Askofu Pengo: "Muhimbili Panatosha na Nimeridhika Na Huduma Za Hapa, Sioni Haja ya Kwenda Kutibiwa Nje" - LEKULE BLOG

Breaking

Header Ads

Friday, 8 January 2016

Askofu Pengo: "Muhimbili Panatosha na Nimeridhika Na Huduma Za Hapa, Sioni Haja ya Kwenda Kutibiwa Nje"


Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Katoliki  la Dar es salaam,Muadhama, Kardinali  Pengo amesema kwamba ameridhishwa na huduma za afya zinazotolewa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili(MNH), hivyo itakuwa ni vigumu kwa Serikali kumshawishi kwenda kutibiwa nje ya nchi.

Kauli hiyo ilitolewa jana  na Askofu Pengo ambaye amelezwa katika  Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete iliyopo katika hospitali ya  MNH  jijini Dar es Salaam kuanzia  Januari Mosi, mwaka  2016 hadi sasa mara baada ya kuzungumza na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu  ambaye alimtembelea  jana  mchana  ili kuweza kufahamu maendeleo ya afya yake.

“Ninapenda kutoa taarifa kwa umma wa Watanzania  na kuwaondoa hofu kuwa hali ya Baba Askofu Pengo imeimarika na  anaendelea vizuri, hajawekewa oxygen wala hajalazwa katika wodi ya uangalizi maalum(ICU) na ameridhika na huduma zinazotolewa,.

“Ameridhika  na  huduma zinazotolewa za moyo, itakuwa ni vigumu sisi kama Serikali kumshawishi kwenda kutibiwa nje ya nchi, ” alisema  Waziri huyo.

Aidha Waziri Ummy alitembelea sehemu ya ICU, katika taasisi hiyo, ambapo alisema operesheni ambazo ni ngumu zinafanyika, katika opresheni za moyo kiwango cha kimataifa ni asilimia 6, wakati Tanzania imefikia kiwango cha asilimia 4, hivyo tunafanya vizuri.

Aliongeza kwamba hatua hiyo inapunguza idadi ya wagonjwa wanaokwenda kutibiwa nje ya nchi, pia aliwataka hata wagonjwa kutoka taasisi binafsi kwenda kutibiwa katika taasisi hiyo.

Kwa upande wake Mkuu wa taasisi hiyo, Profesa Mohamed Janabi alisema  Baba Askofu huyo ameridhika na matibabu aliyoyapata ambayo yanaweza kufanyika Tanzania, hivyo changamoto iliyopo kwa Serikali kupitia wizara hiyo ni kuiwezesha taasisi hiyo kibajeti ili kuwezesha wagonjwa anagalau 50 kati ya 300 ambao wako kwenye orodha  ya kupatiwa huduma.

Aliongeza kwamba Baba Askofu huyo, ataruhusiwa siku za karibuni, baada ya hali kuendelea vizuri.

 Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu (kulia) akiwa na Mkuu wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete iliyopo katika Hospitali ya  Taifa ya Muhimbili (MNH)  jijini Dar es Salaam Profesa Mohamed Janabi alipomtembelea   jana,Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Katoliki  la Dar es salaam,Muadhama, Kardinali  Pengo. 
Post a Comment