CUF: Hatutapotea katika siasa nchini - LEKULE

Breaking

26 Mar 2016

CUF: Hatutapotea katika siasa nchini

Chama cha Wananchi (CUF) kimesema uamuzi wa kutoshiriki uchaguzi wa marudio Zanzibar hauwezi kukipoteza katika ramani ya siasa nchini.

Badala yake, kimesema umekiongezea heshima kwa maelezo kuwa “ni heri kushindwa kwa kutoshiriki kuliko kushinda katika uchaguzi usio wa haki na uliojaa ukiukwaji mkubwa wa Katiba sheria”.

Januari 28, mwaka huu, Baraza Kuu la Uongozi la chama hicho lilitangaza msimamo wa kutoshiriki uchaguzi wa marudio na kutoa hoja 12 likielezea kuwa ni batili na hivyo kushiriki ni kuhalalisha haramu kuwa halali.

Uchaguzi huo ulifanyika Machi 20 na mgombea urais wa CCM, Dk Ali Mohammed Shein aliibuka mshindi kwa asilimia 91. Shein aliapishwa juzi.

Akizungumzia mwelekeo wa CUF baada ya kukosa nafasi zote za uwakilishi, udiwani na urais, Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi wa chama hicho, Omary Ali Shehe alisema hakuna mwanachama wala mgombea atakayetetereka kwa kuwa wanajivunia uimara wa uongozi na msimamo wa wanachama.

Alisema CUF imejipanga kuendelea kujijenga kwa sababu lengo ni kuongoza nchi na kwamba, matokeo ya uchaguzi huo hayawatishi wala kuwayumbisha, badala yake yamewaimarisha zaidi.

“CUF haitakata tamaa mpaka pale ambapo CCM watajua maana ya siasa za vyama vingi na kuheshimu demokrasia. Tunajua athari ya kutoshiriki uchaguzi na tumepanga kuikabili hali hii, ila tungepata athari zaidi kama tungeshiriki,” alisema Shehe.

“Tutakachokifanya ni kurudi nyuma na kuanza kukijenga chama. Hatuwezi kuyumba wala kutetereka, maana hali kama hii imekuwa ikijitokeza lakini tunazidi kuimarika.”  

No comments: