Hukumu
ya kesi ya mauaji ya mwandishi wa habari wa kituo cha televisheni cha
Channel 10, Daudi Mwangosi itatolewa Julai 21 baada ya Mahakama Kuu
kusikiliza majumuisho na maoni ya Baraza la Wazee. Kesi hiyo inamkabili
askari wa kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) mkoani Iringa, Prisifius
Simon.
Akitoa
majumuisho ya kesi hiyo jana, Jaji Paul Kihwelo alisema ni wajibu wake
kutoa majumuisho kwa kuangalia mazingira na ushahidi uliomgusa moja kwa
moja mtuhumiwa.
Jaji Kihwelo alieleza mahakama kuwa askari huyo anatuhumiwa kufanya mauaji hayo kwa kukusudia Septemba 2, 2012.
Alieleza
kuwa jukumu la kuthibitisha kosa kwa mtuhumiwa ni upande wa mashtaka na
wanatakiwa wathibitishe bila kuacha wasiwasi wowote na si jukumu la
upande wa pili kuthibitisha kuwa mtuhumiwa hakutenda kosa.
Alitaja
vielelezo ambavyo vilitolewa mahakamani bila kupingwa kuwa ni pamoja na
ramani ya tukio, taarifa ya uchunguzi ya kifo cha marehemu, ungamo la
mtuhumiwa na kitabu cha kuchukilia silaha ofisi za FFU.
Akisoma
majumuhisho kwenye upande wa ungamo, Jaji Kihwelo alisema maungamo
yanayofanywa mbele ya mlinzi wa amani, yanaweza kutumika kutoa ushahidi.
Mtuhumiwa
huyo alieleza mahakama wakati akitoa ushahidi wake kuwa kabla ya kufika
kwa mlinzi wa amani, aliitwa kuhojiwa na RPC na RCO ndipo akaenda
kufanya ungamo na kwamba hakufanya chochote zaidi ya kuambiwa asaini.
Akitoa
maoni yake mmoja wa wazee wa mahakama, Khadija Husein alisema baada ya
kusikiliza mashahidi wa pande zote kuanzia mwanzo hadi mwisho,
wamegundua kuwa mtuhumiwa alienda kufanya ungamo kwa mlinzi wa amani
akiwa huru na kusaini.
Khadija
alisema si rahisi mtu kusaini kitu ambacho hajakitolea maelezo, hivyo
alichokisaini ndicho alichokitenda na alitoa ungamo akiwa huru bila
kupigwa wala kutishiwa
Alisema
endapo maelezo hayo yalikuwa si yake, yangepingwa mbele ya mahakama na
wakili wake au yeye mwenyewe, lakini kwa kuwa yalipokelewa bila kupingwa
hivyo ana hatia ya kutenda kosa bila kukusudia.
Mzee
mwingine, Said Mbaga alipingana na maelezo hayo, akisema mtuhumiwa hana
hatia kwa sababu shahidi wa kwanza hakuthibitisha kuwa alitenda kosa
kwa sababu hakumuamuru kupiga bomu.
Mzee
wa tatu, Sophia Ng’anguli alisema mtuhumiwa alitenda kosa bila
kukusudia licha ya ushahidi wa upande wa mashtaka kuacha mashaka.
Alidai
kitu cha msingi kinachomfunga mshitakiwa ni ungamo alilolitoa kwa
mlinzi wa amani, ambalo aliandika na kusaini huku akikiri na kujutia
kusababisha kifo cha Mwangosi.
No comments:
Post a Comment