Rais Magufuli atajwa mgogoro Chuo cha Ualimu Mpwapwa - LEKULE

Breaking

26 Mar 2016

Rais Magufuli atajwa mgogoro Chuo cha Ualimu Mpwapwa

RAIS John Magufuli anatajwa kuwa mwenye suluhu katika mgogoro unaoendelea katika Chuo cha Ualimu Mpwapwa kilichopo Dodoma, anaandika Dany Tibason.

Mgogoro huo unamuhusisha Victoria Komanya, mkufunzi wa chuo hicho kilichopo katika Wilaya ya Mpwapwa na Deogratius Rugalema, mkuu wa chuo hicho.

Wakati Komanya akilalamika kutopangiwa vipindi vya kufundisha, Rugalema anadai mkufunzi huyo lazima ang’oke kwa kuwa ni jeuri na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi inamlea.

Rugalema anasema, kwa kuwa wizara ndiyo inayomlea Komanya, Rais Magufuli ndiye pekee anayeweza kutatua mgogoro huo kwa kumuondoa mkufunzi huyo.

Komanya analalamikia kitendo cha kukaa chuoni hapo kwa miezi 11 sasa bila kufundisha kutokana na mkuu wake kutompangia vipindi na kwamba, mshahara anaoupata bila kuufanyia kazi ni sawa na kuiingizia hasara serikali.

“Ninasikitika sana kutofanya kazi kwa miezi 11 sasa (kuanzia Mei mwaka jana) lakini ninaendelea kulipwa mshahara wa serikali jambo ambalo licha ya kutofanya kazi naamini naitia serikali hasara.

“Nasema hivyo kutokana na mkuu wangu wa chuo kuninyima haki zangu za msingi na zaidi ikiwa ni kunyimwa vipindi vya kufundisha pamoja na kutopata fursa ya kuhudhuria mafunzo mbalimbali,” amesema.

Alisema amekuwa na mgogoro na mkuu wake wa chuo tangu mwaka 2014 baada ya Rugalema kumlazimifa kuhama nyumba anayoishi sasa na kwa miaka saba iliyopita.

Amesema, mgogoro wake ulifikia katika kamati ya usuluhishi wa migogoro kazini lakini Rugalema amegoma kusikiliza ushauri huo.

“Kamati ya nyumba ilinitaka kuhamia katika nyumba ambayo hainitoshi kwani ilikuwa na chumba kimoja na sebure.

“Na kwa sasa mimi nina familia ya zaidi ya watu watano wakike na kiume lakini nalazimishwa kuondoka kwenye nyumba ya sasa, jambo lingine niliomba ruhusa ya kumuona baba yangu mzazi akiwa ICU katika Hospitali ya Kahiruki, Dar es Salaam lakini nilinyimwa hadi baba alipofariki.

“Imefikia hatua ya kutaka kufukuzwa kazi ikiwa ni pamoja na kutakiwa kushushwa mshahara wangu lakini baada ya kukata rufaa mshahara wangu umebaki pale pale,”amesema.

Kuhusu malalamiko hayo Rugalema amekiri huwepo kwa mgogoro huo kwa madai kwamba, wizara imeonekana kumlea licha ya kuwa ni jeuri.

Alisema ugomvi mkubwa ni mwalimu kukataa kuondoka katika nyumba ambayo alitakiwa kuwapisha walimu ambao wana familia.

Kuhusu kulipwa mshahara huo bila kufanya kazi amesema ni sahihi kwani mwalimu huyo alisimamishwa kazi na baada ya kukara rufaa alishinda na kuhitajika kurudi kazini.

Amedai mkufunzi huyo alitakiwa kuondoka katika nyumba hiyo ili kuwapisha watumishi wenye familia.

Gofrey Lugano, Kaimu Katibu wa Tume ya Utumishi ya Walimu (TSD) amesema, mkufunzi huyo alihukumiwa na tume ngazi ya wilaya baada ya kumkuta na hatia ya kudharau na kutotii mamlaka husika.

Lugano amesema, TSD ilitoa hukumu hiyo katika kikao ilichoketi tarehe 16 Desemba mwaka jana.
Amesema, mkufunzi huyo hakukubaliana na hukumu hiyo hivyo alikata rufaa katika ngazi ya TSD Mkoa wa Dodoma.

Kuhusu kupangiwa vipindi Lugano amesema, mkufunzi huyo hawezi kupangiwa hadi rufaa yake itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.

No comments: