Watu 26 wauawa katika shambulio Ouagadougou - LEKULE

Breaking

17 Jan 2016

Watu 26 wauawa katika shambulio Ouagadougou

Askari wa Ufaransa wakipiga kambi karibu na hoteli ya Splendid, mjini Ouagadougou, Januari 16, 2016.
Askari wa Ufaransa wakipiga kambi karibu na hoteli ya Splendid, mjini Ouagadougou, Januari 16, 2016
Na RFI
Watu wasiopungua 26, ikiwa ni pamoja na wageni wengi, wameuawa katika shambulio la wanamgambo wa kiislamu lililoendeshwa Ijumaa hii dhidi ya hoteli na mgahawa mjini Ouagadougou.
Upande wa wauaji, wanajihadi wanne wameuawa. Operesheni ya kuwasaka wahalifu ilioendeshwa na vikosi vya usalama Jumamosi hii katika mji mkuu wa Burkina Faso haikufaulu kuwapata wauaji walio mafichoni.
Saa chache kabla ya shambulio hilo la kigaidi kumalizika katikati mwa mji wa Ouagadougou, idadi ya vifo bado haijawa sahihi. Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufaransa (Quai d'Orsay) imetangaza Jumamosi hii mchana kwamba raia wawili wa Ufaransa wameuawa na mwengine mmoja amejeruhiwa. Kitengo cha kupambana na ugaidi cha Ofisi ya mashitaka mjini Paris kimeanzisha uchunguzi.
Operesheni ilioendeshwa Jumamosi mchana imepelekea kuwaokoa watu 126, ikiwa ni pamoja na wengine 150 waliojeruhiwa. Akitembelea katika hoteli ya Splendid, Rais wa Burkina Faso Roch Marc Kaboré amesema watu wasiopungua 23 kutoka mataifa mbalimbali wameuawa. Kwa sasa, Waziri wa Mawasiliano wa Burkina Faso, Rémi Dandjinou, amesema kuwa ripoti rasmi ya mwisho inaeleza watu wasiopungua 26 wameuawa.
Kwenye akaunti yake ya Twitter, Gilles Thibault, Balozi wa Ufaransa, amesema kuwa shambulio hilo limesababisha vifo vya watu 2, na nchi wanakotoka hazijafahamika, akibaini kwamba"watu 150 kutoka mataifa 18 waliokolewa na kwa sasa wanapatishiwa huduma za mwanzo. "
Washambuliaji ni akina nani?
Upande wa wauaji, wanajihadi wanne wameuawa katika hoteli ya Splendid na vikosi vya usalama vya Burkina Faso, vikisaidiwa na vikosi vya Ufaransa na Marekani. "Washambuliaji waliouawa ni pamoja na Mwarabu mmoja na Waafrika wawili weusi", amesema Waziri wa Usalama, Simon Compaoré.
Kwa mujibu wa afisa wa polisi nchini Burkina Faso, mwanamgambo wa nne wa kiislamu ameuawa katika hoteli ya Yibi, ambapo alikua alikimbilia baada ya operesheni ya vikosi vya usalama dhidi ya hoteli ya Splendid. Afisa huyo amesema kuwa wanawake wawili walikuwa miongoni mwa wanamgambo hao.
Lakini taarifa hii haijathibitishwa. "Hatuna taarifa yoyote ya wanawake hao, lakini operesheni bado inaendelea", Alpha Barry, Waziri wa Mambo ya Nje wa Burkina Faso ameiambia mchana RFI.
Kulingana na taarifa za RFI, kundi hili la magaidi limekua likiundwa na watu zaidi ya kumi na tano. Ikimaanisha kwamba wengi wao hawajapatikana.

Shambulio hili limedaiwa kutekelezwa na AQMi, kundi lenye mafungamano na Al-Qaeda, kwa niaba ya kundi la al-Mourabitoune.

No comments: