (NCCR-Mageuzi) alieleza kuwa hali ya kiusalama inazidi kuwa mbaya Pemba na Unguja baada ya uchaguzi wa marudio wa Machi 20 kutokana na baadhi ya wananchi kupigwa na vikosi alivyodai ni vya usalama. 
Mbatia alisema kuwa vikosi vya ulinzi hususani jeshi la polisi vimekuwa vikishiriki katika vitendo vya ukiukwaji wa haki za raia Pemba kwa zaidi ya miezi miwili kwa polisi kupiga mabomu ya machozi, kuwakamata ovyo wananchi, kuwapiga na kuwatesa na kisha kuwafungulia mashtaka bandia. 
Kutokana na vitendo hivyo, Mbatia alisema wabunge wa Ukawa wanapenda kusikia kauli ya wazi ya Dk Magufuli juu ya uonevu huo uliodumu kwa muda mrefu dhidi ya Wazanzibari na kutoheshimiwa haki za binadamu zikiwamo za kutoa maoni na kujikusanya. 
Mbatia, ambaye ni Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, alisema Rais anapaswa kutimiza wajibu wake kuhakikisha usalama wa raia kama anavyotakiwa kikatiba na kuhakikisha polisi wanawalinda wananchi na siyo kuwaonea. 
 
“Ukawa inasema wazi kuwa inaendelea kukusanya taarifa za vitendo vya ubakaji wa demokrasia na haki za binadamu ili kupata ushahidi wa kutosha wa kumfikisha Dk Magufuli ICC akajibu makosa hayo,” alisema Mbatia. 
Katika mkutano huo uliohudhuriwa na wabunge 66 waliosaini tamko hilo, Mbatia alisema Ukawa inamtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Ernest Mangu kuitoa amri ya kusitishwa kwa matendo hayo na achukue hatua dhidi ya askari wake ambao huwatesa raia ili kurudisha imani kwa wananchi. 
Alisema wananchi wa Pemba na Unguja waendelee kuikataa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa amani na pia wadumishe utaratibu wa kuheshimu sheria na kujizuia kufanya vitendo vya kukinzana na sheria. 
Lakini alipotakiwa kuzungumzia tamko hilo, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai alitupa lawama zote kwa Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad. 
Alisema kuwa ndiye adui mkubwa wa Ukawa baada ya kususia uchaguzi wa marudio na kuhamasisha wananchi wasiitambue Serikali na sasa wafuasi hao wanatekeleza maagizo hayo kwa kukata mazao na kuleta fujo kwa wananchi wenzao. 
“Kazi ya dola ni kuhakikisha mtu havunji amani. Watu wanaofanya vitendo hivyo washughulikiwe ipasavyo na vyombo vya dola,” alisema Vuai. 
Alisema hakuna sababu ya kumpeleka Rais Magufuli katika mahakama ya ICC kwa kuwa anafanya kazi nzuri ya kuongoza nchi na kwamba kauli zilizotolewa na Ukawa ni za kitoto. 
Alivisihi vyombo vya dola kuendelea kuimarisha usalama visiwani humo ili watu wenye nia mbaya wasizoroteshe amani kutokana na matakwa ya viongozi wao. 

Awali katika mkutano huo, Mbunge wa Malindi (CUF), Ally Saleh alisema wameamua kutoa tamko hilo kutokana na hali kuzidi kuzorota Pemba na kwamba ni lazima Serikali itekeleze wajibu wake kuzuia machafuko zaidi. 
Kuhusu mipango yao ya kumshtaki Rais, alisema kesi hiyo haina haraka kwa kuwa hata wajukuu zao wanaweza kuifungua kwa kuwa makosa ya jinai hayafi. 

“Baada ya kukusanya ushahidi wa kutosha na kujiridhisha kufanya hivyo, tutafanya. Tanzania siyo kisiwa ulimwengu mzima unaangalia nini kinaendelea Zanzibar, hivyo tusipowajibika, dunia itatuwajibisha,” alisema Saleh. 
Mbunge wa Chambani (CUF), Yusuph Salim Hussein alisema vyombo vya usalama vimekuwa vikiwatuhumu wafuasi wa CUF kufanya vurugu hizo lakini tangu zianze tuhuma hizo hakuna mtu hata mmoja aliyewahi kushtakiwa kwa uharibifu mali au fujo. 
“Tangu mwaka 1992 hizo tuhuma kuwa sasa hakuna mtu aliyewahi kushtakiwa mahakamani na kutiwa hatiani. Ni wao (Serikali) ndiyo wanawaonea wananchi,” alisema. 
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yusuph Masauni alisema ni jambo la kusikitisha kuona viongozi wanawalinda wahalifu badala ya kuhimiza amani na usalama. 
Masauni alisema baada ya uchaguzi wafuasi wetu ndiyo wanafanya fujo hadi Machi 20 hali ilikuwa shwari Pemba laki ni viongozi wa CUF ndiyo chanzo cha matukio ya uhalifu unaoendelea Pemba baada ya Maalim Seif kwenda visiwani huko na kuwataka wasiitambue Serikali. 
“Hivi kabla ya tamko la Maalim Seif vikosi vya ulinzi na usalama havikuwapo ili vikakate mikarafuu na kuchoma nyumba za watu? Askari wetu wamefunzwa vizuri, wamekula kiapo kulinda usalama wa raia wote bila kujali chama,” 

Alisema nchi haiwezi kuendeshwa kwa kuacha watu wavunje amani na kwamba vyombo vya usalama vitamshughulikia mtu yeyote atakayekiuka sheria bila kujali chama.  

No comments: