Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ateketea kwa Moto Akiwa Ndani ya Gari Lake - LEKULE

Breaking

7 Apr 2016

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ateketea kwa Moto Akiwa Ndani ya Gari Lake


Mhadhiri  wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Idara ya Sayansi na Uhandisi wa Kompyuta (CoICT), Dk Richard Mgaya amefariki baada ya kuteketea ndani ya gari lake jijini Dar es Salaam juzi.

Gari la Dk Mgaya liliteketea baada ya kugongana na lori katika eneo la Mbezi Africana, Wilaya ya Kinondoni usiku wa kuamkia juzi na kuwaka moto uliosababisha kifo chake.

Juzi picha mbalimbali zilisambaa zikionesha gari aina ya Toyota Prado lililopata ajali eneo hilo la Africana baada ya kugongana na lori, baadaye ilibainika kuwa aliyekuwa katika gari hilo ni Dk Mgaya.

Akizungumza  kwa njia ya simu, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Christopher Fuime alisema gari la Dk Mgaya liliteketea na hata kushindwa kujulikana dereva wa gari hilo.

Alisema baadaye ndugu wa marehemu ndio walithibitisha kuwa gari hilo lililoteketea na dereva aliyekuwemo ni Dk Mgaya ambaye hata hivyo naye aliteketea ndani ya gari hilo.

“Lile gari liliungua na hakuna kitu kilichopatikana, hata wakati polisi wanafika eneo la tukio walikuta tayari dereva amekuwa majivu kutokana na kuteketea kwa moto… labda baada ya kupima vinasaba ndio itathibitika kama ilikuwa ni yeye,” alisema Kamanda Fuime.

Alisema hata gari hilo hawakuweza kulitambua mara moja na baada ya kufuatilia Mamlaka ya Mapato (TRA) ilibainika kuwa mmiliki wake ni Dk Mgaya.

Alisema “ndugu wa marehemu ndio wamesema kuwa ni ndugu yao.” 

Dk Mgaya alijiunga na idara hiyo miaka kadhaa iliyopita akitokea masomoni nchini Marekani na alikuwa ni mtaalamu wa artificial intelligence.

No comments: