EWURA Yasema Nchi Inaakiba Ya Kutosha Ya Mafuta - LEKULE BLOG

Breaking

Header Ads

Sunday, 10 January 2016

EWURA Yasema Nchi Inaakiba Ya Kutosha Ya Mafuta

SERIKALI imewatoa hofu Watanzania kuhusu uwepo wa mafuta ya kutosha nchini baada ya kuamriwa kurudishwa kwa meli iliyokuwa imebeba shehena ya mafuta yenye kiwango kisichofaa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa huduma za Nishati na Maji (Ewura), Felix Ngamlagosi, alisema kuna akiba ya kutosha na hivyo watanzania wasiwe na hofu kwani kurudishwa kwa meli hiyo hakuna athari zozote kwa upande wa mafuta.
Alisema ipo akiba ya mafuta ya kutosha na kwamba Ewaura inaendelea kupokea shehena za mafuta kama kawaida na kwa kiasi kitakachoendelea kutosheleza mahitaji ya nchi. 
Aliongeza kuwa hadi kufikia Januari 8 mwaka huu kulikuwa na kiasi cha lita 255,052,370 kwa ajili ya soko la ndani, lita milioni 143.547 kwa ajili ya soko la nje, na lita milioni 27.875 za dizeli kwa ajili ya matumizi ya migodi.
“Wananchi wasiwe na hofu. Kilichofanywa na TBS hakijaathiri chochote. Kwa takwimu hizi ni dhahiri kuwa nchi ina akiba ya kutosha ya mafuta na bado tunaendelea kupokea,” alisema Ngamlagosi.
Aidha alisema katika kipindi cha Desemba 2015 na Januari 2016 bei za mafuta katika soko la dunia zimeendelea kushuka na kwamba bei za mafuta katika soko la Tanzania zilifuata mwenendo wa bei za mafuta katika soko la dunia.

Katika kudhibiti ubora wa mafuta, alisema Ewura inaendelea kuchukua sampuli kwenye vituo vya mafuta, maghala makubwa ya kuhifadhi mafuta na magari ya kubeba mafuta, lengo likiwa ni kukagua ubora wa mafuta.
Post a Comment