WAKUU
wa idara tisa katika Halmashauri ya manispaa ya Kigoma Ujiji mkoani
Kigoma, wamesimamishwa kazi kupisha uchunguzi wa tuhuma za ufisadi
kwenye matumizi ya fedha na uuzwaji wa majengo ya halmashauri hiyo.
Inaelezwa
kuwa kusimamishwa kwa watumishi hao kunafuatia maagizo ya Waziri Mkuu,
Kassim Majaliwa kwa Katibu Tawala wa mkoa huu, John Ndunguru kuunda tume
na kufanya uchunguzi kuhusu uuzwaji wa jengo la KIGODECO na MIBOS
kutokana na mchakato wa uuzwaji kukiuka sheria ya manunuzi.
Akitoa
taarifa kwa waandishi wa habari hivi karibuni, Ndunguru aliwataja wakuu
hao wa Idara kuwa ni pamoja na Ofisa Mipango, Wilfred Mwita, Emanuel
Mkwe ambaye ni Mwanasheria, pamoja na Mhandisi wa Ujenzi wa Manispaa
hiyo, Boniface William.
Wengine
ni Ofisa Biashara, Mussa Igugu, Mkaguzi wa Ndani, Ellymboto Zakharia,
Ofisa Misitu wa manispaa hiyo ambaye wakati wa uuzwaji huo alikuwa
akikaimu nafasi ya Ofisa Mipango, Leonald Nzilailunde, Ofisa Ugavi,
Shida Thadei, Ofisa Mapato, Bawili Mkoko na Fundi Mkuu wa Magari, Omari
Rwabibi.
Akizungumzia
hatua dhidi ya Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Boniface Nyambele, Katibu
Tawala huyo alisema Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(Tamisemi) ndiye mwenye jukumu la kumchukulia hatua za kinidhamu na
kuzitangaza.
“Watumishi
hawa wamesimamishwa kupisha uchunguzi na baada ya uchunguzi kukamilika
hatua zaidi zitachukuliwa iwapo itabainika kuhusika kwao, lakini pia
Tamisemi italeta timu yao ya uchunguzi kuchunguza suala hilo na
imeagizwa kufanya uchunguzi maalumu na CAG katika miradi mbalimbali
inayotuhumiwa,” Alisema Ndunguru.
Miongoni
mwa mambo yaliyofanya Waziri Mkuu kutoa agizo hilo ni pamoja na
mchakato wa uuzwaji wa jengo la KIGODECO ambapo taratibu za kisheria
zilikiukwa huku mnunuzi wa jengo hilo ambaye ni benki ya CRDB ikijipa
kazi ya kulifanyia uthamini na kutoa bei elekezi ambayo jengo linapaswa
kuuzwa.
Aidha,
inaelezwa kuwa ilitathminiwa kuwa jengo hilo linapaswa kuuzwa kwa Sh
milioni 450, lakini Halmashauri iliamua kuliuza kwa Sh milioni 370.
Ndunguru
alisema pia kuwa, kabla ya kununua jengo hilo, CRDB ilipangisha jengo
hilo na baadaye Halmashauri ikachukua mkopo kwenye benki hiyo kwa
mkataba wa kuifanya benki hiyo itumie jengo hilo kwa miaka mitatu katika
mkataba ambao unaeleza kuwa pindi Hamashauri itakapotaka kuvunja
mkataba itabidi ilipe tozo kwa benki.
Alisema,
Halmashauri hiyo iliamua kuliuza jengo hilo kwa benki ya CRDB na kwamba
benki hiyo ilikata deni lake la Sh milioni 50 pamoja na tozo ya Sh
milioni 117 kufuatia kuvunjwa kwa mkataba wa ukodishaji ili liuzwe.
Katika
tuhuma nyingine, Manispaa ya Kigoma Ujiji inatuhumiwa kuuza jengo la
MIBOS kwa Sh milioni 50 bila kulifanyia tathmini huku uthamini ukionesha
kuwa bei ya soko kwa sasa kwa jengo hilo ni Sh milioni 72.
Pia,
manispaa hiyo inakabiliwa na tuhuma za kubadilisha matumizi ya Sh
milioni 809 za miradi ya mifugo, uboreshaji wa miundombinu ya mji wa
Kigoma Ujiji na uboreshaji wa miundombinu ya shule za msingi na
sekondari katika manispaa hiyo bila kibali.
Hata
hivyo, inaelezwa kuwa kikao cha fedha na uongozi kilikataa kuidhinisha
fedha hizo kwa ajili ya ujenzi wa maabara za shule za sekondari na
badala yake ikaidhinisha matumizi ya Sh milioni 70.
Taarifa
hiyo inasema, licha ya kamati ya fedha na uongozi kukataa kuidhinisha
matumizi ya fedha hizo, hakukuwa na taarifa iliyotolewa Tamisemi kuhusu
jambo hilo na uchunguzi uliofanywa na tume hiyo umebainisha kuwepo kwa
shaka katika matumizi ya fedha za kugharimia ujenzi huo wa maabara.
No comments:
Post a Comment