Watu sita wamekufa na wengine zaidi ya 38 kujeruhiwa na kulazwa
Hospitali ya Rufani Mkoa wa Iringa baada ya basi walilokuwa wakisafiria
kutoka Mwanza kwenda Iringa kupinduka mlima Ipogolo Manispaa ya Iringa.
Mganga
Mkuu Mkoa wa Iringa, Dk Robert Salim alisema waliokufa ni sita, wawili
kati yao walifia hospitalini wakati wakipatiwa matibabu.
Dk Salim alisema waliokufa ni wanaume wanne na wanawake wawili na
kwamba, maiti waliotambuliwa ni wawili, Makka Msigwa na Venant Mhagama.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Iringa, Peter Kakamba alisema ajali hiyo ilitokea
juzi saa 3.30 usiku baada ya basi la Lupondije aina ya Scania lililokuwa
likitoka Mwanza kwenda Iringa kumshinda dereva na kupinduka.
Alisema majeruhi 38 walifikishwa hospitalini hapo, 11 walitibiwa na kuruhusiwa na wengine 27 wamelazwa kwa matibabu.
Kakamba alisema wanaendelea na uchunguzi kubaini chanzo cha ajali hiyo.
Mmoja
wa abiria walionusurika katika ajali hiyo, James John alisema
walipofika Iringa, dereva waalikataa kuwashusha abiria waliokuwa
wakiishia mjini ili awapeleke waliokuwa wakienda Mbeya kwenye basi
jingine eneo la Ipogolo.
John alisema kutokana na uamuzi huo
abiria waliotakiwa kushuka Kituo cha Kihesa na Kituo Kikuu cha Mabasi
Iringa walipitiliza, lakini hawakufika Ipogolo wakapata ajali eneo la
mlimani.
Dereva huyo, Castory Mwalusako (35) alisema basi hilo
lilimshinda wakati akishuka mlima kutokana na kupoteza upepo kwenye
breki na kulikwepa gari dogo lililokuwa mbele yake na kupoteza mwelekeo
kisha kupinduka.
No comments:
Post a Comment