Mishahara ya vigogo wa Serikali Waliokuwa Wanalipwa Milioni 36 hadi milioni 40 kwa mwezi yaanza kufyekwa - LEKULE BLOG

Breaking

Header Ads

Thursday, 7 April 2016

Mishahara ya vigogo wa Serikali Waliokuwa Wanalipwa Milioni 36 hadi milioni 40 kwa mwezi yaanza kufyekwa


Siku chache baada ya Rais Dk. John Magufuli kutoa agizo la kupunguza mishahara mikubwa ya watendaji wa mashirika ya umma, hatimaye Serikali kupitia Bodi ya Mishahara imeanza kazi ya kufanya marekebisho hayo.

Hatua hiyo imekuja baada ya Rais Magufuli, kuagiza kushushwa kwa viwango vya mishahara ya viongozi wa mashirika ya umma ambapo wengine hulipwa Sh milioni 36 hadi milioni 40 kwa mwezi.

Jana  Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angellah Kairuki, alisema katika kipindi cha miezi 15 kuanzia sasa mishahara ya watumishi hao itapunguzwa na kuwa yenye uwiano.

“Katika kuhakikisha agizo hilo linatekelezwa tunayo Bodi ya Mishahara ambayo ilianzishwa katika Serikali ya awamu ya nne na jukumu lake kubwa ni kufanya mapitio ya mishahara mbalimbali na kuhakikisha mishahara ya watumishi wa umma haipishani sana.

“Hatua ambazo tumeanza kuzitekeleza, tayari mamlaka zetu zimeanza kukutana kupitia Utumishi, Hazina na Msajili wa Hazina ili kuangalia namna ya kulitekeleza agizo hilo,” alisema Waziri Kairuki.

Alisema kutokana na hali hiyo mamlaka hizo hivi sasa zinaangalia mishahara ya taasisi mbalimbali na watumishi ili kuweza kubaini wale wanaolipwa zaidi ya Sh milioni 15 ni wangapi na itakatwa vipi.

Akizungumzia taasisi zinazozalisha kwa kiwango kikubwa na kuwa na uwezo wa kujiendesha, Waziri Kairuki, alisema Bodi ya Mishahara hivi sasa ina jukumu la kuangalia uwiano baina ya mtumishi wa umma na mashirika ya Serikali.

“Unakuta mtumishi wa taasisi X kiwango chake cha elimu, uzoefu, ujuzi, muda wa kuingia kazini pamoja na kazi anayoifanya ni sawa na ya mtumishi wa taasisi Y lakini unakuta mtumishi X analipwa mshahara mkubwa zaidi ya mara tano ya mtumishi Y jambo ambalo si haki katika utumishi,” alisema.

Kauli ya Rais Magufuli
Machi 30, mwaka huu akiwa wilayani Chato, Mkuu huyo wa nchi, alisema kuna watu wanalipwa kiwango kikubwa cha mishahara na wamekuwa wakiishi kuliko hata malaika na sasa ni lazima washushwe ili waishi kama shetani.

Hatua ya Rais Magufuli, kupitisha panga na kuweka uwiano wa mishahara kwa watendaji wa taasisi hizo unaelezwa kuwa utaisaidia uwajibikaji na usawa kwa watendaji.

Katika mkutano huo, Rais Magufuli, alishangazwa na baadhi ya bodi za wakurugenzi kushindwa kufanyakazi zao kwa mujibu wa sheria na badala yake wamekuwa na kazi ya kupandisha mishahara kwa watendaji.

Alisema anashangazwa na bodi hizo, kwani kila kukicha zimekuwa zikifanya kazi ya kupandisha mishahara pamoja na kufanya vikao nje ya nchi.

Alisema hivi sasa ameunda timu ya wataalamu ambayo imeanza kufanya kazi ya upunguzaji mishahara mikubwa kwa watendaji wakuu wa mashirika ya umma.

“Tena hawa wakurugenzi ndio wanaongoza kwa kulipwa fedha nyingi na hata kwenda kufanya vikao ulaya. Ninasema hapa kwamba suala hili litaanza kushughulikiwa katika bajeti hivi karibuni,” alisema Rais Magufuli.

Alisema tayari ameunda timu ya wataalamu ambayo inafanya kazi ya kupunguza mishahara hiyo na kufikia Sh milioni 15 kwa mwezi ili asipatikane Mtanzania anayelipwa zaidi ya kiwango hicho.


“Kuna watu wanaishi kuliko hata malaika lazima tuwashushe waishi kama shetani,” alisema Rais Magufuli.
Post a Comment