Wanakijiji Wala Nyama ya Ng’ombe Aliyegongwa na Nyoka - LEKULE

Breaking

26 Mar 2016

Wanakijiji Wala Nyama ya Ng’ombe Aliyegongwa na Nyoka

Mwandishi Wetu, Risasi Jumamosi.

DODOMA: Hatari! Baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Saji kilichopo wilayani Bahi, Dodoma wamejikuta wakila nyama ya ng’ombe aliyekufa baada ya kuumwa na nyoka bila kujali madhara yake, Risasi Jumamosi linakuhabarisha.

Tukio hilo la aina yake lilinaswa na paparazi wa gazeti hili wiki iliyopita baada ya kuwakuta wakazi hao wakijinunulia nyama hiyo kutoka kwa muuzaji kwa njia ya kubadilishana na nafaka au kwa pesa taslimu.

Ishu hiyo ilijulikana baada ya paparazi wetu kukuta nyama hiyo ikining’inia kwenye mti huku baadhi ya wakazi wakinunua ambapo mwenyeji mmoja alimtaka kuachana na nyama hiyo kwa vile, ng’ombe wake alikufa kwa kuumwa na nyoka zizini usiku.

“Nakushauri uachane na hiyo nyama. Ng’ombe wake alikutwa asubuhi amekufa kwa kuumwa na nyoka. Wananchi wa huku ng’ombe au mbuzi akifa kwa kuumwa na nyoka hawatupi mzoga, wanakula.
Alipoulizwa wananchi hao wanajuaje kama ng’ombe aliumwa na nyoka wanapomkuta asubuhi amekufa, mwenyeji huyo alisema:

“Wanapomkagua wanakutana na jeraha la meno ya nyoka. Lakini pia nyama ya ng’ombe aliyeumwa na nyoka huwa nyekundu zaidi ya wekundu wa kawaida.”

Mwanakijiji mmoja aliyejitambulisha kwa jina la  Saimosi alisema hakuna madhara yoyote kwa kula nyama hiyo kwa vile wanajua jinsi ya kutoa sumu hiyo.

“Ng’ombe akifa kwa kuumwa na nyoka, nyama yake tunaichemsha kwa muda mrefu sana ili kutoa sumu. Baada ya hapo hata ikiliwa haina madhara,” alisema mkazi huyo.

Paparazi wetu alifanya jitihada za kumpata daktari wa mifugo wa Wilaya ya Bahi ili kumsikia anazungumziaje suala hilo lakini hakufanikiwa.

Pia alimtafuta Mbunge wa Jimbo la Bahi, Omar Ahemed Badwel kwa njia ya simu ili kusikia kauli yake ambapo namba moja ilionesha kutotumika huku nyingine ikiwa imefungwa

No comments: