Waziri
wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amewaagiza watendaji wa
Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma
za Nishati na Maji (EWURA) kutafuta uwezekano wa kufupisha muda wa
kushughulikia maombi ya wawekezaji wanaotaka kuwekeza katika uzalishaji
umeme.
Alitoa
agizo hilo hivi karibuni jijini Dar es Salaam alipokutana na Viongozi
wa mashirika hayo kujadili masuala mbalimbali yanayohusu uwekezaji
katika sekta ya nishati.
Profesa
Muhongo alisema utaratibu unaotumika sasa katika kushughulikia maombi
ya wawekezaji katika sekta ya nishati unachukua muda mrefu hali
inayosababisha usumbufu kwa wawekezaji.
“Utaratibu
wa kutumia muda mrefu kiasi cha miezi sita au zaidi kushughulikia
maombi ya wawekezaji haufai. Sisemi mvunje sheria kwa kutofuata
utaratibu au kutumia njia za mkato, lakini inabidi mtafute namna ya
kushughulikia maombi husika kwa haraka,” alifafanua Waziri Muhongo.
Ili
kuhakikisha sheria inazingatiwa wakati wa kutekeleza agizo hilo, Waziri
aliwataka Watendaji hao pamoja na mambo mengine kufuatilia ili kujua
Sheria ya Manunuzi Serikalini inatoa mwongozo upi katika suala husika.
Waziri
Muhongo alisema Serikali imedhamiria kuhakikisha nchi inafikia uchumi
wa kipato cha kati ifikapo mwaka 2025 na hivyo ni lazima nishati ya
umeme ambayo ni moja ya vigezo muhimu izalishwe kwa kiasi kikubwa
kufikia megawati 10,000 ili kutimiza malengo hayo.
Alisema,
Wizara yake imejipanga kuhakikisha umeme wa kutosha, wa uhakika na bei
nafuu unazalishwa kutoka vyanzo mbalimbali vilivyopo nchini ambavyo ni
gesi asilia, maji, jotoardhi, upepo, jua, mawimbi ya bahari na makaa ya
mawe.
Tangu
alipoapishwa na kuanza kazi rasmi hapo Desemba 12, 2015, Waziri Muhongo
amefanya ziara kadhaa kujionea na kushughulikia changamoto mbalimbali
zinazoikabili sekta ya nishati hususan masuala ya upatikanaji wa umeme
wa uhakika na wa bei nafuu.
No comments:
Post a Comment