Bunge
limesimamisha utekelezaji wa miradi yote mipya ya Shirika la Taifa la
Hifadhi ya Jamii (NSSF) mpaka hapo Kamati na Wizara itakapopitia taarifa
ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG), sambamba na
kuitisha taarifa za utekelezaji wa miradi yote iliyofanywa na mifuko ya
hifadhi ya jamii nchini.
Aidha,
imeagiza ukaguzi wa kina wa ujenzi wa jengo jipya la Ofisi za Makamu wa
Rais kwa kuangalia usalama wa jengo, hesabu zilizotumika kama
zinaendana na thamani ya jengo na kama washauri walitoa ushauri wao
ipasavyo.
Akizungumza
katika kuhitimisha ukaguzi wa miradi mbalimbali ya serikali iliyofanywa
na Kamati ya Katiba na Sheria, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mohamed
Mchengerwa alisema NSSF ilitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi ikiwa
haijitoshelezi kwa kutoonesha gharama zilizotumika mpaka sasa, bajeti
iliyopangwa kutumiwa na kiasi kilichosalia ili kubaini kama fedha
zilizotumika zinalingana na thamani ya ujenzi wenyewe.
Kamati
ya Bunge ya Katiba na Sheria kwa takribani siku tano kuanzia Machi 29,
mwaka huu, ilitembelea Wizara ya Katiba na Sheria, Ofisi ya Waziri Mkuu,
Wizara ya Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu na Mahakama.
Akizungumzia
taarifa za utekelezaji wa miradi iliyofanywa na mifuko yote ya hifadhi
za jamii, Mchegerwa alisema kamati yake inataka kupitia taarifa zote za
utekelezaji wa miradi sambamba na kupitia sera ya uwekezaji ili
kuangalia kama yamefuata taratibu na hakuna upotoshaji.
“Kwanza
kuna madeni makubwa ambayo mifuko hiyo inadai kwa wapangaji wao. Pia
tunaangalia sera ya uwekezaji ili kujiridhisha kama ushauri wa kitaalamu
uliotolewa unakidhi matakwa ya ujenzi unaoendelea.
Aliongeza: “Kuna
majengo mengi yamejengwa hayana wapangaji lakini sera ya uwekezaji
itatusaidia kujua kama inafuatwa. Pia itatusaidia kubaini mapungufu
yaliyojiri, maana wajumbe wengi wana wasiwasi kuwa huenda ujenzi wa
majengo unalenga kwa wahusika kupata asilimia 10 bila kuangalia mahitaji
halisi, kwani majengo mengi yako wazi.”
No comments:
Post a Comment