Makusanyo TRA yashuka - LEKULE

Breaking

26 Mar 2016

Makusanyo TRA yashuka

Kiwango cha ukusanyaji wa mapato ya serikali yanayotokana na kodi mbalimbali kimeshuka kati ya Desemba mwaka jana na mwezi huu.

Itakumbukwa kuwa Novemba mwaka jana, makusanyo ya Mamlaka ya Mapato (TRA) yalipanda kutoka wastani wa Sh. bilioni 800-900 kwa mwezi mpaka Sh. trilioni 1.3.

Kiwango hicho kiliongezeka na kuwa Sh.trilioni 1.4 kwa Desemba kabla ya TRA kukusanya jumla ya Sh. trilioni 1.06 Januari na Sh. trilioni 1.04 mwezi uliopita.

Kaimu Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa mlipa kodi wa Mamlaka hiyo, Diana Masalla, aliiambia Nipashe katika mahojiano wiki iliyopita kuwa,  TRA imejiwekea lengo la kukusanya Sh. trilioni 1.3 kwa mwezi huu.

“Kwa mwezi wa Machi lengo ni kukusanya Sh.trilioni 1.3, kiasi hiki ni lengo lakini tunaweza kuvuka na kufikia zaidi ya hapo,” alisema Massala.

Wakati akilihutubia Bunge mjini Dodoma Novemba 20, mwaka jana, Rais John Magufuli alisema kwa zaidi ya miaka mitatu ukusanyaji wa mapato ulikuwa chini kwa sababu mbalimbali.

Alisema Serikali ya awamu ya Tano itaongeza nguvu katika upanuzi wa wigo wa kodi na kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato.

“Tutahakikisha kwamba kila mtu anayestahili kulipa kodi analipa kodi stahiki. Hatutasita kumchukulia hatua mtu yoyote atakaye kwepa kulipa kodi," alisema.

"Tunawaomba wananchi mhakikishe mnapewa risiti kila mnaponunua bidhaa au huduma. Kodi ni kitu muhimu lazima kila mtu anayestahili kulipa kodi alipe."

Rais Magufuli pia alieza kuwa, serikali yake itahakikisha kwamba kila senti inayoongezeka katika mapato ya Serikali inaelekezwa katika kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi kwa kuziba mianya ya upotevu wa fedha za Serikali ambayo inaipunguzia Serikali uwezo wake wa kuwahudumia wananchi.

Lakini tangu iweke rekodi ya makusanyo Desemba mwaka jana, TRA imeshindwa kurudi katika kiwango cha makusanyo ya Sh. trilioni 1.4.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa kodi wa TRA, Richard Kayombo alisema kila mwezi TRA hujiwekea  malengo ya kukusanya kodi kiasi fulani, na kwa miezi mitatu iliyopita wameweza kuvuka lengo.

“Kila mwezi una malengo tuliyojiwekea na miezi yote mitatu tumevuka malengo tuliyojiwekea,” alisema Kayombo.

WATAALAM WA UCHUMI WAELEZA SABABU
Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Dk. Bill Kiwia alieleza sababu zinazoweza kusababisha makusanyo ya kodi kupanda na kushuka kwa serikali au halmashauri.

Alisema serikali inaweza kuwa na makusanyo mengi katika mwezi fulani kutokana na malimbikizo ya kodi kuwa mengi kutoka kwa wafanyabiashara.

Alisema kwa mfano mwezi Desemba, serikali ilikusanya Sh.trilioni 1.4 kwa sababu wafanyabiashara wengi walikuwa wanalipa kodi tofauti na udanganyifu walioufanya miaka ya nyuma.

Alisema makusanyo yanaweza kupungua kutokana na udanganyifu unaofanywa na baadhi ya wafanyabishara, akitolea mfano, mfanyabiashara anakua na namba mbili hadi tatu za utambulisho wa biashara (TIN).

Alisema endapo serikali inahitaji kukusanya mapato mengi zaidi inapaswa kutoa elimu kwa wananchi ya umuhimu wa kulipa kodi.
“Sera ya ukusanyaji kodi iendane na aina ya biashara, tusije tukawa tunahamasisha ukusanyaji wa kodi huku tukawa tunaua sekta binafsi,” alisema Dk. Kiwia.

Naye Mkuu wa Idara ya Uchumi wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Jehovaness Aikaeli alisema kinachosababisha mapato kuongezeka ama kushuka inategemea nguvu au juhudi ya ukusanyaji wa mapato iliyojiwekea serikali kwa mwaka.

Alisema nguvu hiyo ni pamoja na kuziba mianya ya rushwa.
Alisema utofauti wa shughuli za kiuchumi au kibiashara kwa mwezi husika nayo inaweza kusababisha makusanyo ya kodi kupanda au kushuka.

“Kwa mfano mwezi wa kumi na mbili (Desemba), shughuli nyingi za kibiashara zinafanyika, watu wanafunga biashara zao, hivyo lazima makusanyo kwa serikali yatakuwa makubwa,” alisema Dk. Aikaeli.

Aidha, Dk. Aikaeli alisema miezi mingine kama vile Januari, wafanyabishara wengi wanakuwa na shughuli zingine za kiuchumi mbali na kulipa kodi hivyo hata mapato kwa serikali hupungua.

No comments: