Serikali ya Marekani imeamua kutaifisha mali za mfanyabiashara wa dawa
zilizopigwa marufuku za kulevya kutoka Tanzania, Ali Khatib Haji Hassan,
maarufu kwa jina la “Shikuba” na mtandao wake na kupiga marufuku
kampuni za nchi hiyo kujihusisha na biashara zake.
Shikuba,
ambaye amekuwa akihusishwa na biashara kubwa ya usafirishaji dawa za
kulevya kati ya Afrika Mashariki, Asia, Ulaya na Marekani, alikamatwa
mwaka 2014 nchini Tanzania akihusishwa na shehena ya kilo 210 za heroin
zilizokamatwa mkoani Lindi mwaka 2012.
Taarifa iliyotolewa juzi
na kitengo cha udhibiti wa mali za nje cha Wizara ya Fedha ya Marekani
imeeleza kuwa serikali imemtambua Shikuba kama kinara wa usafirishaji wa
dawa za kulevya kwa mujibu wa Sheria ya Utambuzi wa Vinara wa Dawa za
Kulevya wa Nje (Foreign Narcotics Kingpin Designation Act) ya Marekani.
“Hassan
(pichani) ni kinara mkubwa wa kimataifa wa dawa za kulevya ambaye
anasafirisha mamilioni ya tani za heroine na cocaine kwenda barani
Afrika, Asia, Amerika Kaskazini kwa kutumia mtandao wake uliopo Afrika
Mashariki,” inasema taarifa hiyo ya Serikali ya Marekani iliyotolewa
Washington juzi.
“Kutokana na uamuzi wa leo (juzi), mali zote za
Hassan na mtandao wake ambazo ziko ndani ya mamlaka ya Marekani au
kwenye mikono ya raia wa Marekani zinataifishwa.”
Sheria hiyo ya
Marekani ilipitishwa mwaka 1999 na kuanza kazi mwaka uliofuatia, ikiwa
na lengo la kudhibiti wasafishaji wa dawa za kulevya, biashara na
shughuli zao kuingia kwenye mfumo wa kifedha wa nchi hiyo na kudhibiti
biashara na miamana baina ya wasafirishaji wa dawa hizo na kampuni za
Marekani na raia wake.
Kwa mujibu wa gazeti la The New York
Times, sheria hiyo imekuwa ikitumiwa na Marekani kufuatilia wahalifu
kadhaa wanaojihusisha na biashara hiyo duniani.
Kwa mujibu wa taarifa
hiyo ya Marekani, Hassan amekuwa akijaribu mara kadhaa kurubuni viongozi
wa Serikali za Afrika kuepuka kukamatwa na kufunguliwa mashtaka
kutokana na biashara zake haramu.
“Uamuzi wa leo unaweka vikwazo
kwa Ali Khatib Haji Hassan na mtandao wake kusafirisha heroine na
cocaine duniani na kumzuia kutumia faida haramu kurubuni maofisa wa
Serikali za Afrika,” anasema kaimu mkurugenzi wa OFAC, John E. Smith
katika taarifa hiyo.
“Wasafirishaji wa dawa za kulevya kama
Mtandao wa Usafirishaji Dawa za Kulevya wa Hassan ni tishio kubwa kwa
uthabiti wa mfumo wa kimataifa wa fedha na kanda, na Hazina inaendelea
kuwa thabiti katika kuuanika na kufuatilia na wale wanaochochea biashara
hiyo duniani.”
Tangu mwaka 2006, amekuwa akiongoza wanachama wa
mtandao wake kutuma shehena za dawa hizo kwenda sehemu kadhaa duniani
kama China, Ulaya na Marekani.
Hassan alikuwa msambazaji wa kwanza kwa
wasafirishaji dawa za kulevya wa Tanzania ambao mara kwa mara walikuwa
wakipokea maelfu ya kilo za heroine kutoka pwani ya Makran nchini
Pakistan na Iran.
Hassan, pia alisimamia mtandao wa
wasafirishaji hao barani Amerika Kusini na kuzisafirisha hadi Afrika
Mashariki, zikiwa njiani kwenda Ulaya na China.
Akizungumzia
hatua hiyo, aliyekuwa Kamishna wa Kikosi cha Kupambana na Dawa za
Kulevya nchini, Godfrey Nzowa alisema Hassan alikamatwa Januari mwaka
2014 Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA) baada
ya mbinu nyingi kugonga mwamba.
“Mtandao wa Shikuba ulikamatwa
mapema kabla yake na ilituchukua muda mrefu kumkamata baada ya mbinu
zetu nyingi kugonga mwamba,” alisema.
Kuhusu sheria, Kamanda
Nzowa alisema iwapo itahakikishwa kuwa Hassan amepata mali zake kwa njia
ya kuuza dawa za kulevya, zitataifishwa kama walivyofanya Marekani.
No comments:
Post a Comment