Katibu
Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Mbogo Futakamba akitoa
zawadi kwa mfanyakazi bora wa mwaka 2015 toka DAWASCO wakati
alipotembelea Shirika hilo mapema wiki hii. Pamoja na mambo mengine
alielekeza shirika juu ya utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na
Serikali ya kuunganisha Wateja Milioni Moja ifikapo June 2016. Picha na
Everlasting Lyaro- DAWASCO.
WIZARA
ya maji na umwagiliaji, imesema inaridhishwa na kasi ya utekelezaji wa
mipango ya usambazaji wa huduma za maji, inayofanywa na shirika la
majisafi na majitaka jijini Dar es Salaam (DAWASCO) na kutoa rai kwa
watumishi wa shirika hilo kushirikiana ili kufikia malengo ya utoaji wa
huduma kwa wananchi.
Hayo
yalisemwa jana na katibu mkuu wa wizara hiyo mhandisi Mbogo Futakamba,
alipokuwa akiwahutubia wafanyakazi wa DAWASCO, katika makao makuu ya
shirika hilo jijini Dar es Salaam.
Mhandisi
Futakamba, alisema kasi ya utoaji wa huduma bora za maji kwa wakazi wa
jiji la Dar es Salaam, imepunguza malalamiko mengi ya wananchi, na
kwamba serikali imeanza kupata matumaini makubwa na kujenga imani kwa
shirika hilo kwa kufanikisha malengo makuu ya usambazaji wa huduma hiyo
kwa wananchi.
Aidha
alisema kwa kiwango kikubwa wizara ya maji na umwagiliaji kwa sasa
inajivunia kwa kazi nzuri iliyofanywa na shirika hilo, hasa kwa
kuzingatia kuwa DAWASCO ndio jicho la wizara kutokana na wingi wa
wananchi wanaohitaji huduma za maji zinazosambazwa na shirika hilo.
“Nimeona
jitihada zenu, nimependa jinsi mnavyofanya kazi kama timu, naomba muwe
na uaminifu mkubwa sana katika kazi, kuweni wawajibikaji ili wananchi
wapate huduma ya maji”, alisema mhandisi Futakamba.
Katika
hatua nyingine katibu mkuu huyo alipongeza juhudi kubwa zilizofanywa na
shirika hilo za kupunguza kiwango cha upotevu wa maji pamoja na
kudhibiti wizi wa maji, ambavyo vimekuwa kikwazo kinachochochea
malalamiko ya wananchi kwa shirika hilo.
Awali
akitoa taarifa ya shirika hilo, afisa mtendaji mkuu wa DAWASCO, mhandisi
Cyprian Luhemeja, alisema shirika hilo limefanikiwa kuboresha huduma ya
upatikanaji wa maji, baada ya kuongeza uzalishaji kutoka mita za ujazo
7,834,234 hadi mita za ujazo 8,421,370 kati ya mwezi Mei hadi Novemba
2015.
Alizitaja
sababu za mafanikio ya ongezeko la kiwango cha maji ni pamoja na
udhibiti wa upotevu wa maji katika bomba kubwa, kufanya matengenezo ya
tahadhari, maboresho ya maslahi ya wafanyakazi na kuboreshwa kwa kitengo
cha upotevu wa maji.
Mhandisi
Luhemeja alibainisha kuwa DAWASCO, imefanikiwa kufunga dira katika
maungio ya maji, kuziba maeneo yanayovujisha maji kwa wakati, kupambana
na wezi wa maji, kuhakiki ufanisi wa dira za maji, kusajili maboza ya
wauzaji maji na kuboresha usomaji wa dira, ambavyo viliwezesha kupunguza
kiwango cha maji yanayopotea kutoka asilimia 62 hadi 45, kati ya mwezi
Mei mpaka Novemba 2015.
Aliongeza
kuwa mafanikio ya utekelezaji wa mipango ya uboreshaji wa huduma za
maji yaliwezesha shirika hilo la DAWASCO, kuongeza makusanyo ya mapato
kutoka shilingi bilioni 2.9 hadi kufikia bilioni 6.2 kati ya mwezi Mei
hadi Novemba 2015.
Wakati
huo huo shirika hilo limeanza kutekeleza agizo la serikali linaloitaka
DAWASCO, kuongeza idadi ya wateja wake hadi kufikia milioni moja, katika
jiji la Dar es Salaam, miji ya Kibaha na Bagamoyo mkoani, hadi kufikia
mwezi Juni 2016.
Katika
utekelezaji wa agizo hilo DAWASCO iko katika utekelezaji wa Maagizo ya
serikali ya kuhakikisha wananchi waishio katika Jiji la Dar s salaam,
Miji ya Kibaha na Bagamoyo Mkoani Pwani wanaunganishiwa Maji ifikapo
Julai 2016. Katika kutekeleza agizo hilo Dawasco imejipanga katika awamu
kuu NNE (4)
1.
Awamu ya kwanza itawahusu wateja wote walioko katika maeneo ambayo kwa
sasa yanapata maji na kuna miundo mbinu ya mabomba karibu.
2.
Awamu ya Pili itahusu maeneo ambayo yamepitiwa na mabomba makubwa ya
Maji jirani lakini wananchi wake hawana maji kwa sababu ya kukosekana
kwa miundo mbinu ya usambazaji.
3.
Awamu ya Tatu itahusisha maeneo yote yaliyopitiwa na mradi maarufu wa
Mabomba ya Kichina, Maunganisho katika awamu hii yataanza baada ya
kukamilika kwa Miradi ya Ruvu Chini na Ruvu Juu,
4.
Awamu ya Nne itaanza katika maeneo yote ambayo kwa sasa hakuna miundo
mbinu ya Maji na yako mbali kutoka katika mabomba makubwa
Gharama
ya kuunganishiwa huduma ya Majisafi ni Tsh 200,000 kwa wateja wadogo
(Domestic Customers)na Tsh 400,000 kwa wateja wakubwa (Corporate
Customers)
No comments:
Post a Comment