Waziri Mkuu Aridhishwa na Huduma za Matibabu Wanazopewa Wazee - LEKULE

Breaking

8 Jan 2016

Waziri Mkuu Aridhishwa na Huduma za Matibabu Wanazopewa Wazee


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kuwa amefarijika kuona wazee wanapata huduma za matibabu bure na kwa utaratibu mzuri katika hospitali ya Mkoa wa Ruvuma.

Akizungumza na madaktari, wauguzi na watumishi wengine wa hospitali hiyo wiki hii, alivyokuwa kwenye ziara mkoani humo, Waziri Mkuu  Majaliwa amesema  utaratibu wa kutenga chumba maalum chenye madaktari wawili  mahsusi kwa ajili ya kuwahudumia wazee  unaotekelezwa hospitalini hapo  umeondoa  adha kubwa  kwa wazee kusubiri matibabu kwa muda mrefu  jambo  ambalo ni kero kwao.

Amesema  kuwa hospitali ya Mkoa wa Ruvuma  imethibitisha kwamba    agizo la Serikali la kutaka  hospitali zote za Serikali  nchini ziwe na dirisha maalum kwa ajili ya wazee na  watibiwe bure linatekelezeka na kuzitaka hospitali zote nchini kuiga mfano huo.

 “Hospitali zote nchini  ziige  mfano wa hospitali ya  Mkoa wa Ruvuma kwa  kuwaheshimu wazee wanaokwenda kutibiwa katika hospitali hizo kwa kuanzisha dirisha maalum kwa ajili yao kama agizo la serikali linavyosema na wasitozwe malipo ya aina yoyote” alisema Waziri Mkuu.

 Aidha, ameongeza kwa kusema kuwa hata wanapokwenda kuchukuwa dawa uwekwe utaratibu wa kuwapa kipaumbele kwa kuwahudumia kwanza ili wasisubiri kwa muda mrefu. Na kusisitiza kuwa kibali maalum kinachowapa fursa wazee kutibiwa bure hospitalini hapo kindelee kutolewa na kiheshimiwe.

Awali, alitembelea chumba maalum cha wazee  ambapo Waziri Mkuu alipata fursa ya kuzungumza na Bibi Antonia Moyo  ambaye alisema hajawahi kutozwa fedha wala kukaripiwa  wakati wote alipofika hospitalini hapo kwa ajili ya matibabu kupitia dirisha la wazee.

Waziri Mkuu Majaliwa, pia ametembelea wodi mbalimbali, chumba cha upasuaji pamoja na duka la dawa kwa wagonjwa wanaotumia huduma za Bima ya Afy

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P 3021,11410 DAR ES SALAAM

ALHAMISI 7, 2016.

No comments: