Naibu
Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani (katikati) akizungumza
na wananchi katika kijiji cha Chimwenga wilaya ya Mbeya vijijini
ambapo Naibu Waziri aliwaeleza wananchi hao umuhimu wa kukaa mbali na
vyanzo vya maji ili kutoviharibu na kusababisha upungufu wa maji
unaopelekea bwawa la uzalishaji umeme la Mtera kukauka.
Naibu
Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani (kushoto) na Mkuu wa
wilaya ya Mbeya Nyirembe Munasa wakiwa katika kijiji cha Makwenji wilaya
ya Mbeya vijijini ambapo Naibu Waziri alikagua vyanzo vinavyotiririsha
maji kwenye mito inayopeleka maji katika bwawa la uzalishaji umeme la
Mtera.
Naibu
Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani (mwenye tai nyekundu)
akikagua moja ya miradi mikubwa ya kilimo cha umwagiliaji inayofanyika
katika wilaya ya Mbarali mkoa wa Mbeya ambayo hutumia maji kutoka katika
mapitio yanayopeleka maji katika bwawa la uzalishaji umeme la Mtera.
Naibu
Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani (mbele) akiwa katika
ukaguzi wa vyanzo vinavyotiririsha maji kwenye mito inayopeleka maji
katika bwawa la uzalishaji umeme la Mtera.Nyuma yake ni Kamishna
Msaidizi wa Nishati anayeshughulikia Maendeleo ya Nishati, James
Andilile.
Baadhi
ya wananchi katika wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya wakimwangalia Naibu
Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani (hayupo pichani)
wakati akikagua mapitio ya maji yanayoelekea katika bwawa la uzalishaji
umeme la Mtera.
Na Teresia Mhagama, Mbeya
Wananchi
wanaozunguka vyanzo vinavyotiririsha maji katika mito inayomwaga maji
kwenye bwawa la uzalishaji umeme la Mtera wametakiwa kuhakikisha kuwa
hawafanyi shughuli zozote za kiuchumi au ujenzi wa makazi ndani ya eneo
la mita 60 kutoka kilipo chanzo cha maji.
Hayo
yameelezwa na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani
wakati alipofanya ziara ya kukagua vyanzo vya maji katika wilaya ya
Mbeya vijijini ambavyo vinachangia upatikani wa maji katika bwawa la
Mtera lenye uwezo wa kuzalisha umeme wa kiasi cha megawati 80.
Licha
ya kuagiza kwamba eneo hilo la mita 60 lisifanyike shughuli zozote
zikiwemo za kilimo na ufugaji, Dkt. Kalemani pia aliiagiza Ofisi ya Mkuu
wa wilaya ya Mbeya kufanya tathmin ili kufahamu idadi ya watu wanaoishi
ndani ya eneo hilo katika vyanzo vyote vya maji ili kuona uwezekano wa
kuwahamisha kwa kufuata utaratibu.
Vilevile
Naibu Waziri aliagiza kuwa vyanzo vyote vya maji viwekewe alama ili
kuepusha wananchi kuingilia maeneo hayo na kufanya shughuli
zitakazoathiri upatikanaji wa maji katka mabwawa ya uzalishaji umeme.
" Zuio
hili ni lazima liende sambamba na suala la Halmashauri zetu kuwa na
mipango ya matumizi ya ardhi, bila hivyo hakutakuwa na matumizi endelevu
ya maji na matokeo ni kama haya ambapo wananchi wanaamua kufanya
shughuli kama za kilimo na ufugaji katika vyanzo vya maji na kusababisha
uharibifu," alisema Dkt. Kalemani.
Dkt.
Kalemani pia aliwaagiza watendaji wa Wilaya na Halmashauri zinazozunguka
vyanzo hivyo, kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa matumizi bora
ya maji katika vyanzo na mapitio ya maji yanayopeleka maji katika bwawa
la mtera ambalo sasa limesimamisha uzalishaji wa umeme kutokana na
upungufu wa maji.
Kuhusu
suala la wananchi wenye vibali kutumia maji hayo kwa shughuli
mbalimbali ikiwemo kilimo, Naibu Waziri alisema kuwa wananchi hao
wanapaswa kutumia maji kwa kiwango walichoruhusiwa tu na si vinginevyo
na yeyote atakayebainika kuharibu chanzo cha maji atachukuliwa hatua
kali za kisheria.
"
Wadau mbalimbali wanaosimamia sheria zinazoongoza sekta ya maji ikiwemo
Wizara zinazohusika na maji, Kilimo, Mifugo, Nishati na Madini na
Mamlaka za Mabonde, lazima wahakikishe kuwa wanasimamia sheria hizo
kikamilifu, kila mtu atimize wajibu wake na kama kuna yeyote ataonekana
anafanya hujuma atachukuliwa hatua kali," alisema Dkt. Kalemani.
Naibu
Waziri pia alitoa wito kwa wananchi kuvilinda vyanzo vya maji nchini
kwa kushirikiana na serikali katika ngazi za vijiji, wilaya na mikoa ili
kuhakikisha kuwa uharibifu wa vyanzo vya maji nchini unafikia tamati.
No comments:
Post a Comment