Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ametoa mwelekeo wa upangaji wa uongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni na baraza kivuli la mawaziri, huku akionyesha kambi hiyo kuwa tayari kushirikiana na Mbunge wa Kigoma Mjini kwa tiketi ya ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe.
Akizungumza jana mjini Dodoma Mbowe alisema idadi ya wizara hizo itafanana na ya wizara za Serikali ya Awamu ya Tano ambazo zipo 19.
“Tutatangaza baraza kivuli kabla ya kumalizika kwa mkutano wa Bunge Ijumaa wiki hii na baraza hili litashirikisha vyama vyote vinavyounda Ukawa,” alisema Mbowe.
Alisema kigezo cha kwanza kitakuwa uzoefu na taaluma za wabunge kikifuatiwa na mgawanyo wa nafasi kwa kuzingatia kipaumbele hicho kwanza.
“Tutazipanga kulingana na muundo wa Muungano kwa sababu kuna wizara ambazo ni sehemu ya Muungano. Nne tutazingatia jinsia kadri iwezekanavyo na tano tutazingatia uteuzi kulingana na mikoa, yaani mawaziri vivuli watateuliwa kulingana na mikoa wanayotoka kadri itakavyowezekana.”
Alisema miaka yote, upinzani ulikuwa ukiitaka Serikali kupunguza ukubwa wa Baraza la Mawaziri, hivyo uamuzi wa Rais John Magufuli kupunguza idadi ya wizara ni jambo zuri na wao watafanya hivyo katika uteuzi wa baraza hilo kivuli.
Kuhusu Zitto alisema: “Katika siasa na ushirikiano wa vyama hakuna mazingira ya kudumu. Jambo lolote linawezekana lakini kuna taratibu zake na muda ndiyo huwa unaongea.”
Alisema Chadema na NCCR vimewahi kuwa na wabunge ambao kwa sasa ni makada wa CCM, huku akitolea mfano jinsi Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa alivyohama CCM na kujiunga na Chadema na kugombea urais.
“Hatujawahi kama kambi ya upinzani kumtenga Zitto kwenye kila jambo, yapo mambo tunaweza kulazimika kutengeneza ushirikiano na wabunge hata wa CCM ili kufanya jambo fulani kutekelezeka.
“Kushirikiana na Zitto si jambo la ajabu kama ambavyo umeona tukilifanya. Yapo majeraha mengi ambayo tumeyapitia pande zote (Chadema na Zitto) ambayo huwezi kuyatibu kwa siku moja.
"Yapo ambayo yatapona kulingana na muda. Unaweza kumfanyia mtu kitu kibaya, lakini baadaye ukatambua kuwa umekosea. Chochote katika siasa kinawezekana,” alisema Mbowe.
Zitto alifukuzwa Chadema na kujiunga na ACT Wazalendo Machi 21, 2015 chama ambacho hakina ushirikiano na vyama vinavyounda Ukawa lakini katika siku za karibuni ameonekana kuwa karibu na umoja huo wa wananchi, ikiwa ni pamoja na kushirikiana kuibua hoja mbalimbali katika mkutano wa Bunge unaoendelea mjini Dodoma.
No comments:
Post a Comment