Rais Magufuli Atoa Kibali Cha Safari Nje ya Nchi Kwa Mawaziri Wawili - LEKULE BLOG

Breaking

Header Ads

Friday, 11 March 2016

Rais Magufuli Atoa Kibali Cha Safari Nje ya Nchi Kwa Mawaziri Wawili

Tangu Novemba 5 wakati Dk John Magufuli alipoapishwa, ni Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na Waziri wa Mambo ya Nje, Balozi Augustine Mahiga pekee waliotoka nje ya nchi, lakini jana Rais aliwaruhusu mawaziri wengine wawili kusafiri nje.

Rais Magufuli alizuia safari za nje siku chache baada ya kuapishwa akisema watumishi wa umma watakaokuwa wakitaka kwenda nje watalazimika kuomba kibali kutoka Ikulu, ikiwa ni mkakati wake wa kudhibiti matumizi ya fedha za Serikali.

Tangu wakati huo, safari za nje kwa watumishi wa umma zimekuwa za nadra na mawaziri wamekuwa wakifanya ziara za kwenda mikoani kufuatilia utendaji na utoaji wa huduma kwa wananchi.

Jana, Rais Magufuli aliwaruhusu mawaziri wawili kwenda Vietnam kujifunza mbinu za kuinua kilimo na kujenga viwanda ili kuwaondoa Watanzania kwenye lindi la umaskini. 
Mawaziri wawili waliopata kibali hicho ni Waziri wa Viwanda na Biashara, Charles Mwijage na Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mwigulu Nchemba.

Rais Magufuli alitoa uamuzi huo jana baada ya kufanya mazungumzo na Rais Truong Tang Sang wa Vietnam juzi na kukubaliana kuweka sawa mazingira ya biashara na uwekezaji baina ya nchi zao.

Akizungumza jana baada ya kumtembeza Rais huyo kwenye Eneo Maalumu la Uwekezaji la Benjamini Mkapa (EPZ) lililopo Ubungo jijini hapa, Waziri Mwijage alisema Dk Magufuli ametoa kibali hicho baada ya kuridhishwa na mabadiliko ya muda mfupi ya Vietnam.

“Kutokana na hatua waliyopiga, Rais ameniruhusu mimi na Waziri wa Kilimo, Mwigulu Nchemba kwenda nchini humo muda mfupi baada ya Rais Truong kuondoka.

"Nitakwenda kujifunza mbinu zao ili sekta ya viwanda iajiri zaidi ya asilimia 46 ya vijana wa Kitanzania,” alisema Mwijage.

Baada ya kuondolewa vikwazo na Marekani, Vietnam ilichagua kuendeleza maeneo maalumu ya biashara na kufanikiwa kujijenga kiuchumi na kufikia uchumi wa kati katika kipindi cha miaka 23.

Rais Truong alieleza kuwa waliwekeza Sh10 bilioni katika miradi na asilimia 80 ya fedha hizo ilielekezwa katika mauzo ya nje.

“EPZ zina mchango mkubwa kwenye uchumi wetu. Ninaamini, Tanzania inaweza kupata zaidi ya Dola 20 bilioni kwa mwaka itazipata kutoka katika maeneo haya.

"Hata sisi wakati tunaanza tulikuwa na EPZ chache lakini sasa tunazo nyingi na zinatuingizia dola 20 bilioni (za Marekani) kwa mwaka,”alisema. 
Pamoja na eneo hilo, Mwijage alisema Serikali ina mpango wa kuijenga Bagamoyo na kuifanya kuwa mji wa uwekezaji.

“Taratibu za kuwalipa wananchi ili kupisha eneo la kilomita 100 za mraba zimekamilika na ndani ya mwaka huu mchakato huo utahitimishwa kabla wawekezaji hawajaanza kukaribishwa,” alisema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa EPZ, Kanali mstaafu Joseph Simbakalia alisema Serikali imeuagiza kila mkoa kutenga eneo la uwekezaji ili kuongeza idadi ya viwanda vilivyopo nchini.

“Kwa sasa EPZ zinaingiza kiasi cha dola bilioni moja za Marekani (zaidi ya Sh2 trilioni) kwa mwaka.Serikali kwa kushirikiana na Singapore imetenga dola 10 bilioni (zaidi ya Sh20 trilioni) ambazo zitatumika kujenga mji wa Bagamoyo,” alisema Kanali Simbakalia.


Mikoa mingine iliyotengwa kwa ajili ya kujenga EPZ ni Kigoma, Morogoro na Mtwara. 
Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Charles Mwijage akimtambulishaMkurugenzi Mkuu wa EPZA, Mhe. Kanali Mstaafu Joseph Simbakalia
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe. Mwijage akimwelezea Rais wa Vietnam, Mhe. Truong shughuli zinazofanywa na Kampuni ya Simu ya Halotel kutoka nchini Vietnam, ambapo alimwonyesha Vocha za muda wa maongezi za mtandao huo ambazo zinapatikana katika gharama tofauti kulingana na nafasi ya kifedha ya mtumiaji.
Mhe. Mwijage akiwasilisha taarifa ya Wizara juu ya fursa za uwekezaji zilizopo nchini Tanzania, hali halisi ya uwekezaji katika kituo cha EPZA na jitihada zinazofanywa na Serikali katika kuanzisha maeneo ya uwekezaji katika mikoa yote nchini kufuatia shughuli za kiuchumi zinazofaa katika Mkoa husika.
Post a Comment