BUNGE
limepitisha kwa kauli moja Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali
Namba 2 ya mwaka 2016 ambayo pamoja na mambo mengine, imeongeza adhabu
kwa watu wanaowapa mimba au kuoa ama kuolewa na mwanafunzi, sasa
watafungwa jela miaka 30.
Sheria
hiyo ilipitishwa jana bungeni mjini Dodoma baada ya Muswada
kuwasilishwa Juni 24, mwaka huu na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG)
ambao baadhi ya wabunge walipata fursa ya kuuchangia.
Muswada
huo ulilenga kufanya marekebisho katika sheria 21 kwa lengo la kuondoa
mapungufu yaliyobainika wakati wa utekelezaji wa sheria hizo na
umepitishwa kuwa sheria.
Sheria
zilizopendekezwa kurekebishwa na sheria hiyo ni pamoja na ya Kudhibiti
Utakatishaji wa Fedha Haramu; Kudhibiti Usafirishaji Haramu wa Binadamu;
Kanuni za Madai; Usajili wa Makandarasi; Elimu; Ajira na Mahusiano
Kazini na Sheria ya Taasisi za Kazi.
Muswada
huo uliowasilishwa bungeni na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George
Masaju unatamka adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela katika marekebisho
ya Sheria ya Elimu kwa watakaompa mimba, kumuoa au kuolewa mwanafunzi.
Awali
adhabu iliyotamkwa katika sheria hiyo ya elimu ni mshitakiwa akibainika
kuwa na kosa kutozwa faini ya Sh 500,000 na iwapo ni kosa la pili
anatozwa faini ya Sh 500,000 au kifungo kisichozidi miaka mitatu.
Akiizungumzia
sheria hiyo inayosubiriwa kusainiwa na Rais John Magufuli, Masaju
alisema inawalinda watoto wote chini ya miaka 18 walioko na wasio
shuleni na kuwa kosa hilo likifanywa na mtoto atahukumiwa kwa mujibu wa
sheria ya mtoto.
Kifungu
cha 60 A (i) kimeeleza kuwa itakuwa kinyume cha sheria katika mazingira
yoyote yale kwa mtu yeyote kumuoa au kuolewa na mwanafunzi wa shule ya
sekondari au ya msingi na atakayekiuka atafungwa jela miaka 30.
Katika
Sheria ya Taasisi za Kazi inataka mwajiri anapokiuka masharti ya sheria
ya kazi, ikiwa ni pamoja na kuchelewesha michango ya waajiriwa, kutoza
faini na Ofisa wa Kazi ya papo kwa hapo isiyopungua Sh 100,000.
Wakichangia
muswada huo, wabunge wameonesha furaha yao juu ya Sheria ya Elimu
inayohusu adhabu ya miaka 30 jela. Hata hivyo, pamoja na furaha hiyo,
baadhi ya wabunge wametoa angalizo la kutaka kupimwa kwanza DNA kabla ya
kutoa hukumu huku wengine wakitaka kuwapo kwa nyongeza ya viboko.
Mbunge
wa Geita Mjini, Constantine Kanyasu (CCM) alipongeza marekebisho hayo
na kutaka adhabu ya miaka 30 iongezwe na kuchapwa viboko 12 kila mwezi
mpaka aliyehukumiwa anamaliza kifungo kutokana na wahalifu hao kuwa na
mazoea ya kuzoea gereza.
Naye
Mbunge wa Viti Maalumu, Subira Mgalu (CCM) alisema pamoja na serikali
kuja na marekebisho hayo pia waangalie namna ya kukabiliana na utoro
shuleni ili kuwafanya wanafunzi kupata elimu.
Kwa
upande wake, Mbunge wa Njombe Kusini, Edward Mwalongo (CCM) alitaka
sheria imtake anayekutwa na kosa hilo kuacha fedha za fidia ambazo mama
atazitumia wakati mwanaume akiwa jela.
Akijibu
hoja ya kutumika kwa vipimo vya vinasaba (DNA), Masaju alisema kwa sasa
utaratibu wa vipimo hivyo utatumika mahakamani na waendesha mashitaka
kuhakikisha hawaachi shaka kwenye ushahidi kutokana na Tanzania kutokuwa
na uwezo wa kumpima DNA mtoto akiwa tumboni.
Kuhusu
Sheria ya Taasisi za Kazi, Mbunge wa Viti Maalumu, Hawa Chakoma (CCM),
alitaka adhabu hiyo kuongezwa ili sheria kuleta tija na kutaka kazi ya
kutoza faini hiyo isifanywe na Ofisa wa Kazi kama ilivyotamkwa katika
sheria badala yake ifanywe na Mamlaka ya Usimamizi wa Mifuko ya Jamii
(SSRA) kutokana na mifumo mizuri ya ufuatiliaji.
Akijibu
hoja hiyo, Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu,
Jenista Mhagama alisema serikali imekuja na sheria hiyo ili kuwabana
waajiri wanaochelewesha michango ya waajiriwa na kuwa katika kutekeleza
sheria waziri ataweka makundi na kuwa kampuni zenye kipato kikubwa
adhabu yao itakuwa kubwa zaidi.
No comments:
Post a Comment