Siku
chache baada ya Rais Dk. John Magufuli, kutaja mshahara wake kuwa ni
Sh. milioni 9.5 kwa mwezi, Wizara ya Ofisi ya Rais, Menejiment ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, imefafanua mshahara aliokuwa anapokea
Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, kuwa unalingana na wa kiongozi
huyo.
Katibu Mkuu Utumishi, Dk. Laurean Ndumbaro jana alisema Kikwete aliondoka madarakani akiwa anapokea Sh. milioni 9.5, ikiwa ni kiwango sawa na cha Rais Magufuli.
“Hadi
Kikwete anaondoka madarakani, mshahara wake kwa mwezi ulikuwa Sh.
milioni 9.5, siyo kweli kuwa alikuwa akipokea Sh. milioni 34 kama
ilivyowahi kuelezwa kwenye baadhi ya vyombo vya habari,” alisema.
Mwishoni
mwa wiki akiwa kwenye mapumziko nyumbani kwake Wilaya ya Chato mkoani
Geita, Rais Magufuli alitaja mshahara wake, huku akiahidi kuweka
hadharani stakabadhi za mshahara (salary slip) atakaporudi Dar es
Salaam.
Rais
alilazimika kufanya hivyo kufuatia Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu
Lissu (Chadema) na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo),
kumpa changamoto ya kutaja mshahara wake, baada ya kueleza nia ya
serikali yake kupunguza mishahara ya watumishi wa mashirika na taasisi
zake kutoka Sh. milioni 40 hadi milioni 15.
Iwapo
Rais mstaafu Kikwete, alikuwa analipwa kiasi hicho, kwa mujibu wa
sheria, kwa sasa analipwa asilimia 80 ya mshahara huo ambayo ni Sh.
milioni 7.6 ya mshahara wa Rais aliyeko madarakani.
Hivi
karibuni, baadhi ya vyombo vya habari vilinukuu taarifa iliyotolewa
Julai, mwaka jana na mtandao wa Africa Review ulioandika kuwa Rais
Kikwete wakati akiwa madarakani alikuwa akishika nafasi ya tano miongoni
mwa marais 38 wa Afrika kwa kulipwa mshahara mnono wa Dola 16,000 za
Marekani (sawa na Sh. milioni 34 wakati huo).
Taarifa hizo zilikanushwa vikali na Ikulu, lakini hakukuwa na ufafanuzi wa mshahara halisi anaopokea Rais kwa wakati huo.
Kwa
mujibu wa Katiba ibara ya 43 (1), Rais atalipwa mshahara na malipo
mengineyo na atakapostaafu, atapokea malipo ya uzeeni, kiinua mgongo,
posho, kadiri itakavyoamuliwa na Bunge na mshahara, malipo hayo
mengineyo, malipo ya uzeeni na kiinua mgongo hicho, vyote vitatokana na
Mfuko Mkuu wa Hazina ya serikali na vitatolewa kwa mujibu wa masharti ya
ibara hiyo.
Ibara
ndogo ya pili inasema mshahara na malipo mengineyo yote ya Rais
havitapunguzwa wakati Rais atakapokuwa bado ameshika madaraka yake kwa
mujibu wa masharti ya Katiba.
No comments:
Post a Comment