Jela miaka 5 kwa kusafirisha Wahamiaji Haramu - LEKULE

Breaking

3 Feb 2016

Jela miaka 5 kwa kusafirisha Wahamiaji Haramu



MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Iringa imewahukumu kwenda jela miaka mitano au kulipa faini ya Sh milioni 1.5 kila mmoja, dereva Hansi Mwakyoma (28) na utingo wake, Alex Adam (32) baada ya kukamatwa na kukiri kusafirisha wahamiaji wasio na vibali 83 kutoka Ethiopia.

Wahamiaji hao wamehukumiwa kwenda jela miaka miwili au kulipa faini ya Sh milioni moja kila mmoja.

Kwa kutumia gari aina ya Scania lenye namba za usajili T478 DFE, mali ya Flora Mwambenja wa Mbeya, Januari 16, mwaka huu, dereva huyo na utingo wake, walikamatwa katika kijiji cha Ruaha Mbuyuni wilayani Kilolo Barabara Kuu ya Iringa - Mbeya, wakiwasafirisha watu hao kwenda Kyela mpakani mwa Tanzania na Malawi.

Akitoa hukumu hiyo juzi, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mkoa wa Iringa, Andrew Scout alisema ameridhika na maelezo yaliyotolea na Wakili wa Serikali na vielelezo, likiwamo gari lililotumiwa na watuhumiwa hao kusafirisha watu hao kutoka Kongowe, Dar es Salaam kwenda Kyela mkoani Mbeya.

Baada ya kusoma hukumu hiyo, baadhi ya raia hao wa Ethiopia waliangua kilio mahakamani hapo na kusababisha watu waliokuwa karibu na jengo hilo, kusogea ili kujionea kulikoni.

Mkalimani wa wahamiaji hao, ambao hawazungumzi Kiingereza wala Kiswahili zaidi ya lugha ya kwao, Emmanuel Mtaltisili ambaye ni mtangazaji wa kituo cha redio ya Ebony FM cha mjini Iringa alisema;“walichokitarajia wahamiaji hao ni kupewa hukumu ya kurudishwa kwao baada ya kukiri kosa hilo.”

Awali akisoma maelezo ya kosa la watuhumiwa hao baada ya wote kukiri kosa mbele ya mahakama hiyo, Wakili wa Serikali kutoka Idara ya Uhamiaji, Godfrey Ngwijo alisema ilikuwa Januri 16, mwaka huu katika eneo la Ruaha Mbuyuni watuhumiwa hao walikamatwa wakiwa ndani ya gari hilo lenye bodi lililofunikwa, wakisafiri kutoka Kongowe kwenda Malawi kinyume cha Sheria ya Uhamiaji ya Mwaka 2002 iliyofanyiwa Marejeo mwaka 2015.

Alisema katika tarehe isiyojulikana, watuhumiwa 83 raia wa Ethiopia waliingia nchini kwa kutumia njia zisizo halali na kwenda Dar es Salaam, walikoanzia safari yao ya kwenda Kyela mkoani Mbeya ili waingie nchini Malawi.

No comments: